Cerca

Vatican News
Serikali ya Tanzania imepania kutafuta soko la uhakika wa zao la korosho Serikali ya Tanzania imepania kutafuta soko la uhakika wa zao la korosho 

Serikali ya Tanzania kutafuta soko la uhakika zao la korosho

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa korosho nchini Tanzania kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kupata masoko ya uhakika ya zao hilo.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Serikali ya Tanzania imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kupata masoko ya uhakika ya zao hilo. Kauli hiyo imetolewa Alhamisi, Novemba 8, 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu bei ya korosho ambayo imeshuka katika msimu wa mwaka huu hadi kusababisha wakulima kugomea baadhi ya minada, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali. “Tunaendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa ili tujue ni nani atanunua korosho na kwa kiasi gani, hivyo tunawaomba wakulima waendelee kuwa watulivu, Serikali inajitahidi kuhakikisha zao hilo linatafutiwa masoko. Korosho zitanunuliwa tu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya ujenzi wa viwanda vya mbolea, ambapo inatoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vikiwemo vya pembejeo. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Neema Mgaya aliyetakakujua Serikali ina mpango gani katika kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya mbolea ili wakulima waweze kuipata kwa gharama nafuu. Amesema viwanda vya mbolea vilivyopo nchini ni vichache na havitoshelezi mahitaji, hivyo kwa sasa kuna utaratibu wa kujenga viwanda vingine viwili kimoja kitajengwa Kilwa mkoani Lindi na kingine kitajengwa Mtwara. Kukamilika kwa viwanda hivyo kutaongeza uzalishaji wa mbolea na kupunguza uagizaji kutoka nje ya nchi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amefafanua kuhusu suala la wakulima wa mahindi kukosa masoko, ambapo amesema ruhusa ya kuuza mahindi nje ya nchi ilishatolewa. Amesema jambo hilo lilitolewa ufafanuzi na Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba. Waziri Mkuu amesema licha ya kuwepo kwa kibali cha kuuza mahindi nje ya nchi ni lazima Serikali itambue kiasi gani kinachotolewa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, hivyo muuzaji anatakiwa awasisilishe taarifa zake kwa wakuu wa wilaya. “Tunahitaji kuwa na takwimu za mauzo na bei ili kujua kiasi kilichouzwa pamoja na kiasi cha fedha kilichopatika.”

Kuhusu upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu ikiwemo mbolea, Waziri Mkuu amesema suala hilo linaratibiwa vizuri na Wizara ya Kilimo na tayari asilimia 60 ya mahitaji ya pembejeo tayari imeshaingia nchini, hivyo Serikali itahakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Lucia Mlowe, Mbunge wa Viti Maalumu aliyehoji Serikali inatoa tamko gani kuhusu tatizo kubwa la wakulima wa mahindi kukosa masoko ya uhakika.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 28 Oktoba, 2018, Rais John Pombe Magufuli alikutana na wanunuzi wa zao la korosho na kutoa msimamo wa Serikali kuhusu bei ya zao la korosho kufuatia kuwepo kwa mvutano wa bei ya zao hilo kati ya wanunuzi na wakulima. Rais Magufuli bila kupindisha maneno aliungana na wakuliwa nchini Tanzania kukataa bei zilizotolewa na wanunuzi katika mnada uliofanyika hivi karibuni ambapo kampuni za ununuzi wa korosho zilitangaza kununua korosho kwa bei kati ya shilingi 1, 900/ na shilingi 2, 717 kwa kilo ikiwa imeshuka kutoka zaidi ya shilingi 3, 600 ya msimu uliopita. Msimamo wa Serikali ni bei ya kilo moja ya korosho isipungue shilingi 3, 000/. Lengo ni kusaidia pia wakulima kupata faida na hatimaye, kuboresha hali ya maisha yao.

Rais Magufuli katika mkutano huu, aliondoa utozaji ushuru wa mara mbili; wanunuzi kununua magunia yao wenyewe na kwamba, amekubali wafanyabiashara hawa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirishia korosho kwenye masoko ya kimataifa! Amewataka wafanyabishara hao kuzingatia masharti ya usafirishaji, viwango vya uzito na kamwe wasithubutu kutorosha korosho nje ya nchi! Rais Magufuli amewataka wanunuzi hao kuwekeza katika viwanda vya kubangulia korosho ama kuwahamasisha washirika wao kwenda kuwekeza katika viwanda hivyo nchini Tanzania na kwamba, Serikali ya awamu ya tano itaunga mkono juhudi hizi ikiwa ni pamoja na kuweka vivutio vya kodi.

08 November 2018, 11:48