Vatican News
Unicef inasema milioni 131 ya watoto wasichana duniani hawasomi shule Unicef inasema milioni 131 ya watoto wasichana duniani hawasomi shule 

11 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya watoto wa kike!

UNICEF inatangaza kuwa kwa ngazi ya dunia, milioni 131 ya wasichana duniani hawasomi shule, msichana 1 kati ya 3 kulinganisha na mvulana 1 kati ya 6 wenye umri kuanzia 15-29 hawana kazi, wala hawakupata kisomo. Dunia, karibu milioni 15 ya wasichana, wa umri kati ya 15-19 wanalazimisha kuwa na mahusiano ya kingono au kulazimishwa ndoa za utotoni

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katika siku ya Kimataifa ya watoto wa kike na wasichana, UNICEF  inatangaza kuwa kwa ngazi ya dunia, milioni 131 ya wasichana duniani hawasomi shule, msichana 1 kati ya 3 kulinganisha na mvulana 1 kati ya 6 wenye umri kuanzia 15-29 hawana kazi, wala hawakupata kisomo au mafunzo yoyote. Katika dunia, karibu milioni 15 ya wasichana, wenye umri kati ya 15-19 wanalazimisha kuwa na mahusiano ya kingono au aina nyingine za nguvu ya kijinsia wakati wa  maisha yao.

Milioni 600 wasichana wenye uwezo, nguvu, ubunifu kujibu suala la ajira

Tarehe 11 Oktoba  Katika fursa za Siku ya Kimataifa kwa ajili ya watoto wa wadogo wa kike na wasichana UNICEF inakumbusha kuwa duniani, kuna milioni 600 ya wasichana wadogo wenye uwezo, nguvu, ubunifu, hata  mwamko wa kujibu katika suala la kutafuta ajira katika viwanda duniani. Kutokana na ongezeka la wasichana milioni 131 kuwa nje ya shule, na idadi hii kwa sasa inaonesha kwamba mwaka 2030 zaidi ya nusu ya wasichana diniani, hawatakuwa na uwezo wa kufikia hata shule za msingi na kujua kusoma na kuandika kwa maana hiyo  hata mzunguko wa kuendelea kwa ngazi ya Sekondari.

Serikali kusikiliza watoto wa kike na wapatieni haki zao

Kutokana na hilo hata  wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika kilele cha maadhimisho hayo wametaka serikali zote duniani zisikilize sauti za watoto wa kike na wasichana kama njia mojawapo ya kuwapatia haki zao za msingi. Wataalamu hao kupitia taarifa yao iliyotolewa tarehe 9 Oktoba 2018, huko mjini Geneva, Uswisi wamesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa hivi sasa, vikwazo vingi vimezingira kundi hilo na hivyo kuwazuia kustawi licha ya kwamba mataifa kupitia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs wameahidi kuwalinda.

“Mila na tamaduni potofu zinazohusiana na umri na jinsia mara nyingi zinazuia wasichana kusonga mbele na hivyo ni lazima tutambue mazingira ambamo wanaishi na changamoto wanazokabiliana nazo ili haki zao za kibinadamu ziweze kutimizwa na hatimaye wawezeshwe na wawe wachangiaji kwenye jamii zao,” imesema taarifa. Wataalamu hao wamesema kupitia malengo namba 1, 4, 5, 8 na 16, jamii ya kimataifa imeazimia kujenga mazingira ambamo kwayo wasichana wanaweza kukua bila kubaguliwa, kunyanyaswa na ambamo umri na jinsia yao katu havitakuwa vikwazo vya wao kuchanua na kustawi.

Ndoto kuwa mbali za kufikia malengo

Hata hivyo wamesema ahadi hizo zimesalia ndoto na kuna hatari ya kwamba hata mafanikio yaliyopatiakana yanaweza kufutika, wakisema kuwa “idadi ya watoto wa kike wanaoandikishwa shule ya msingi imeongezeka lakini wanapofikia umri wa barubaru wako hatarini zaidi kuozwa mapema na hivyo elimu inasalia ndoto.”

Kando  ya ndoa za mapema, wataalamu hao wamesema watoto wa kike na wasichana wanakabiliwa na usafirishaji haramu, ukeketaji na hata kukosa haki ya kujisafi wanapokuwa shuleni pindi wanapokuwa kwenye kipindi cha mabadiliko yao. Kwa mantiki hiyo wataalamu hao wamesema ni lazima kusikiliza kile ambacho watoto wa kike na wasichana wanasema na wapatiwe fursa ili waweze kufanikiwa na haki zao za kibinadamu siyo tu ziheshimiwe bali pia zilindwe na zitimizwe.

11 October 2018, 16:24