Tafuta

Vatican News
Maziko ya Kitaifa ya watanzania waliofariki dunia kwa ajali ya Kivuko cha MV. Nyerere, tarehe 20 Septemba 2018 Maziko ya Kitaifa ya watanzania waliofariki dunia kwa ajali ya Kivuko cha MV. Nyerere, tarehe 20 Septemba 2018  (AFP or licensors)

Ajali ya Kivuko cha Mv. Nyerere: Kenya yatoa rambi rambi shilingi milioni 125

Rais Kenyatta ametoa kiasi cha shilingi milioni 125 kama rambi rambi ya wananchi wa Kenya kwa watanzania waliofikwa na msiba mzito uliopelekea watu 228 kupoteza maisha yao na wengine wengi kujeruhiwa. Watu 41 waliokolewa katika ajali hiyo iliyotokea tarehe 20 Septemba 2018 kwenye Ziwa Victoria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Ikulu, Dar Es Salaam.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amemshukuru sana Rais Uhuru Kenyatta pamoja na wananchi wote wa Kenya, kwa kuguswa na ajali ya kivuko cha MV. Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba 2018 kwenye Ziwa Victoria na kusababisha watanzania 228 kupoteza maisha na wengine wengi kupata majeruhi. Katika ajali hiyo, watu 41 akiwemo mwandishi wa kivuko hicho Alphonce Charahani walinusurika. Rais Kenyatta ametoa kiasi cha shilingi milioni 125 kama rambi rambi ya wananchi wa Kenya kwa watanzania waliofikwa na msiba huu mzito!

Rambi rambi hii imewasilishwa kwa Rais Magufuli, hapo tarehe 8 Oktoba 2018 na Dr. Dan Kazungu, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, wakati walipokutana Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Dr. Kazungu amesema, rambi rambi hii ni kielelezo cha ujirani mwema, upendo na mshikamano kati ya Tanzania na Kenya, kwani janga hili limewagusa pia wananchi wa Kenya katika ujumla wao. Kwa namna ya pekee kabisa, Rais Magufuli amemshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuguswa na msiba huu mzito kwa watanzania na kuahidi kwamba, fedha hii itaelekezwa kuwasaidia wananchi wa visiwa vya Ukerewe ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali kubwa yenye hadhi ya wilaya.

Hapo awali, Serikali ya Tanzania ilikuwa imepanga kujenga wodi tatu za wagonjwa. Kama sehemu ya shukrani na kutambua mchango wa Rais Uhuru Kenyatta, Rais Magufuli kadili ya taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari amesema kwamba, wodi moja itapewa jina la Kenyatta kama kumbu kumbu endelevu ya moyo huu wa mshikamano!

Itakumbukwa kwamba, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, hivi karibuni aliunda Tume ya kuchunguza ajali ya Kivuko cha Mv. Nyerere, yenye wajumbe saba, ambayo inaongozwa na Jenerali Mstaafu George Waitara. Serikali ya Tanzania pia imeshatoa maamuzi ya kuboresha zaidi hali ya usafiri kisiwani hapo ili kwenda na kasi ya maendeleo ya watu!

Mv. Nyerere 2018
09 October 2018, 10:30