Tafuta

Serikali ya Tanzania inataka kuona vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu vikizingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa! Serikali ya Tanzania inataka kuona vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu vikizingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa! 

Serikali ya Tanzania yasema, inataka: ubora na viwango vya elimu kitaifa na kimataifa!

Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo kwa vyuo vikuu vyote: vya binafsi na vya umma ili viendelee kutoa elimu ya juu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kukidhi matakwa na ushindani kwenye soko la kitaifa na kimataifa. Suala hilo ni muhimu likapewa uzito unaostahili kwani wahitimu hao wakitoka vyuoni wanakwenda kutoa huduma katika jamii.

Na OFISI YA WAZIRI MKUU. – Dodoma, Tanzania.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo kwa vyuo vikuu vyote nchini, vya binafsi na vya umma ili viendelee kutoa elimu ya juu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kukidhi matakwa na ushindani kwenye soko la kitaifa na kimataifa.  Amesema suala hilo ni muhimu likapewa uzito unaostahili kwani wahitimu hao wakitoka vyuoni wanakwenda kutoa huduma katika jamii ya Watanzania na pia ya kimataifa, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa ikazingatia ubora na viwango vinavyostahiki.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Ijumaa, Novemba 23,2018 kwenye mahafali ya tisa ya chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania Kampasi ya Chifu Mazengo, Dodoma yaliyofanyika kwenye ukumbi wa CCM. Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, inatambua na kuthamini mchango wa Sekta Binafsi hususan wa vyuo vikuu binafsi kama Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania, katika maendeleo ya elimu ya juu.  “Serikali inatambua mchango wa vyuo hivyo katika kupanua fursa kwa Watanzania wengi kupata elimu ya juu, ambapo hadi sasa udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwenye vyuo vikuu binafsi nchini ni takriban asilimia 25 ya wanafunzi wote.”

Amesema Serikali inatambua mchango wa chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania katika kutayarisha watalaamu wa fani mbalimbali. Aidha, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, chuo hicho kimetoa wahitimu zaidi ya 10,000. Amesema kati ya wahitimu hao wapo Wafamasia, Wauguzi, Walimu wa Sayansi, Walimu wa Sanaa, Wataalamu wa Maabara, na Wasimamizi na Waendeshaji wa fani mbalimbali kama Utawala, Masoko na Wahasibu, mchango ambao unahitajika kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa uchumi wa Taifa katika nyanja tajwa.

Waziri Mkuu amesema baadhi ya wahitimu watapata ajira lakini si kila mhitimu atapata fursa ya kuajiriwa, hivyo Serikali itaendelea kuunga mkono azma yao kama chuo kikuu ya kutoa wahitimu wenye tabia, utashi na uwezo wa kutengeneza kazi na siyo watafuta kazi tu. Akizungumzia kuhusu changamoto zinazokabili sekta ya elimu ya juu, amesema baadhi ya changamoto zinafanana katika vyuo vikuu vyote nchini na pia zipo changamoto zinazokabili vyuo vikuu binafsi na wakati mwingine zipo changamoto zinazohusu chuo kikuu kimoja kimoja. 

Amesema moja ya changamoto kubwa katika elimu ya Juu ni uhaba wa Wahadhiri wenye sifa stahiki ili kuendana na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na vyuo vyao. “Nafahamu jitihada ambazo vyuo vikuu binafsi vinafanya katika kuendeleza Rasilimali Watu wao na hasa katika eneo la taaluma ili viwe na Wahadhiri na Maprofesa wa kutosha.”  Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito vyuo vingine binafsi nchini viwekeze katika eneo la kuendeleza Rasilimali Watu kwa bidii zaidi na kwa upande wa Serikali, ipo mikakati mbali mbali ya kuajiri lakini pia kusomesha wale waliopo kazini ili kufikia viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Waziri Mkuu amesema changamoto nyingine inayovikabili vyuo vikuu ni miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kama vile mabweni na nyumba za watumishi, hivyo kusababisha baadhi ya vyuo kushindwa kukidhi matakwa ya ithibati zao na kuzuiwa kufanya udahili au kufungiwa kabisa. “Ni kweli tunahitaji Watanzania wengi wapate elimu ya juu kwenye vyuo vyetu vikuu. Hata ninyi wanafunzi, mngependa kupata elimu iliyo bora itakayoweza kuwasaidia maishani na itakayowakomboa kifikra, itakayowapa ujuzi na maarifa ya kupambana na changamoto za maendeleo. Kila mmoja anataka elimu bora na si bora elimu.” 

Waziri Mkuu amesema kuwa dhamira hiyo ndiyo inayoifanya Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu kuhakikisha kuwa vyuo vyote visivyokidhi matakwa ya ithibati yao haviendelei kutoa mafunzo ya aina yoyote. “Nitoe rai kwa vyuo vikuu vyote vizingatie matakwa ya ithibati zao ili viweze kutoa elimu iliyo bora itakayokidhi matamanio ya Watanzania na ushindani wa soko la ndani na nje.” Kuhusu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania ambacho kimeomba kuruhusiwa kufanya udahili baada ya kufungiwa, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kujiridhisha iwapo chuo hicho kimekidhi vigezo kabla ya kukipa kibali cha kudahili wanafunzi wapya.

23 November 2018, 16:08