Tafuta

Serikali ya Tanzania yaridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa reli ya kisasa, SGR. Serikali ya Tanzania yaridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa reli ya kisasa, SGR. 

Kasi na viwango vya ujenzi wa reli ya kisasa Tanzania vinaridhisha!

“Nimeridhishwa na viwango na maendeleo ya ujenzi kwa sehemu ulivyofikia pamoja na ushiriki wa Watanzania wengi katika mradi huu, tunataka muendelee kujenga kwa kasi hii.” Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona malengo ya Rais Dkt. John Magufuli ya kutaka kuona SGR inakamilika na kuanza kutumika nchini yanatimia.

Na OFISI YA WAZIRI MKUU, - Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa mfumo wa reli ya kisasa (SGR) inayojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi. Amesema kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa km. 300 ambacho kilitakiwa kukamilika Julai 2019, wataalamu wamesema watakamilisha Aprili,2019. Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumamosi, Novemba 3, 2018 alipotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia eneo la Shaurimoyo Dar esSalaam hadi Soga, Pwani.

“Nimeridhishwa na viwango na maendeleo ya ujenzi kwa sehemu ulivyofikia pamoja na ushiriki wa Watanzania wengi katika mradi huu, tunataka muendelee kujenga kwa kasi hii.” Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona malengo ya Rais Dkt. John Magufuli ya kutaka kuona SGR inakamilika na kuanza kutumika nchini yanatimia. Kuhusu suala la ajira, Waziri Mkuu amesema amefarijika kusikia asilimia 96 ya watu walioajiriwa katika mradi huo ni Watanzania, amewataka wawe mabalozi wazuri. “Watanzania mnaofanya kazi katika mradi huu hakikisheni mnawajibika kwa kufanyakazi kwa bidii, uaminifu na muwe mabalozi wazuri ili wengine waweze wapate ajira.”

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya mradi huo wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora unagharimu sh. trilioni 7.1. Alisema mradi wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa km 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza umegawanyika katika vipande vitano, kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu km 300 na kitagharimu sh. trilioni 2.7. “Kipande kingine ni kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa km. 422 ambacho kitagharimu sh. trilioni 4.4, Makutupora hadi Tabora km. 376.5, Tabora hadi Isaka km 162.5 na Isaka hadi Mwanza km. 311.25.”

Mkurugenzi huyo alisema kukamilika kwa reli hiyo ya kisasa kutachochea mipango ya Serikali katika kutekeleza sera ya viwanda na kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Pia reli hiyo itachochea mapinduzi ya kiuchumi kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususan kwa nchi zisizopakana na bahari kwani watasafirisha mizigo yao kwa haraka na uhakika. Akizungumzia mradi huo kwa ujumla, Kadogosa alisema maendeleo ya mradi huo ni asilimia 32 kwa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro na asilimia 3. 31 kwa kipande cha Morogoro-Makutupora.

05 November 2018, 14:11