Tafuta

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa: Tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa: Tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho 

Serikali ya Tanzania yawasha moto kwa wanunuzi wa korosho!

Serikali ya Tanzania yatoa siku nne kwa wanunuzi wa korosho: yawataka waandike barua wakionesha tani wanazohitaji na lini watazichukua; yasema zaidi ya hapo haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dar es Salaam.

Serikali ya Tanzania imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho wawe wamepeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua. “Hivyo wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi saa 24.”

Hayo yamesemwa Ijumaa, Novemba 9, 2018, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma. Baada ya kupita siku hizo Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima kitu ambacho imesema haitakubaliana nacho. “Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua kwani ofisi yangu ipo wazi saa 24 wana nafasi ya kuleta barua wakati wowote wakionesha nia yao na kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo Serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.”

Waziri Mkuu amesema kwenye msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu, walishuhudia kusuasua kwa minada, ambapo Serikali ilikutana na wanunuzi wa korosho katika kikao kilichoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambapo walikubaliana kununua kwa bei inayoanzia sh 3,000 na kuendelea. “Mjadala ulikuwa wa wazi na wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo ilikuwa inaanzia sh. 3,000, hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi katika minada imeendelea kusuasua na hata tani zilizokuwa zikinunuliwa zilikuwa kidogo sana. Sisi tunaiona hali hii kama mgomo baridi ambao si sawa sawa sana kwani malengo yetu sisi na sekta binafsi ni kumfanya mkulima apate bei nzuri. Hali hii haifurahishi kwa sababu Serikali imedhamiria kuboresha mazao yanayolimwa na wakulima kwa kuwasaidia kuanzia katika hatua za utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na masoko ili waweze kunufaika na kilimo na kupata tija katika mazao hayo.”

Waziri Mkuu amesema baada ya kugundua bei imekuwa tatizo Serikali ilifanya jitihada za kupeleka wataalamu wake katika masoko makuu duniani na kupata bei halisi ambayo bado inatosha kumlipa mkulima sh 3,000. Hatua hiyo imekuja baada ya zao la korosho kuendelea kununuliwa kwa bei ya chini na idadi ya wanunuzi kuwa ya chini licha ya uzalishaji wa mwaka huu kuwa mdogo ukilinganisha na msimu wa mwaka 2017. Amesema msimu wa mwaka jana uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 300,000 na mwaka huu zinatarajiwa tani zaidi ya 200,000 hivyo wafanyabiashara wanao uwezo kununua korosho zilizopo. Hata hivyo Serikali imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini Tanzania kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo.

09 November 2018, 10:40