Tanzania:maktaba kubwa zaidi Afrika Mashariki imezinduliwa!
Sr. Angela Rwezaula – Vatican
Maktaba ya kisasa inayotumia mfumo wa teknolojia ya mawasiliano ambayo inaelezwa ndio kubwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki pamoja kusini mwa Afrika, imefunguliwa tarehe 27 Novemba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa maktaba hiyo iliyojengwa kwa ufadhili wa nchi ya China, Rais Magufuli amesema maktaba hiyo ni nyumba ya maarifa hivyo itasaidia kuinua kiwango cha elimu pamoja na maendeleo katika sekta nyingine kupitia utafiti.
Hata hivyo mapema, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye ameelezea uwezo wa maktaba hiyo katika kuwahudumia wanafunzi. Na pia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamekiri kufurahishwa na ujenzi wa maktaba hiyo.
Kwa mujibu wa balozi wa China nchini Tanzania, Daktari Wang Ke, amethibitisha kuwa nchi yake imetumia kiasi cha dola za kimarekani million 41 kujenga maktaba hiyo ya kisasa pamoja na kituo cha kufundishia lugha ya kichina. Ujenzi wa maktaba hiyo ni mradi wa pili mkubwa kufadhiliwa na China nchini Tanzania, baada ya ule wa reli ya Tazara, kutoka Tanzania hadi Zambia, iliofunguliwa kunako mwaka 1975.
Katika tukio lisilotegemewa, Rais Magufuli alimpongeza hata Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye alikuwa ni mmoja wa wageni katika hafla hiyo kwa kumtaja kuwa ni mwanasiasa aliyekomaa lakini akitoa onyo kwa wanasiasa wanaovunja sheria. Pamoja na hayo hata Bwana Lowasa ameipongeza juhudi zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na serikali kwa ujumla katika kuimarisha elimu.