Tafuta

Vatican News
Mafuriko kwenye bonde la Msimbazi jijini Dar es salaam Tanzania, mapema mwaka huu yalisababisha vifo vya watu 15 Mafuriko kwenye bonde la Msimbazi jijini Dar es salaam Tanzania, mapema mwaka huu yalisababisha vifo vya watu 15  (ANSA)

Bonde la Msimbazi Tanzania kutafutiwa ufumbuzi!

Mradi wa Benki ya Dunia unaweza kuleta matumaini kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kuboresha bonde la Msimbazi Dar es Salaam kwa mijibu wa warsha zinazofanyika kutafuta ufumbuzi wake. Na wakati huo huo Ripoti mpya ya Benki ya Dunia inasema kuna Gharama kubwa ya nyumba katika Muungano wa Ulaya (EU)

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Taarifa inasema kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wanatekeleza  mradi wa kupunguza madhara ya mafuriko kwenye bonde la Msimbazi jijini Dar es salaam, mafuriko ambayo mapema mwaka huu yalisababisha vifo vya watu 15. Katika Jiji la Dar es salaam, nchini Tanzania ambako takwimu zinaonyesha kuwa kutokana na fursa za uchumi zilizopo, kila siku watu 1000 huingia katika  jiji hilo.

Uchafuzi wa mazingira ikiwemo mto Msimbazi

Licha ya fursa hizo, uchafuzi wa mazingira ikiwemo mto Msimbazi unatishia mazingira ya jiji hilo kutokana na takataka zinazotupwa hovyo na kutelekezwa na hatimaye mvua zinaponyesha huleta madhara na  hata vifo kama anavyoelezea  mkazi mmoja wa bonde la Msimbazi kwamba mafuriko yanapotokea yanawaathiri  kwa njia nyingi. Hawali ya yote ni  afya zao kwa njia ya  maji hayo machafu. Pia yanaharibu nyumba zao na watoto hawawezi kwenda shule kwa sababu vitabu vyao na sare za shule vimelowana.

Vikao vya kubaini mustakhabali huo vimefanyika kwa zaidi ya miezi tisa

Kutokana Mradi wa Benki ya Dunia unaweza kuleta matumaini kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania ili  kuboresha bonde hilo la Msimbazi ambapo warsha zinafanyika zikileta wadau wote wakiwemo viongozi wa serikali, wataalam wa kiufundi na wananchi kwa lengo la kuamua mustakabali wa bonde hilo. Daktari Venance Makota kutoka Baraza la Mazingira la Taifa, NEMC amenukuliwa akifafanua juu ya matokeo ya warsha hiyo.  “Hadi sasa kuna mapendekezo matatu. Kuna kisiwa cha hazina, kuna bustani oevu na eneo litakaloendelezwa mbele ya mto. Hatimaye tutakuwa na chaguo moja ambayo itaboresha eneo hilo.” Vikao vya kubaini mustakhabali huo vimefanyika kwa zaidi ya miezi tisa na uendelezaji wa mradi wa bonde la mto Msimbazi ni sehemu ya miradi mitatu ya Benki ya Dunia ya kujenga mnepo kwa miji nchini Tanzania.

Gharama ya juu ya nyumba EU yakatisha tamaa vijana

Na wakati huo huo Ripoti mpya ya Benki ya Dunia inasema Gharama ya juu ya nyumba katika Muungano wa Ulaya EU yakatisha tamaa vijana. Hatma ya mamilioni ya vijana kupata ajira kwenye miji mikuu ya Muungano wa Ulaya, (EU) iko mashakani kutokana na bei za nyumba kuwa ni za juu kupita kiasi sambamba na kodi ya pango. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki ya Dunia iliyotolewa mapema wiki hii ikipatiwa jina Kuishi na Kuondoka: Nyumba, Mwenendo na Ustawi kwenye EU ambapo inaelezwa kuwa bei za nyumba zinapandishwa na kuwa za juu kuliko inavyotakiwa.

Utafiti uliohusisha raia katika nchi 28 wanachama wa  Muungano wa Ulaya (EU)

Ripoti hii inatokana na utafiti uliohusisha raia katika nchi 28 wanachama wa  Muungano wa Ulaya EU ambapo inasema kwa wakazi wa miji mikuu kwenye nchi 26 kati ya 28 kupata makazi mazuri katika bei nafuu si rahisi. “Nyumba kwenye maeneo ya miji mikuu ya Muungano wa nchi za Ulaya  (EU) hazishikiki kwa wakazi wengi kwa sababu ujenzi mpya wa majengo hauendani na mahitaji,”. Hayo yamesemwa na  Gabriela Inchauste, mchumi kiongozi wa Benki ya Dunia na mwandishi mwenza wa ripoti hiyo. Akiendelea amesema kuwa,“kwa kuwa kiwango kikubwa cha hisa za nyumba kinamilikiwa na kizazi cha zamani, hii inakuwa imewaengua vijana ambao wanashindwa kuishi kwenye maeneo yanayoweza kuwapatia kazi zenye tija na fursa za juu zaidi za ajira kama kwenye miji mikuu.”

Mapendekezo matatu yametolewa

Mapendekezo matatu yametolewa na ripoti hiyo ili kurekebisha hali hiyo ya sasa ambapo pendekezo la kwanza kwa watunga sera wa Muungani wa nchi za Ulaya EU wanasema ni “kubaini maeneo ya ardhi ya umma ambayo hayatumiki na kuyapatia vibali yaweze kuendelezwa kuwa makazi ya umma.” Ripoti pia inataka kuwekeza katika miradi mipya isiyohusisha ubomoaji wa majengo au miradi ya awali sambamba na kuboresha miundombinu ya usafiri inayounganisha maeneo ya mijini na viungani na mwisho ni kuandaa maeneo ya umma yaliyo wazi ambayo yanaweka bayana masuala ya bei za nyumba ili kuweka ushindani sawia wa bei kati ya maeneo.

Kuweka sera bora za kuhakikisha ujenzi wa makazi

Kwa mujibu wa ripoti hiyo gharama kubwa za makazi ni kwenye nchi za Ugiriki, Bulgaria, Denmark, Ujerumani, Romania na Uingereza wakati huo huo hali ya mambo ni shwari huko Malta, Cyprus, Finland, Ireland, Estonia na Ufaransa. Naye Arup Banerji, ambaye ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za EU amesema suala la makazi linaonekana kuwa ni suala la kitaifa hivi sasa kwa mataifa mengi ya muungano huo wa Ulaya na watu wengi wanaingia hofu. “Kwa kuweka sera bora za kuhakikisha kuwa ujenzi wa makazi unaongezeka kadri bei za nyumba zinavyopanda, Muungano wa Ulaya EU inaweza kusaidia vijana kumudu bei za nyumba, hali ambayo itakuwa na athari chanya kwenye maisha yao kijamii na utendaji wao wa kazi utakuwa wa tija”.

13 November 2018, 14:43