Msitu wa Sahel karibu na Kayes nchini Mali Msitu wa Sahel karibu na Kayes nchini Mali 

Sahel:mabadiliko ya tabianchi yanahatarisha amani!

Rais wa Baraza la Kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa (Ecosoc) anasema kuwa ukosefu wa usalama umesambaa kufuatia: mzozo wa makundi yaliyojihami, ukatili na operesheni za kijeshi, madhila kwa binadamu na mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kila uchao katika ukanda wote wa Sahel

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa mataifa (ECOSOC) kwa ushirikiano na kamisheni ya kujenga amani tarehe 12 Novemba limefanya kikao cha kujadili mabadiliko ya tabianchi na uhusiano wake katika kukwamisha juhudi za ujenzi wa amani  na kudumisha amani katika Ukanda wa Sahel. Akihutubia kikao hicho rais wa Ecosoc, Inga Rhonda King amesema ukanda wa Sahel unakabiliwa na changamoto zinazochukua sura mbalimbali kwani,“ukosefu wa usalama umesambaa kufuatia mzozo wa makundi yaliyojihami, ukatili na operesheni za kijeshi, madhila kwa binadamu na mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kila uchao. Watu milioni 4.9 wamefurushwa makwao mwaka huu huku watu milioni 24 wakihitaji msaada wa kibindamu katika ukanda mzima.”

Watu milioni 4.9 wamefurushwa makwao mwaka huu huku na  watu milioni 24 wakihitaji msaada wa kibindamu ukanda wa Sahel

Bi. Rhonda amesema ukanda huo ni moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi kimazingira duniani huku viwango vya joto vikitabiriwa kuwa mara 1.5 zaidi ya viwango vya dunia nzima. Ameongeza kuwa, “ukanda huo unategemea kwa kiasi kikubwa kilimo cha mvua na hukabiliwa mara kwa mara ni kiangazi na mafuriko na kusababisha athari kubwa kwa usalama wa chakula. Tunapozungumza watu takriban milioni 33 hawana uhakika wa chakula wakati watoto milioni 4.7 walio na umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri.”

Mabadiliko ya tabianchi katika ukanda wa Sahel yanaweza kuchochea hatari

Rais huyo wa ECOSOC ameongeza kuwa wakati idadi ya watu ikitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2.8 kila mwaka katika mazingira ambamo rasilimali zinapungua, ikiwemo ardhi na raslimali maji, mabadiliko ya tabianchi katika ukanda wa Sahel yanaweza kuchochea hatari: “hatari ambazo zinaweza kuzua mizozo na kulazimisha watu kuhama, changamoto ambazo zinakumba ukanda huo” amaethibitisha. Hali hii inahitaji kushughulikiwa haraka.” Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi katika kuchochea mizozo wiki hii Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “ili kupata amani na maendeleo endelevu na kutoka katika uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu na kupunguza na kumaliza mahitaji ya kibindamu, ni lazima tutatue miziz ya mizozo na majanga. Hii inapatikana katika ubaguzi, ukiukwaji wa haki za bindamu, utawala dhaifu, mizozo na athari za mabadiliko ya tabianchi’.

Ion Jinga- Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri dunia nzima

Kwa upande wake Mwenyekiti ya kamisheni ya kujenga amani, Ion Jinga amesema, “mabadiliko ya tabianchi yanaathiri dunia nzima na kusababisha, majangwa, ukame, mafuriko na ukosefu wa chakula na vyote vikihatarisha vizazi na maendeleo.” Ameongeza kusema kuwa ECOSOC kwa ushirikiano na kamisheni yake zinaweza kusaidia miradi hasa katika kuambatanisha sera, kujenga ushirikiano na kuwekeza rasilimali na kuchagiza umiliki wa kitaifa katika miradi inayowekezwa. Mkutano huo pia ulijadili namna Umoja wa Mataifa utakavyoimarisha mifumo kwa ajili ya kusaidia nchi za ukanda wa Sahel katika kuimarisha ustahimili wake dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

 

 

 

14 November 2018, 13:34