Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokeataarifa ya ajali ya MV. Nyerere, tarehe 25 Oktoba 2018 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokeataarifa ya ajali ya MV. Nyerere, tarehe 25 Oktoba 2018 

Waziri Mkuu Majaliwa apokea ripoti ya ajali ya MV. Nyerere!

Waziri Mkuu amesema Serikali inaamini mambo yote yaliyosheheni katika taarifa hiyo ni yale ambayo Watanzania wanasubiri kuona yakifanyiwa kazi. MV Nyerere ilipindika na kuzama Septemba 20, mwaka huu katika ziwa Victoria ambapo Watanzania zaidi 200 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 40 waliokolewa.

Na Mwandishi maalum Dar es Salaam & Padre Mjigwa, R. – Vatican

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amepokea ripoti ya uchunguzi wa  ajali ya kivuko cha MV Nyerere kutoka kwa kamati iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo. Amepokea ripoti hiyo Alhamisi, Oktoba 25, 2018 kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati  hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstafu, Jenerali George Waitara,kwenye makazi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuishikuru kamati hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imethibitisha umakini wao.

Pia ameipongeza kamati hiyo kwa namna walivyotumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya mambo waliyoyabaini. “Nimepokea taarifa kwa niaba ya Serikali, Serikali itafanya mapitio ya taarifa yote na viambatisho vyake na itapitia kwa kina mapendekezo mliyoyatoa ambayo yote yatafanyiwa kazi.” Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inaamini mambo yote yaliyosheheni katika taarifa hiyo ni yale ambayo Watanzania wanasubiri kuona yakifanyiwa kazi. MV Nyerere ilipindika na kuzama Septemba 20, mwaka huu katika ziwa Victoria ambapo Watanzania zaidi 200 walipoteza maisha na wengine Zaidi ya 40 waliokolewa.

Septemba 24 mwaka huu Waziri Mkuu alitangaza kamati ya kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe saba ambayo iliyoongozwa na Jenerali mstaafu, Waitara. Akitangaza majina hayo kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, Waziri Mkuu alisema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja. Aliwataja wajumbe wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi. Wengine ni SACP Camillus Wambura na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uratibu Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bashiru Taratibu Hussein.

Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 21 Mei 1996 MV Bukoba ilizama katika Ziwa Victoria na kusababisha watu Zaidi ya 800 kupoteza maisha. Tarehe 10 Septemba 2011 Meli ya MV Spice ilipata ajali Bahari ya Hindi na kusababisha vifo vya watu 200 na tarehe 18 Julai 2012 Meli ya MV. Skagit ilizama katika Bahati ya Hindi na kusababisha vifo vya watu 150. Ni matumaini ya watanzania kwamba, ripoti ya Tume ya Waitara, itatoa ushauri ambao utaisaidia Tanzania kuweza kuboresha usafiri wa majini kwa kuimarisha usalama pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa na wadau mbali mbali, ili kuokoa maisha ya watu na mali zao!

25 October 2018, 15:28