Tafuta

Urithi Festal ni chachu ya kukuza, kulinda, kuimrisha na kutangaza utamaduni wa malikale za Tanzania na hivyo kuzigeuza kuwa ni zao la utaii. Urithi Festal ni chachu ya kukuza, kulinda, kuimrisha na kutangaza utamaduni wa malikale za Tanzania na hivyo kuzigeuza kuwa ni zao la utaii.  

Urithi Festival ni chachu ya kukuza, kulinda na kutangaza utamaduni na malikale za Tanzania

Waziri Mkuu wa Tanzania amesema Urithi Festival ni chachu ya kukuza, kulinda, kuimarisha na kutangaza utamaduni na malikale zetu na kuvigeuza kuwa zao la utalii. Tamasha hili litatuweka pamoja zaidi na kudumisha umoja, utaifa na uzalendo kwa nchi yetu.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Arusha.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa muda wa miezi miwili na nusu kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezoiwe imekamilisha mchakato wa Tanzania kuwa na vazi la Taifa. Amesema Watanzania bado hawajaunganishwa kwa kuwa na vazi la Taifa, ambalo mchakato wake umeendeshwa kwa miaka mingi na wizara hiyo bila ya kujulikana wamefikia wapi. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumamosi, Oktoba 13, 2018 wakati akifunga tamasha za Urithi Festival, lililofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

“Ifikapo Desemba 30,2018 tuwe tumeanza kupata sura ya vazi la Taifa ili wadau walijadili na waamue ni vazi gani la Mtanzania ambalo litawakilisha Taifa kama nchi nyingine walivyomudu kuwa na vazi la Taifa.” Aliongeza kuwa ili kufikia azma Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iandae tamasha maalumu kwa ajili ya kuonesha aina tofauti za nguo ili kupata vazi la Taifa.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza waandaaji wa tamasha la Urithi Festival wahakikishe kuanzia mwakani kuwe na uratibu wa pamoja baina ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara ili tamasha lifunguliwe upande mmoja na kufungwa upande mwingine wa Muungano. Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wametoa fursa kwa walio Zanzibar kujifunza na kuona utamaduni wa bara na wa bara kujifunza ya Zanzibar, hivyo itasaidia kudumisha  umoja wa kitaifa. “Hakikisheni ikiwa tamasha litafunguliwa Tanzania Bara basi lifungwe Zanzibar ili liweze kuwa na tija’’.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, inaitaka Serikali kuongeza msukumo katika kukuza utalii na kutangaza vivutio vyetu vya utalii vikiwemo utamaduni na malikale.  “Mtakubaliana nami kwamba tunapaswa kuendeleza mila, tamaduni na desturi zetu kwani ndizo kichocheo muhimu cha uzalendo tulionao hususan katika suala zima la maadili. Vilevile, utamaduni ni zao la uhakika kwenye sekta ya utalii na ukarimu.” 

Amesema thamani ya utamaduni mara nyingi imekuwa ikionekana kwenye sekta nyingine kama elimu, afya, michezo, kilimo, viwanda na maendeleo ya jamii, ambapo alitoa rai kwaWizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wadau wote wa utalii hususani Sekta binafsi na wananchi kwa ujumla washirikiane katika kulinda, kutunza, kutangaza na kuendeleza vivutio vya utalii nchini  “Lengo la Serikali ni kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,102,026 mwaka 2015 hadi 2,000,000 ifikapo mwaka 2020. Lengo hili linatekelezwa kwa kuwezesha sekta binafsi kuwekeza kwenye huduma ya miundombinu ya utalii na kuendelea kutangaza utalii ili kuwafikia watalii wengi zaidi.”  

Amesema Urithi Festival ni chachu ya kukuza, kulinda, kuimarisha na kutangaza utamaduni na malikale zetu na kuvigeuza kuwa zao la utalii. Tamasha hili litatuweka pamoja zaidi na kudumisha umoja, utaifa na uzalendo kwa nchi yetu. Aidha, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuikumbusha Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mkoa wa Dodoma kuanza maandalizi mara moja ya kutekeleza agizo la Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan la kutenga eneo mahususi ambalo litatumika kwa ajili ya Tamasha la Urithi kila mwaka kitaifa Mkoani Dodoma. 

 “Napenda kutumia fursa hii na hasa nikizingatia maagizo ya Makamu wa Rais kuwapa changamoto Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa utalii kuhakikisha kuwa kuanzia mwaka kesho (2019) tamasha hili linatambulika Kimataifa na kuwa moja ya kichocheo kikuu cha kukuza pato la Taifa litokanalo na utalii“ Amesema wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo Septemba 15, 2018 jijini Dodoma, Makamu wa Rais, Mama Samia aliagiza kila Mkoa kutenga bajeti kwa ajili ya Tamasha la Urithi. “Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha tena Wakuu wa Mikoa kuanza maandalizi mapema.“ “Tamasha la Urithi sio tu linaenzi utamaduni na mila zetu, lakini ndio njia bora zaidi ya kurithisha vizazi vijavyo mila, desturi, tamaduni na historia yetu. Kwani yeyote yule ambaye haenzi utamaduni wake basi huyo ni mtumwa“

13 October 2018, 15:29