Tafuta

Viashiria vya joto duniani ni pamoja na kiwango cha asidi baharini na kuendelea kuyeyuka kwa barafu huko ncha ya kaskazini mwa dunia kwa mujibu ripoti ya shirika la hali ya hewa (WMO) Viashiria vya joto duniani ni pamoja na kiwango cha asidi baharini na kuendelea kuyeyuka kwa barafu huko ncha ya kaskazini mwa dunia kwa mujibu ripoti ya shirika la hali ya hewa (WMO) 

Ripoti mpya inaonesha kuwa joto linazidi kuongeza mwaka 2018!

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya tabianchi duniani iliyotolewa tarehe 29 Novemba na shirika la hali ya hewa duniani, WMO, ikionyesha kuwa miaka 20 yenye joto zaidi ilirekodiwa miaka 22 iliyopita, ambapo iliyoshika viwango vya juu zaidi ni miaka minne iliyopita

Sr. Angela Rwezaula Vatican

Hali ya joto duniani imeendelea kuongezeka mwaka 2018 huku wastani wa kiwango cha joto duniani kote ikitarajiwa kushika nafasi ya nne na kuvunja rekodi. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya hali ya tabianchi duniani iliyotolewa tarehe 29 Novemba 2018 na shirika la hali ya hewa duniani (WMO), ikionyesha kuwa miaka 20 yenye joto zaidi ilirekodiwa miaka 22 iliyopita, ambapo iliyoshika viwango vya juu zaidi ni miaka minne iliyopita.

Viashiria vya mabadiliko ya tabianchi

Katika Ripoti hiyo imeweka bayana viashiria vya mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ongezeko la joto kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari, joto na kiwango cha asidi baharini na kuendelea kuyeyuka kwa mabarafu huko ncha ya kaskazini mwa dunia. Taarifa ndani  ya ripoti hiyo zinatokana na michango kutoka kwa wadau wa Umoja wa Mataifa wakielezea kwa kina madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Ripoti inaonyesha kuwa katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka huu wa 2018, wastani wa kiwango cha joto duniani ulikuwa karibu nyuzi joto 1, kiwango ambacho kilikuwepo kati ya zama za mapinduzi ya viwanda (1850-1900).

Naye Petteri Taalas, Katibu Mkuu wa WMO amesema:“Bado hatuko kwenye mwelekeo wa kufikia malengo tuliyojiwekea ya kupunguza kiwango cha joto,” na kwamba: “mkusanyiko wa hewa chafuzi kwa mara nyingine tena unazidi kuongezeka na kufikia viwango vya juu na iwapo mwelekeo huu utaendelea tunaweza kushuhudia ongezeko la joto hadi kati ya nyuzijoto 3-5 ifikapo  mwishoni mwa karne hii.” Katibu Mkuu huyo wa WMO amesema ni vyema kusisitiza kwa mara nyingine tena kuwa, “sisi ni kizazi cha kwanza cha kuelewa vyema mabadiliko ya tabianchi na ni kizazi cha mwisho kuweza kuchukua hatua yoyote dhidi yake.” Shirika la hali ya hewa duniani WMO hata hivyo limegundua hewa chafu ya ukaa katika anga imeongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka milioni 3 na kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani WHO, zinathibitisha kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa mijini kote duniani wanavuta hewa chafu.

Mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi

Ripoti hii ya WMO ni ushahidi zaidi wa kisayansi ambao unatolewa kuelekea mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP24 utakaofanyika mwezi ujao huko Katowice, Poland kuanzia tarehe 2 hadi 14 Desemba 2018. Lengo la mkutano huo ni kupitisha miongozo ya utekelezaji wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015 unaolenga kuhakikisha kuwa ongezeko la kiwango cha joto duniani hakivuki nyuzi joto 1.5.

Hata hivyp Bwana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres  akiwa mjini New York Marekani kabla ya kusafiri kwenda Argentina mahali panapofanyika mkutano wa nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi (G20),  amewaambia wanahabari kuwa changamoto kubwa hivi sasa ni ukosefu wa kuaminiana duniani. Amesema, “dunia yetu inakabiliana na mgogoro wa kukosa imani. Wale ambao wameachwa nyuma na utandawazi wanakosa kuziamini serikali na taasisi. Kukosekana kwa usawa kumeenea na kuongezeka hususani ndani ya mataifa.” Zaidi ya hayo amesema migogoro ya biashara inaongezeka na hali ya mvutano wa kijiografia inaongeza shinikizo zaidi kwa uchumi wa dunia. Ni muhimu tushughulikie sababu za msingi na kufanya kazi pamoja ili kukuza utandawazi ulio wa haki”

Malengo ya maendeleo endelevu SDGs ni chachu muhimu kwa utandawazi ulio wa haki

Bwana Guterres amesisitiza kuwa malengo ya maendeleo endelevu SDGs ni chachu muhimu kwa utandawazi ulio wa haki pia yeye anayo matumaini kuwa viongozi wa G20 watakubaliana naye. Katibu Mkuu amesema, “wengine wanaweza kusema huwezi kupambana na mabadiliko ya tabianchi na ukawa na uchumi mzuri. Ninakataa kwa nguvu zote. Kimsingi kinyume chake ndicho sahihi. Gharama za kijamii, kiuchumi na kimazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ni ndogo kulinganisha na kuchukua hatua sasa.”

Aidha amesisitiza kuwa, kushindwa kuchukua hatua kunamaanisha majanga zaidi na dharura na uchafuzi wa hewa ambavyo amesema vinaweza kuugharimu uchumi wa dunia kufikia dola za kimarekani trilioni 21 kufikia mwaka 2050. Bwana Guterres ameongeza kusema kuwa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi ni fursa na teknolojia iko upande wetu. Na biasahara ya kijani ni biashara nzuri. Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “wanachama wa G20 wanawajibika zaidi ya robo tatu ya uchafuzi wa hali ya hewa na pia wakati huo huo wanachama wa G20 wana nguvu ya kuibadili hali hiyo. Pia wana rasilimali za kutoa misaada ya kifedha inaayotakiwa kuirejeshaa hali kaatika ubora wake.”

Mkutano wa G20 huko Argentina

Hata hivyo Bwana Guterres mara baada ya mkutano wa G20 huko Argentina ataelekea Poland katika mkutano 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP24, amesema anaenda na ujumbe huo huo katika mikutano yote miwili kuwa kuzuia hewa chafu ya ukaa ni jambo linalowezekana lakini “tunahitaji nia kubwa na tuko katika mbio kwa ajili ya mstakabali wa maisha yetu yajayo na kwamba ni mbio ambazo tunaziwezekana na tunatakiwa kushinda".

30 November 2018, 15:57