Tafuta

Vatican News
Mkutano Kimataifa kuhusu Matumizi Endelevu ya Bahari umefanyika mjini Nairobi Kenya kuanzia tarehe 26-28 Novemba. Kuna haja ya kuwa na maeneo yaliyotengwa ya baharini Mkutano Kimataifa kuhusu Matumizi Endelevu ya Bahari umefanyika mjini Nairobi Kenya kuanzia tarehe 26-28 Novemba. Kuna haja ya kuwa na maeneo yaliyotengwa ya baharini  

Kenya:Mkutano wa Kimataifa kuhusu Matumizi Endelevu ya Bahari!

Mkutano Kimataifa kuhusu Matumizi Endelevu ya Bahari umefanyika mjini Nairobi Kenya kuanzia tarehe 26-28 Novemba.Washiriki wa mkutano huo wameangazia pamoja mambo mengi na umuhimu wa kuwa na maeneo yaliyotengwa ya baharini kwa ajili ya matumizi endelevu ya bahari

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi endelevu ya bahari kwa ajili ya ukuaji wa uchumi umemalizika tarehe 28 Novemba 2018 huko Nairobi, Kenya ambapo wadau wamekubaliana juu ya namna ya kushirikiana ili kupata faida za rasilimali zitokanazo na bahari. Mkutano huo ulioanza Jumatatu 26 Novemba kwa ufunguzi rasmi na  Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, ambaye  alihutubia wajumbe kutoka mataifa 180. Katika hotuba yake Rais Kenyatta alisema, zaidi ya watu bilioni 2.5 wanakabiliwa na changamoto ya mazingira machafu duniani kote.Pia Rais Kenyatta amesema kuna faida nyingi zitokanazo na miji iliyokaribu na bahari, kama vile usafirishaji wa mizigo kutoka taifa moja hadi lingine kupitia bandari za mataifa hayo na hivyo ameyahimiza mataifa yenye bahari kuitunza vyema raslimali hiyo.

Kuendeleza ukuaji wa miundo msingi ya kisasa bila kuharibu mazingira

 Pamoja na mengi aliyoyoweza kuhutubia  Rais Kenyatta, amehimiza ulimwengu kuweka mikakati ya kuzuia uchafuzi wa mazingira, sambamba na kuweka mipango thabiti ya kuendeleza ukuaji wa miji kupitia miundo msingi ya kisasa na hasa bila kuharibu mazingira. Na washiriki wa mkutano huo kwa pamoja wamezungumza mambo mengi na mengine umuhimu kama vile ku wa na maeneo yaliyotengwa ya baharini kwa ajili ya matumizi endelevu ya bahari.

Kati ya viongozi walioshiriki mkutano huo ni marais wa Ushelisheli, Namibia, Uganda, Jamhuri ya Kongo, Somalia na Fiji. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Daktari Ali Mohamed Shein naye  aliudhuria ambapo amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari John Pombe Magufuli. Inakadiriwa zaidi ya wajumbe 15,000 wameshiriki katika mkutano huo mjini Nairobi ambao ni wa kwanza wa aina yake duniani.

Afrika kubarikiwa sana kuwa na maji kwa wingi

Akihojiwa na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa,  (UNIC) kilichoko  mjini Nairobi, kando ya mkutano huo, Mwakilishi Mkazi wa FAO nchini Kenya, Gabriel Rugalema amesema nchi nyingi za Afrika hususan za Afrika Mashariki zinazingirwa na rasilimali ya maji, ambayo inaweza kusaidia katika kukabiliana na njaa, kutokomeza umaskini na kubuni ajira kwa wakazi kwani kwa upande wake anasema: “Upande huu wetu wa Afrika tumejaliwa sana maji kwa wingi. Je tunayatumiajie? kwa sababu tukiimarisha utumiaji tutaweza kuongeza ajira na kuongeza uzalishaji wa viwanda, ukiangalia bahari ya hindi Msumbiji, Tanzania, Kenya, Somalia zina sehemu ya bahari, tunaweza kuweka utalii viwanda vya kutoa maji chumvi na kuwekeza katika sekta ya uvuvi.”

Pamoja na hayo yote Bwana Rugalema ametoa wito kwa serikali zote kufanya kazi na sekta binafsi ili kuweza kuvuna uchumi wa maji kwa sababu anasema: “Kwa sasa ukiangalia sekta ya bahari, rasilimali zinachukuliwa na watu wengine ambapo meli zinaingia kwenye baharí zetu na kuchukua rasilimali ambapo wanatajirika na sisi tupo hapa.” Kutokana na mantiki hiyo, mwakilishi wa FAO hiyo amesema wakati ni sasa kutumia rasilimali zitokanazo na bahari kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwenye jamii.

Mkutano wa uchumi wa bahari ni wa kwanza kufanyika nchini Kenya

Mkutano huo wa uchumi wa bahari ni wa kwanza kabisa wa aina yake nchini Kenya na ambapo umeeandaliwa na Kenya, Canada na Japan ukichochewa na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015 na kongamano la Umoja wa Mataifa la bahari la 2017 la kuchagiza hatua hizo!

 

28 November 2018, 10:39