Tafuta

Vatican News
kundi la wapiganaji la Civilian Joint Task Force (CJTF) mjini Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria, wameaachilia huru watoto 833 kundi la wapiganaji la Civilian Joint Task Force (CJTF) mjini Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria, wameaachilia huru watoto 833   (AFP or licensors)

Nigeria: watoto 833 Nigeria waachiwa na kundi la wapiganaji

Kupitia taarifa iliyotolewa na UNICEF, tarehe 12 Oktoba 2018 mjini Geneva Uswisi na Maiduguri Nigeria, watoto 833 kaskazini mashariki mwa Nigeria waachiwa na kundi la wapiganaji. Taarifa inathibitisha kuwa hii ni mara ya kwanza watoto kuachiwa kutoka kundi la wapiganaji (CJTF) tangu mwaka 2017

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, linatoa pongezi kwa  kitendo cha kundi la wapiganaji la Civilian Joint Task Force (CJTF) mjini Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria, kuwaachilia huru watoto 833 ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya kuacha kuwatumia watoto katika mapigano. Kupitia taarifa yake iliyotolewa tarehe 12 Oktoba 2018 mjini Geneva Uswisi na Maiduguri Nigeria, UNICEF imesema hii ni mara ya kwanza watoto kuachiwa kutoka CJTF tangu mwaka 2017 wakati kundi lilipotia saini  mpango kazi wa kuweka mikakati ya kuacha na kuzuia kuwatumia watoto kufuatiwa kuwa kundi hilo kutajwa katika tripoti ya mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya masuala watoto na matumizi ya watoto katika mapigano.

Kutekeleza sheria za kimataifa za utu, haki za binadamu

Naye Bi Pernille Ironside, Naibu mwakilishi wa UNICEF nchini Nigeria amesema kuachiliwa kwa watoto hawa kunaonesha uwajibikaji au kujitolea katika kutekeleza vifungu vya mpango kazi na kutekeleza sheria za kimataifa za utu, haki za binadamu na pia sheria nyingine za kikanda na kitaifa ili kulinda haki za watoto.

Bi. Ironside akiwa  pia ni  mwenyekiti mwenza wa kikosi kazi cha Umoja wa Mataifa nchini humo kinachofuatilia na kuripoti kuhusiana na ukiukwaji wa haki za watoto amesema: “hii ni hatua kubwa katika kuelekea  suala la kumalizika kuchukua watoto na kuwatumia katika vita, lakini pamoja na hayo watoto wengi zaidi bado wanasalia katika makundi mengine ya wapiganaji katika nafasi ya upiganaji au katika majukumu ya usaidizi.”

UNICEF pia imesaidia kuzitafuta familia zao, kuwarejesha katika jamii zao

Hadi kufikia hii leo, jumla ya watoto 1,469 kati yao wavulana 1,175 na wasichana 294 waliohusishwa na kundi hilo la wapiganaji, wameshatambuliwa jiji Maiduguri. Tangu mwaka 2017, UNICEF imewasaidia kijamii na kiuchumi watoto8,700 ambao wameachiwa kutoka kwenye makundi ya wapiganaji. UNICEF pia imesaidia kuzitafuta familia zao, kuwarejesha katika jamii zao na kuwapa msaada wa kisaikolojia, elimu, mafunzo ya ufundi na fursa nyingine za kuboresha maisha yao.

Vurugu na ukatili dhidi ya watoto wa Sudan ya Kusini unatisha

Hata hivyo taarifa nyingine taarifa nyingine inasema kuwa, kiwango cha vurugu na ukatili wanachokabiliana nacho watoto wa Sudan Kusini kinatisha. Amethibitisha hayo Bi. Virginia Gamba mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya watoto na migogoro ya silaha.  Hii ni kutokana na ripoti iliyotolewa tarehe 15 Oktoba 2018,  mjini New York, Marekani na ofisi ya Bi. Gamba, ikionyesha kuwa, zaidi ya watoto 9,200 wametambuliwa na Umoja wa Mataifa kama waathirika wa ukiukwaji mkubwa wa haki zao katika kipindi cha miaka minne kilichoangaziwa na ripoti hiyo kuanzia Oktoba 2014 hadi Juni mwaka 2018. Bi Gamba amesema “Ukiukwaji mkubwa dhidi ya haki za watoto ilikuwa ni pamoja na kutekwa kwa minajiri ya kutumiwa katika mapigano, watoto wa kiume na wa kike walioingizwa katika mapigano waliuawa au kuumizwa au kufanyiwa vitendo viovu vya kingono. Watoto wengi pia wametumiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya wananchi na watoto wengine na hivyo kuleta mzunguko wa vurugu”.

Sudan Kusini, zaidi ya watoto 5,700  wamechukuliwa na kutumikishwa

Nchini kote Sudan Kusini, zaidi ya watoto 5,700 wamethibitishwa kuwa waliwahi kuchukuliwa na kutumikishwa na hivyo kuufanya kuwa ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki. Kwa kuongezea, takribani watoto 2000 walitekwa na zaidi ya 980 waliuwawa au kuumizwa na pande zote mbili yaani vikosi vya serikali na hata makundi ya wapiganaji. Vitendo viovu vya kingono, vikiwemo dhidi ya watoto, vilitumika kama mbinu ya kivita na kama adhabu. Ripoti pia inasema zaidi ya watoto 650 wamethibitika kufanyiwa vitendo viovu vya kingono katika kipindi hicho za utafiti, asilimia 75 ya matukio mengi yakihusisha kubakwa na watu wengi. Kutokana na kuwa si matukio mengi yaliyoripotiwa, ikiwemo matendo hayo dhidi ya watoto wa kiume, huenda idadi ni kubwa zaidi.

Halikadhalika ripoti hiyo imesema: jitihada za kuwalinda watoto kama vile kuutekeleza mpango kazi wa mwaka 2012 ambao SPLA waliuridhia tena mnamo mwa 2014, ulikiukwa kwa kuanza kwa mgogoro ndani ya kipindi cha utafiti. “Ni muhimu kuangazia ukatili unaofanywa na kuufufua upya mpango kazi uliopo ili kumaliza na kuzuia matendo yote ya kikatili dhidi ya watoto, kama ilivyokuliwa na mamlaka wakati wa ziara yangu ya septemba,” Bi Gamba amesema.

 

16 October 2018, 14:18