Cerca

Vatican News
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania anakumbukwa na wengi kutokana na mchango wake wa kutetea haki, ustawi na maendeleo ya wengi. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania anakumbukwa na wengi kutokana na mchango wake katika kutetea haki, ustawi na maendeleo ya wengi. 

Mwalimu J. K. Nyerere ni mfano bora wa kuiga katika kuwatetea wa wanyonge

Wadau wa kisiasa nchini Tanzania wanasema, Katiba Mpya si kati ya vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano, lakini ni kati ya mahitaji na changamoto kubwa zilizoachwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya watanzania katika medani mbali mbali za maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa taifa la Tanzania ataendelea kukumbukwa na wengi ndani na nje ya Tanzania, kwa kusimamia misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu bila ubaguzi. Hata Tanzania ya wakati huu, na Afrika katika ujumla wake, ina kiu kikubwa na watu kama hawa wanaoweza kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao ya wengi, badala ya kujikita katika uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na kwamba uongozi ni huduma!

Familia ya Mungu nchini Tanzania kila mwaka ifikapo tarehe 14 Oktoba inafanya kumbu kumbu ya Siku ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipofariki dunia nchini Uingereza kunako mwaka 1999. Ni kiongozi aliyejipambanua kwa kujenga, kuimarisha na kutetea umoja wa taifa na muungano wa watanzania. Alisimamia harakati za mapambano ya kisiasa na ukombozi ndani ya Tanzania na kusini mwa Bara la Afrika. Alijitahidi kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi jirani, kwa kuzingatia misingi ya: haki, amani, utu na heshima ya binadamu.

Ni kiongozi aliyekazia maendeleo endelevu ya binadamu yanayozingatia mahitaji yake msingi: kiroho na kiutu; kwa kukazia: haki msingi za binadamu, utu na heshima yake na wala si maendeleo ya vitu, bali watu wenyewe wapewe kipaumbele cha kwanza! Wadau wa kisiasa wanasema, Katiba Mpya si kati ya vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano, lakini ni kati ya mahitaji na changamoto kubwa zilizoachwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya watanzania katika medani mbali mbali za maisha.

Kanisa mahalia bado linaendeleza mchakato wa Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwamini mlei, Baba wa familia na kiongozi wa kisiasa, ili siku moja, aweze kutangazwa kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu, kama mfano bora wa kuigwa katika uwanja wa kisiasa aliyejitahidi kuhakikisha kwamba, siasa kamwe haiwezi kuwa ni kikwazo katika ukuaji na ukomavu wake wa maisha ya kiroho!

Mwalimu Nyerere

 

14 October 2018, 15:23