Kinamama wanastahili kusubiri kwa mwaka mmoja baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine kwa mujibu wa watafiti Kinamama wanastahili kusubiri kwa mwaka mmoja baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine kwa mujibu wa watafiti 

Utafiti mpya kwa wamama:Subiri angalau mwaka kabla ya ujauzito mwingine!

Utafiti mpya kuhusu muda wa kupata ujauzito tena, umebaini kwamba, kupata ujauzito chini ya miezi 12 baada ya kujifungua ni hatari kwa wanawake wa miaka yote. Ni hatari zaidi kwa mama aliye na umri wa zaidi ya miaka 35, na vile vile ni hatari kwa mtoto mchanga ikiwa mama ana miaka kati ya 20 na 34

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kinamama wanastahili kusubiri kwa mwaka mmoja baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine ili kupunguza hatari ya kumpoteza mama na mtoto, ni uthibitisho wa utafiti mpya. Watafiti hao hata hivyo wanasema hawastahili kusubiri kwa muda wa miezi 18 kama ilivyopendekezwa katika kanuni iliyopo sasa ya shirika la Afya Duniani WHO.

Wakifafanua juu ya suala hili watafiti  wanasema, muda mfupi kati ya mimba moja hadi nyingine humweka mama katika hatari ya kuzaa mtoto ambaye hajatimiza wakati wa kuzaliwa,mtoto mdogo au kifo chake. Watafiti hao wanatumaini matokeo ya uchunguzi huu utawapatia hakikisho wanawake hasa waliyo na umri mkubwa. Mmoja wa watafiti hao Dr Wendy Norman amesema kuwa hizi ni habari njem kwa wanawake waliyo na zaidiya miaka 35 ambao wana mpango wa  familia zao. “Wanawake waliyo na umri mkubwa kwa mara ya kwanza watapata mwongozo wa uhakika kuhusiana na suala la kupanga uzazi wa watoto wao”.

Utafiti uliohusisha kuzaliwa kwa karibu watoto 150,000 nchini Canada,  na ambao ulifanywa na vyuo vikuu vya British Columbia (UBC) na Harvard Marekani umebaini kuwa miezi 12 hadi 18 ni muda mwafaka kwa mwanamke kujipumzisha baada ya kujifungua kabla ya kupata tena ujauzito. Mwongozo wa sasa wa shirika la Afya Duniani unapendekeza muda wa usiyopungua miezi 18 hadi 24.

Utafiti huo pia ulibaini kwamba, Kupata ujauzito chini ya miezi 12 baada ya kujifungua ni hatari kwa wanawake wa miaka yote. Ni hatari zaidi kwa mama aliye na umri wa zaidi ya miaka 35, na vile vile ni hatari kwa mtoto mchanga ikiwa mama ana miaka kati ya miaka 20 na 34. Wanawake waliyo na miaka zaidi ya 35 waliyo pata ujauzito miezi sita baada ya ujauzito mwingine walikua katika hatari ya kupoteza maisha kwa 1.2% , na  (visa 12 vimeripotiwa kwa kila mimba 1000). Kusubiri kwa miezi 18 kabla ya kupata ujauzito mwingine kunapunguza hatari hiyo kwa 0.5% (visa vitano kwa kila mimba 1,000).

Wanawake wadogo waliopata ujauzito miezi sita baada ya kujifungua walikuwa katika hatari ya kupata uchungu wa uzazi kabla ya muda wa kujifungua kwa asilimia 8.5%. Hali hii ingeweza kupunguzwa  hadi 3.7% ikiwa wanawake hao wangelisubiri kwa miezi 18 kati ya ujauzito mmoja hadi mwingine. Utafiti huo uliangazia zaidi wanawake nchini Canada, kwa njia hiyo  haijabainika ikiwa matokeo yake yatakuwa sawa sawa kote duniani, japokuwa ni muhimu kutambua suala hili.

Mtafiti  mmoja Dr. Sonia Hernandez-Diaz anasema matokeo yaliashiria hali tofauti kwa wnawake wa miaka tofauti. “Ujauzito wa haraka haraka huenda ukaashiria kutozingatia uzazi wa mpango, kwa baadhi ya wanawake wa umri mdogo.

Naye Mandy Forrester, kutoka taasisi ya wakunga ya Royal College, anasema utafiti huu, “ni muhimu kwa sababu unaimarisha tafiti nyingine kuhusiana na suala la muda wa kupata ujauzito mwingine baada ya kujifungua”. Yote hayo kwa maana nyingine ni kuwa mwanamke atajiamulia mwenyewe anataka kuchukua muda gani baada ya kujifungua kabla ya kupata ujauzito mwingine, na kuongeza kusema, “jambo la msingi ni kwa wanawake wote  duniani, kuwa na ufahamu wa kujihami nao kuhusiana na suala hili ili wafanya maamuzi yenye busara”.

Ujauzito hubadilisha ubongo wa mwanamke: Hata hivyo Wataalamu wa afya wako tayari kumsaidia mwanamke kufanya maamuzi yake, kulingana na kile kilicho sawa kwa upande wake. Mtafiti akiendelea na ufafanuzi, ameongezea kusema kuwa, “wanawake wanastahili kupata ushauri kuhusiana na mbinu tofauti za kupanga uzazi ili waweze kupanga vema familia zao ikiwa wanaazimia kufanya hivyo na  huduma za kitaalamu zinastahili kufikia wanawake wote”.

31 October 2018, 11:06