Tafuta

Ugonjwa wa Ebola nchini DRC. Ugonjwa wa Ebola nchini DRC. 

Tamko la Serikali ya Tanzania kuhusu ugonjwa wa Ebola

Hadi sasa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola. Hata hivyo, kugunduliwa kwa ugonjwa huu kwenye jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na nchi za Uganda na Rwanda ni jambo la kutuweka kwenye wasi wasi kwani eneo hili liko karibu sana na nchi yetu.

Na Waziri Ummy A. Mwalimu (Mb). Dar Es Salaam.

Utangulizi: Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kutoa taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Nchi hiyo ya DRC imetangaza tena kuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mnamo tarehe 1 mwezi Agosti, 2018, ambapo jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10 vilitolewa taarifa na wagonjwa 4 kati yao walithibitishwa kimaabara kuwa na ugonjwa wa Ebola. Wagonjwa hawa wametokea katika vijiji/Maeneo ya Mangina ikiwa ni kama km 30 tu magharibi mwa mji wa Beni kwenye jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na nchi ya Uganda ikiwa ni kama km 100 tu, na pia likiwa karibu sana na nchi ya Rwanda.

Huu ni mlipuko wa 10 wa ugonjwa wa Ebola kutokea nchini DRC, na umetokea wiki moja baada ya nchi hiyo kutangaza kuisha kwa mlipuko mwingine uliotokea mwezi Mei mwaka huu ambao ulikuwa katika jimbo la Equator, Magharibi mwa DRC, umbali wa zaidi ya km 2,000 kutoka eneo la huu mlipuko mpya uliotokea.

Hadi sasa hapa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola. Hata hivyo, kugunduliwa kwa ugonjwa huu kwenye jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na nchi za Uganda na Rwanda ni jambo la kutuweka kwenye wasi wasi kwani eneo hili liko karibu sana na nchi yetu kuliko eneo lingine lolote ambako ugonjwa huu umeshawahi kutokea kwenye nchi ya DRC. Hivyo nchi yetu ipo hatarini kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na ukaribu na muingiliano wa watu, hasa kuhusiana na wasafiri wanaotoka na kuingia hapa nchini.

Kwa sababu hizi, watanzania hatuna budi kuchukua tahadhari ya hali ya juu ili kujikinga na kudhibiti na ugonjwa wa Ebola.  Hivyo Wizara inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa huu kwa wananchi wote katika Mikoa yote ya Tanzania, lakini hasa ile inayopakana na nchi jirani za DRC, Uganda na Rwanda. Mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe. Aidha tahadhari na hatua stahiki zichukuliwe katika maeneo yote ya mipakani ambapo abiria wanaingia nchini kutoka nchi jirani.

Ugonjwa wa Ebola

Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola ambavyo huambukiza kwa njia zifuatazo; Kugusa Damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo. Kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo. Kugusa wanyama (Mizoga na wanyama wazima) walioambukizwa kama vile Sokwe na Swala wa msituni.

Dalili za Ugonjwa Dalili za Ugonjwa huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa baada ya siku 2 hadi 21 tangu kupata maambukizi. Dalili hizo ni pamoja na;

1. Homa kali ya ghafla,

2.   Kulegea kwa mwili,

3.   Maumivu ya misuli,

4.   Kuumwa kichwa na vidonda kooni.

5.   Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi na pia figo na Ini kushindwa kufanya kazi.

6.   Kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa na damu ndani na nje ya mwili.

Namna ya Kujikinga na ugonjwa wa Ebola: Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni: Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyefariki akiwa na dalili za Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za Afya kwa ushauri.

Kuepuka kula nyama za Wanyama wa porini kama sokwe, swala na popo na pia kugusa mizoga ya Wanyama hao. Kuepuka mila na desturi  zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola. Kuzingatia usafi wa mwili. Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na wa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye  dalili za Ebola.. Kuwahi katika vituo vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili za ugonjwa huu.

Hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara kufuatia kupatikana kwa taarifa ya Ugonjwa huu huko DRC. Mei 2018, hatua zifuatazo zinaendelea/zimechukuliwa na Wizara ili kujiandaa kukabiliana na mlipuko huo: Kufanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini (Operational readiness assessment) kwa nchi nzima kwa kushirikiana na WHO na kuainisha mapungufu ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi. Mapungufu hayo yanaendelea kuyafanyiwa kazi ili kujenga uwezo na utayari katika nchi yetu.

Tumetengeneza mpango mkakati wa kujiandaa na kupambana na mlipuko wa Ebola endapo utatokea nchini (Costed Ebola Contingency Plan). Mpango huu umeandaliwa kwa kushirikiana na WHO. Mpango umeainisha maeneo ya kujenga uwezo kwa wakati huu wa kujiandaa, pamoja na hatua za kuchukua endapo ugonjwa utaingia ikiwa ni pamoja na gharama zake.

Tumefanya mafunzo ya Timu za dharura (Rapid Response Teams) ngazi ya Taifa na katika Mikoa ya Dar es Salaam, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma na Kagera. Tumeimarisha ufuatiliaji wa wasafiri mipakani (travellers entry screening) kwa kutumia vifaa vya kupima joto la mwili (thermo scanners) na fomu maalum za wasafiri. Wizara imepokea vifaa vya kukabiliana na Ebola kutoka WHO vikiwemo; Thermo scanners, Vifaa Kinga, au PPE, kama vile gloves, body bags, vifaa vya ufungashaji wa sampuli nk. Vifaa hivyo vimeanza kusambazwa mikoani kupitia MSD

Uelimishaji wa umma umefanyika na unaendelea kufanyika kwa kupitia vyombo vya habari vya kitaifa na kijamii, na mitandao ya kijamii. Vile vile vipeperushi na mabango vinaendelea kuandaliwa. Vikao vya uratibu vimefanyika katika ngazi ya taifa na mikoa ambayo ipo katika hatari zaidi. Pia ufuatiliaji wa karibu unaendelea kupitia Kituo cha ufuatiliaji wa magonjwa ya dharura cha Wizara (Public Health Emergency Operation Centre is on “High Alert”)

Wataalam kutoka ngazi ya Taifa kwa sasa wako katika mikoa ya: Kigoma, Katavi, Rukwa, Kagera, Kilimanjaro, Mwanza, Songwe na Mbeya kufanya tathmini ya utayari katika ngazi ya mikoa na Wilaya (Readiness Assessment). Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kutekeleza kazi nyingine kama ifuatavyo: Kufanya mafunzo katika mikoa iliyo salia ikiwemo Mwanza, Kilimanjaro na Mbeya ambayo imesalia katika ile mikoa nane iliyo katika hatari zaidi. Mafunzo ya waandishi wa habari 30 (media orientation). Zoezi la udhibiti wa matukio ya dharura (simulation exercise) katika ngazi ya Taifa. Mafunzo kwa wasfirishaji wa sampuli kwenda katika maabara

 Hitimisho: Nawaomba Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wote nchini kuchukua Tahadhari na kuendelea kuelimisha wananchi wote juu ya ugonjwa huu na kuwataka kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwani mpaka sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuugua ugonjwa huu hapa nchini. Aidha Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kuendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti ili ugonjwa huu usiingie nchini. Vilevile Wizara itaendelea kutoa taarifa pamoja na Elimu kwa Jamii kadri itakavyohitajika.

 

 

11 August 2018, 08:35