Tafuta

Siku ya Umoja wa Mataifa, tarehe 24 Oktoba 2018. Siku ya Umoja wa Mataifa, tarehe 24 Oktoba 2018. 

Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa 2018 na changamoto zake!

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2018 anasema, Katiba ya Umoja wa Mataifa inafumbata: matarajio, matumaini na ndoto za watu wengi.

Na Mwandishi maalum Ofisi ya Waziri Mkuu & Padre Mjigwa R. – Vatican.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1971, lilipitisha azimio kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 24 Oktoba, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ziaadhimishe Siku ya Umoja wa Mataifa, ili kukumbuka, ile siku nchi wanachama walipopitisha Katiba ya Umoja wa Mataifa ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto pevu kama vile: athari za mabadiliko ya tabianchi, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji pamoja na ukosefu wa usawa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2018 anasema, Katiba ya Umoja wa Mataifa inafumbata: matarajio, matumaini na ndoto za watu wengi. Kila siku wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanajitahidi kuhakikisha kwamba, Katiba hii inamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, licha ya vizingiti na vikwazo wanavyokumbana navyo kila siku bila ya kukata tamaa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anakaza kusema, umaskini wa kukithiri umepungua, lakini usawa kati ya watu umetoweka; Umoja wa Mataifa unazidi kusonga mbele ili kuwajengea watu: matumaini, kwa kuwapatia fursa na kuwarejeshea amani. Kuna athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, lakini Umoja wa Mataifa bado haujakata tamaa, kwani hii ndiyo njia muafaa ya kupambana na changamoto hizi.

Kuna uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia, lakini Umoja wa Mataifa una amini kwamba, utunzaji wa haki msingi za binadamu ni msingi wa amani duniani ingawa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kushamiri sana na kwamba, watu wanateseka! Kumbe, watu wanahitaji amani na utulivu. Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa yasaidie kukoleza tena dhamana na wajibu wa Umoja wa Mataifa ili kurejesha matumaini; kuwaponya waliovunjika moyo na kutokomeza makovu ya uchafuzi wa mazingira, kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kulinda na kudumisha utu wa binadamu wote!

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kwamba nchini Tanzania hakuna ubanaji wa uhuru wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali. Amesema jambo hilo linadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152, ambavyo kati yake ni vituo vitatu tu ndivyo vinavyomilikiwa na Serikali. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, Jumatano, Oktoba 24, 2018) katika maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. “Tunapenda kuwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania inaongozwa na katiba na sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa kujieleza na kupata habari,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba mwananchi yeyote atakayeenda kinyume na sheria, Serikali itamuwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Amesema Serikali imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na ule wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Sambamba na kusimamia haki hizo, Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake katika kuiwezesha jamii kuishi salama kwa amani na utulivu kwa kuzingatia sheria za nchi. Amesema kukuza, kuimarisha na kulinda haki za binadamu ni wajibu wa Serikali na kwa kuzingatia umuhimu huo mwaka 1984 iliingiza sheria ya haki za binadamu katika katiba.

 Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa zoezi la kuwarejesha wakimbizi wa Burundi nchini kwao lilikuwa ni la hiari na limetekelezwa baada ya hali ya amani kurejea. Amesema hakuna sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi ambao kwa hiari yao wameamua kurejea nchini kwao ili wakaendelee na shughuli za kulijenga Taifa lao. “Nasisitiza kuwa zoezi hili ni la hiari. Tangu mwezi Septemba mwaka jana, Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi na UNHCR imekuwa ikiwarejesha wakimbizi hao kwao.” Amesema zoezi hilo limekuwa likifanyika kwa kuzingatia usalama na utu wa wakimbizi hao. Wakimbizi 52, 283 wa Burundi wamerejea nchini kwao kati ya 81,281 waliokwisha jiandikisha. Waziri Mkuu ameyasema hayo baada Serikali kupokea shutuma katika siku za hivi karibuni kutoka kwa baadhi ya jamuiya ya kimataifa kuhusu uendeshaji wa zoezi hilo.

Hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na washirika wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa mujibu wa mkataba wa UN wa mwaka 1967 wa kuwahudumia wakimbizi ili kufanikisha zoezi hilo la kuwarejesha makwao kwa hiari na kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu. Maadhimisho hayo ya siku ya Umoja wa Mataifa ambao umetimiza miaka 73 tangu uanzishwe yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro. Wengine ni Mratibu wa Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bw. Alvaro Rodrigues pamoja na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania.

Na Habari nyingine kutoka Jijini Mwanza zinasema, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema ushirikiano mzuri baina ya taasisi mbalimbali za dini nchini Tanzania na Serikali ni jambo la muhimu katika kuboresha na kuimarisha amani. Ameyasema hayo Jumatatu, Oktoba 22, 2018 alipowasili jijini Mwanza akiwa njiani kwenda mkoani Simiyu ambako, Jumanne, Oktoba 23, 2018 amefungua maonesho ya wajasiriamali. Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Waziri Mkuu amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wa Serikali na wa dini mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mkakati wa viongozi wa dini wa kuunda kamati za amani nchini ambapo walianzia kwenye ngazi ya mkoa na sasa wamefikia katika kata. “Viongozi wa dini mnadhamana kubwa katika kulifanya  Taifa liendelee kudumisha amani, utulivu na mshikamano, hivyo ushirikiano wenu na   Serikali ni muhimu.” Amesema, viongozi wa Serikali wakati wote wamekuwa tayari kufanyakazi na viongozi pamoja na taasisi mbalimbali za dini, lengo ni kuimarisha amani na utulivu uliopo nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza inawajibu wa kuhakikisha kwamba maeneo ya mkoa huu yanaendelea kuwa salama. Pia, Waziri Mkuu amempongeza Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Bin Mussa Kabeke kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo. “Nakupongeza kaimu sheikh wa mkoa kwa kuteuliwa na ninakutakia kila la heri katika kazi yako na kwamba dhamana yako kubwa ni kuwaunganisha waislamu na waumini wa dini zote.”

24 October 2018, 14:48