Madaktari Bingwa wa Tanzania wamefanikiwa kutengenisha watoto mapacha walioungana sehemu ya tumbo Madaktari Bingwa wa Tanzania wamefanikiwa kutengenisha watoto mapacha walioungana sehemu ya tumbo  

Tanzania:Hospitali ya Muhimbili kufanya upasuaji wa mapacha!

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kufanya upasuaji wa kuwatenganisha pacha walioungana ambao walizaliwa kijiji cha Vigwaza mkoani Pwani Tanzania. Upasuaji huo ulifanyika tarehe 22 Septemba 2018 ukishirikisha jopo la madaktari bingwa 10 wa upasuaji wa watoto.

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Imewezekana nchini Tanzania kufanya upasuaji wa mapacha walioungana. Mapacha ambao wote ni wavulana walizaliwa tarehe 12 Julai 2018 katika kijiji cha Vigwaza mkoani Pwani,  kwa njia ya kawaida, wakati mama yao akiwa njiani kuelekea hospitali  na watoto hao walikuwa wameungana katika tumbo. Kutokana na tukio hilo, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) nchini Tanzania  imefanikiwa kufanya upasuaji wa  kuwatenganisha mapacha  hao walioungana.  Upasuaji huo ulifanyika tarehe  22 Septemba 2018 ukishirikisha jopo la madaktari bingwa 10 wa upasuaji wa watoto.

Sababu ya mafanikio ya huduma ya upasuaji

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano tarehe 26 Septemba, 2018 mkurugenzi mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema sababu mojawapo ya mafanikio hayo ni uwekezaji katika huduma ya upasuaji. Amethibitisha kuwa  tofauti na zamani, kwa sasa miundo mbinu ya upasuaji imeboreshwa hivyo hakuna haja ya kwenda nje ya nchi kufanya upasuaji unaoweza kufanywa nchini.

Kadhalika ameongeza kusema, “Serikali imeboresha huduma hii ya upasuaji kwa watoto ili kupunguza gharama zisizo za lazima za kwenda nje ya nchi”.  Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto, Daktari  Petronia Ngiloi amesema watoto hao waliungana sehemu ya tumbo. “Watoto hawa hawakuungana sana kitu ambacho walichangia ni maini hivyo tumefanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa tunaweza kuwatenganisha hapahapa nchini,"amesema.

Furaha ya mama yao mzazi wa mapacha

Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao ambao bado hawajapewa majina,  Ester Simoni ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo.  “Nimefurahi kuwaona watoto wangu wametenganishwa nilikuwa najiuliza nitawalea vipi wakiwa wameungana,” amesema Ester. Taarifa zinasema kuwa ,watoto hao wenye umri wa miezi miwili wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.

27 September 2018, 15:34