Wakulima wa bunia wa Ethiopia na Burundi wanaombwa watumie fursa zilizopo kupanua soko Wakulima wa bunia wa Ethiopia na Burundi wanaombwa watumie fursa zilizopo kupanua soko  

Burundi na Ethiopia:tumieni fursa ya kahawa kupata masoko

Ingawa soko la kahawa limeendelea kukua lakini Ethiopia yenye asili ya kahawa aina ya arabica na Burundi ambako kilimo cha buni kimeshamiri tangu miaka ya 1920, bado zinaweza kuchukua hatua zaidi ili kunufaika

Sr. Angela Rwezaula – Vatican  

Wakulima wa buni katika nchi za Ethiopia na Burundi ni lazima watumie fursa iliyopo sasa la kupanuka kwa soko la kahawa hususan kwa watu milioni 500 wanaotumia kinywaji hicho kila siku duniani. Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema hayo katika ripoti yake iliyotolewa tarehe 17 Oktoba 2018  huko Geneva, Uswisi ikiangazia sekta ya kilimo cha buni ukanda wa Afrika Mashariki.

Ripoti kuzingatia masoko ya bidhaa duniani

 Ripoti hiyo ambayo ni sehemu ya mfululizo wa ripoti zinazoangazia masoko ya bidhaa duniani, imesema ingawa soko la kahawa limeendelea kukua lakini Ethiopia ambako ni asili ya aina ya kahawa ya arabica na Burundi ambako kilimo cha buni kimeshamiri tangu miaka ya 1920, bado zinaweza kuchukua hatua zaidi ili kunufaika na kupanuka na kuimarika kwa soko la zao hilo ili kuwa na hakikisho la upatikanaji wake na pia ubora wake.

Mkurugenzi wa kitengo cha biashara ya kimataifa na bidhaa UNCTAD, Bi Pamela Coke-Hamilton ametoa mfano wa changamoto ambazo mataifa hayo mawili yanakabiliana nayo na hivyo kushindwa kunufaika ipasavyo na kuendelea kupanuka kwa matumizi ya kahawa kwenye masoko ya hali ya juu. “Katika nchini ya Burundi kilimo cha buni kimekumbwa na mazingira tete, kutokana na hali ya hewa isiyotabirika, mimea iliyozeeka, idadi kubwa ikiwa ina miaka zaidi ya 40, udongo hauna rutuba bila kusahau ukosefu wa mbinu bora za kilimo na ukosefu wa utulivu wa kisiasa”.

Kadhalika ameongeza Bi. Coke-Hamilton pamoja na mauzo ya chai, mauzo ya kahawa nje ya nchi huchangia asilimia 90 ya mapato ya fedha za kigeni ya Burundi. Hata hivyo amesema, “nchi ya Burundi imeshadhihirisha kuwa inaweza kuzalisha kahawa bora ambayo inapendwa na wanywaji,  na hivyo basi hiki ni kichocheo tosha cha kuimarisha wakulima wadogo kupitia vyama bora zaidi vya ushirika”.

Uwekezaji binafsi kuoitia ubia wa serikali na wafanyabiashara

Akihamasisha zaidi  pia juu ya uwekezaji wa kibinafsi kupitia ubia kati serikali na wafanyabiashara amesisitiza kuwa ushirika huo unapaswa kuimarisha ili sekta ya kilimo cha buni iwe na ushindani zaidi.  Na kwa upande wa nchi ya Ethiopia amesema, nayo inakabiliwa na mazingira kama ya Burundi, “isipokuwa tatizo ni ukosefu wa uhakika wa ubora wa kahawa inayozalishwa kutokana na wadudu kushambulia mara kwa mara, mbinu duni za kilimo, ukosefu wa mafunzo kwa wakulima na udhaifu katika usimamizi wa mnyonyoro mzima wa thamani kuanzia shambani hadi kwa mnywaji.”

Pamoja na hayo amethibitisha kwamba, bado kuna fursa zitakazowezesha Ethiopia kutumia fursa ya sasa ili wakulima waweze kunufaika na hatua ya buni  wanayolima kumfikia mnywaji kwenye masoko ya hali ya juu.

18 October 2018, 15:50