Utofauti wa elimu,afya na kipato vinaongeza pengo la usawa!
Sr. Angela Rwezaula - Vatican
Pengo kubwa la usawa kati ya ustawi wa binadamu unarudisha nyuma maendeleo ya ustawi wa binadamu, imesema ripoti mpya kuhusu kipimo cha maendeleo ya binadamu, HDI, iliyotolewa tarehe 14 Septemba 2018 mjini New York, Marekani na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP. Ripoti hiyo inapima mafanikio katika kuboresha afya, elimu na kipato ikihusisha nchi 189 zikipangwa kuanzia ya juu kabisa yenye nafasi nzuri hadi ya mwisho.
Mataifa ambayo bado yamedorora: Norway, Uswisi, Australia, Ireland na Ujerumani ziko nafasi ya juu, na hali nafasi za chini kabisa zinashikiliwa na Syria, Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Chad na Burundi. Mizozo na mapigano imetajwa kuwa ndiyo sababu kuu ya nchi hizo kushika nafasi za chini zaidi.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mtawala Mkuu wa UNDP, Achim Steiner amesema kuwa, “kwa wastani mtoto anayezaliwa leo katika nchi yenye maendeleo duni ya binadamu anatarajiwa kuishi takriban miaka 60,wakati mtoto wa nchi ambayo watu wake wameendelea anaweza kuishi hata miaka 80.”
Kuna mafanikio yoyote?: Hata hivyo kuna mafanikio hususan katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, pamoja na Asia ya Kusini, huduma za zinaonekana kuwa zimeimarika kwa kuzingatia kuwa kiwango cha kuishi pindi mtu anapozaliwa kimeongezeka kwa asilimia 11 wakati katika maeneo mengine ni asilimia 7. Halikadhalika kati ya mataifa 189 yaliyohusishwa 59 kati ya hayo kwa sasa yako katika kundi la mataifa yaliyo na kiwango cha juu na ni mataifa 38 tu ambayo yameshuka hadi kiwango cha chini kwenye kipimo hicho cha maendeleo ya binadamu kwa mwaka huu wa 2018.
Hali ya sasa: Kwa mujibu wa ripoti hiyo idadi hiyo ni mafanikio makubwa kwa kuwa takriban miaka minane iliyopita ni mataifa 46 tu ndiyo yalikuwa juu huku mataifa ya kiwango cha chini yalikuwa 49. Miongoni mwa mataifa ya kiafrika ambayo yanapanda kimaendeleo ni Botswana ambayo ilipanda juu nafasi nane, ikilingana na Uturuki pamoja na Jamhuri ya Dominica. Kuhusu tofauti za kijinsia ,ripoti inasema kumeonekana maendeleo ya kujaribu kuziba pengo kati ya jinsia zote wakati wa umri mdogo lakini pengo linaongezeka wanapokuwa watu wazima.
Imetoa mfano kuwa katika sekta ya nguvu kazi duniani bado idadi ya wanawake ni asilimia 49 ikilinganishwa na asilimia 75 ya wanaume ukosefu wa elimu ukitajwa moja ya sababu zinazokwamisha wanawake kusonga mbele. Kuhusu mchango wa wanawake kushiriki katika siasa za ubunge, idadi ya wanawake bado ni ndogi ingawa ripoti inasema inatofautiana kikanda ambapo katika bara Asia wanawake huchukua asilimia 17.5 na Uarabuni asilimia 18.