Tafuta

Vatican News
Siku ya Kimataifa ya kupinga mazoezi ya silaha za kinyuklia Siku ya Kimataifa ya kupinga mazoezi ya silaha za kinyuklia 

Tarehe 29 Agosti ni Siku ya Kimataifa ya kupinga nyuklia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres, katika ujumbe wake maalumu tarehe 29 Agosti ambayo ni siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya nyuklia amesema, histori ya majaribio ya nyuklia ni ya machungu na ambayo imeathiri watu na wengi wao kutoka katika jamii za wanyonge zisizo jiweza duniani!

Frt.Titus Kimario - Vatican

Histori ya majaribio ya nyuklia ni ya machungu na ambayo imeathiri watu zaidi ya  2,000  wengi wao kutoka katika jamii za wanyonge zisizojiweza duniani. Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika ujumbe wake  maalumu tarehe 29 Agosti ambayo ni  siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya nyuklia. Athari hizo mbaya zisizojali mipaka ya kimataifa  ni dhahiri pia katika mazingira, afya, uhakika wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.

Bwana Guterres ameongeza  kusema kuwa  tangu kumalizika  kwa  vita baridi, kumekuwa na desturi ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia ambayo imekiukwa na taifa moja tu katika karne hii. Siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia ilianza kuadhimishwa baada ya kupitishwa azimio na Baraza Kuu Disemba 2 mwaka 2009 lililotaka kuongeza uchagizaji dhidi ya athari za majaribio ya silaha za nyuklia na  haja ya  kukomesha majaribio hayo kama njia  ya kuwa na dunia isiyo na silaha za nyuklia. Azimio hiloliliwasilishwa na Kazakhstan na kuungwa mkono na  mataifa mengine.

Mwakilishi wa kudumu wa Kazakhstani katika Umoja wa Mataifa ni Kairat Umarov akizungumza na Vyombo vya habari vya Umoja wa Mataifa UN  amefafanua kuhusu athari za majaribio ya silaha hizo. “Madhara ya majaribio ya Nyuklia angani, ardhini na chini ya ardhi ni makubwa, ni sawa na kunyunyuzia kilo 300 za chembechembe zenye sumu za madini ya plotonium katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba elf 18, eneo kubwa ambalo leo hii halitumiki tena”. Ameongeza kusema “ watu wengi katika mameneo ambayo kumefanyika majaribio hayo hawataki kuzaa kwa hofu ya kupata watoto walio na ulemavu kama kutokuwa na mikono wala miguu kutokana na sumu ya athari za nyuklia. Siku hii ya kimataifa pia ni siku ya kukumbuka  kufungwa kwa kituo cha majaribio ya nyuklia cha Urusi  kunako tarehe Agosti 29 1991 kilichokuwa sehemu ya  Semipalatinsk. Kituo hicho japo kilimilikiwa na Urusi lakini kilikuwa nchini Kazakhstan, ambapo zamani eneo lote hilo lilikuwa chini ya muungano wa Soviet kabla ya kusambaratika.

Hatia hivyo mapema Mei mwaka huu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitangaza mwelekeo wake mpya  kuhusu udhibiti wa silaha katika juhudi za kutokomeza  silaha za nyuklia  pamoja na silaha zingine zinazoweza kusababisha maangamizi dunia  kutokana na makosa, iwe  ya kiufundi, kielektroniki au ya kibinadamu.  Bwana Antonio Guterres akizindua ajenda yake yenye kauli mbiu “kutunza usalama katika wakati  wetu pamoja”, kwenye  Chuo Kikuu cha Geneva, huko Uswiss, alisema, Umoja wa Mataifa uliundwa  kwa lengo la kuondoa vita inayotumika kama chombo cha sera ya kigeni.  Lakini kwa  miongo saba sasa imepita, dunia yetu bado imeendelea na hatari zaidi ya ilivyokuwa kabla, na kwa njia hiyo alifafanua kwamba, udhibiti wa silaha unazuia  na kukomesha vita, udhibiti ndio jibu kwa misingi yetu, ambapo anasema, uzinduzi huo wa ajenda umekuja kwa wakati udhibiti wa silaha umekuwa kama wimbo wa kila siku, kwa maana wakati mwingine kuhusu Iran na Siria, na siku nyingine kuhusu rasi ya Korea; lakini pamoja na hayo aliunga mkono juhudi za maendeleo endelevu kwa matarajio ya mshimano na ushirikiano katika kuunga mkono nchi zote duniani. 

Wamaharakati wengi wa kupinga silaha za kinyuklia ni wengi, wakiwemo hata Kanisa, kwa mfano Baraza la Makanisa ulimwenguni  Dr. Olav FykseTveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni alutuma ujumbe aliomwandikia Professa Klaus Schwab, Mwenyekiti mtendaji wa Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mwaka 2018, ambalo lilifunguliwa rasmi tarehe 22 -26 Januari 2018 baada ya kusikiliza mchango wa wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu ya binadamu. Dr. Tveit anawashauri wajumbe kushikamana katika mambo msingi yanayogusa mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa kwa kusimamia kikamilifu Mkataba wa Kimataifa wa kupiga marufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani.

Kadhalika aliandika nchi zinazotengeneza silaha za kinyuklia zinaendelea kutumia wastani wa dola za kimarekani billion 100 kwa mwaka kwa ajili ya kuzalisha silaha za kinyuklia. Ikumbukwe kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inahitaji kwa udi na uvumba rasimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu!  Kwa maana hiyo Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kupiga marufuku uzalishaji na usambazaji wa silaha za kinyuklia, ili kuondoa wasi wasi na hofu ya mashambulizi na hatimaye, mauaji ya alaiki ya watu. Lengo la kuendelea kutoa mwaliko huu ni kutaka kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwelekeo endelevu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu duniani dhidi ya wasi wasi wa mashambulizi ya silaha za kinyuklia.

 

29 August 2018, 16:48