Tafuta

Mazishi ya aliyekuwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan mjini Accra Ghana Mazishi ya aliyekuwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan mjini Accra Ghana 

Mazishi ya Bwana Annani yamefanyika huko Accra nchini Ghana

Tangu kifo cha Kofi Annan, nimekuwa nikitafakari ni kitu gani kilimfanya awe wa kipekee! Hivi ndivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewaeleza maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya mmoja wa watangulizi wake Kofi Annan aliyezikwa tarehe 13 Septemba 2018 huko Accra nchini Ghana.

"Tangu kifo cha Kofi Annan, nimekuwa nikitafakari ni kitu gani kilimfanya awe wa kipekee". Hivi ndivyo Bwana Guterres alivyoanza hotuba yake mbele ya maelfu ya waombolezaje akitaja mkewe Annan, Nane pamoja na wanae na ndugu jamaa na marafiki walioshiriki tukio hilo mjini Accra akiwemo Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo. tarehe 13 Septemba 2018 huko Accra nchini Ghana.

Bwana Guterres amesema baada ya kufikiria sana alibaini kuwa “Kofi Annan alikuwa ni wa kipekee na mmoja wetu. Alikuwa kiongozi wa aina yake wa kimataifa na mtu ambaye yeyote yule duniani angeweza kujiona ndani- wale walio mbali waliokumbwa na umaskini, waliokata tamaa na kumuona mshirika wao, watumishi wa ngazi ya chini wa UN wakifuata nyayo zake, na vijana ambao hadi pumzi yake ya mwisho aliwaeleza kamwe hauko mdogo kuongoza na kamwe hatuko wazee kuweza kujifunza.”

Bwana Guterres akitumia usemi wa zamani ya kwamba Sanaa ya diplomasia ni kutosema chochote hususan unapozungumza, lakini “Kofi Annan aliweza kusema kila kitu na wakati mwingine bila kutoa neno ilitokana na utu na imani  ya maadili na utu ambao ulikuwa ndani yake. Sauti yake ilkuwa laini ikifanya watu watabasamu na kudhania ni muziki. Lakini maneno yake yalikuwa thabiti na yenye busara.”

Katibu Mkuu amesema ingawa Kofi Annan amefariki duniani, ataendelea kukumbukwa akisema kuwa iwapo jamii itaendelea kusikiliza kwa makini bado itasikia sauti yake ikisema “Unafahamu cha kufanya. Tunzaneni. Tunzeni sayari yetu. Tambueni utu wa watu wote na ungeni mkono Umoja wa Mataifa, sehemu ambayo sote tunaweza kukutana na kutatua matatizo yetu na kujenga mustakhbali wetu wote.”

Nnane Annan amezungumza

Naye mkewe Kofi Annan aitwaye Nane ambaye ni raia wa Sweden alipata fursa ya kuzungumza ambapo ameshukuru wananchi wa Ghana kwa jinsi walivyokuwa karibu na familia yao tangu habari za msiba huo mzito wa mumewe. Bi. Annan amesema wameshuhudia salamu za rambirambi kutoka viongozi mbalimbali wa dunia, wakitambua utu wa ke alioonyesha duniani pamoja na mafanikio, halikadhalika ni fikra za wengine wengi ambao majina yao hamuwezi kuyafahamu na ambao aligusa maisha yao.

"Hii hasahasa ni vijana ambao  aliwaamini sana na ambao alizungumza nao moja kwa moja na wao walivutiwa naye kwa kuwa alizungumza  nao kutoka moyoni bila hila na kwa maslahi ya kweli." amesema Bi. Annan. Na akahitimisha hotuba yake kwa kusema kuwa  mchango wake utaendelezwa na taasisi  ya Kofi na wale wote walioamini alichokifanya na zaidi ya yote akasema.. "Mpenzi wangu, sasa uko nyumbani ambako ndio  ulianzia safari yako ndefu, pumzika kwa amani na kuendelea kutuhamasisha na kutuongoza popote pale tulipo."

Ikumbukwe, Kofi Annan, amekuwa  Katibu Mkuu wa 7 wa Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 1997 hadi 2006 alifariki dunia huko Berne nchini Uswisi tarehe 18 mwezi uliopita wa Agosti akiwa na umri wa miaka 80.

14 September 2018, 13:02