Tafuta

Vatican News
Dunia kuna shida ya maji safi na salama ya kunywa kwa mujibu wa ripoti mpya katika wiki ya maji duniani Dunia kuna shida ya maji safi na salama ya kunywa kwa mujibu wa ripoti mpya katika wiki ya maji duniani  (AFP or licensors)

Ripoti:Shule nyingi duniani hazina maji safi na salama ya kunywa

Katika Wiki ya maji Duniani iliyoanza tarehe 26-31 Agosti, Ripoti mpya inasemakuwa ni asilimia 69 ya shule ulimwenguni kote hazina huduma ya maji ya kunywa, katika ripoti ya kwanza ya mashirika ya Umoja wa Mataifa UNICEF na WHO iliyoangazia makadirio ya upatikanaji wa maji ya kunywa, huduma za kujisafisha na usafi shuleni.

Sr. Angela Rwezaula- Vatican 

Je shule anayosoma mwanao ina huduma za maji ya kunywa na vyoo? Au je shule uliyosoma iwe  ya awali, msingi au sekondari ilikuwa na huduma hizo muhimu za msingi? Ripoti ya kwanza kabisa inayofuatialia huduma hizo inaonyesha hali mbaya na ya kusikitisha. Kuna shule za msingi hazina kabisa vyoo, maji wala huduma za kujisafisha.

Katika Wiki ya maji  duniani ikiwa ni siku ya pili ambayo ilianza tarehe 26Agosti na itamalizika tarehe 31 Agosti, imeelezwa kuwa asilimia 69 ya shule ulimwenguni kote hazina huduma ya maji ya kunywa, imesema ripoti ya kwanza ya mashirika ya Umoja wa Mataifa iliyoangazia makadirio ya upatikanaji wa maji ya kunywa, huduma za kujisafi na usafi shuleni.

Takwimu za ripoti hiyo imeripotiwa tarehe 27 Agosti 2018  na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF na lile la Afya dunainia, (WHO) zinaonyesha kuwa shule moja ya msingi kati ya nne haina kabisa huduma ya maji ya kunywa na hali inakuwa mbaya zaidi kwa shule za sekondari ambapo ni shule moja kati ya sita tu ndio yenye maji ya kunywa. Kwa upande wa vyoo, ripoti inasema, ni asilimia 66 tu ya shule ulimwenguni kote ndio zilikuwa na vyoo mwaka 2016 ambapo kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara pamoja na Pacific theluthi moja ya shule hazina kabisa vyoo.

Akizungumzia ripoti hiyo Kelly Ann Naylor, ambaye ni Mkuu wa huduma za maji, kujuisafisha na usafi UNICEF amesema iwapo elimu ni ufunguo wa kumsaidia mtoto kuondokana na umaskini, basi kupata maji safi, na huduma za kujisafisha ni ufunguo wa kumwezesha mtoto kunufaika zaidi na elimu. “Kupuuza hili ni kutojali ustawi na afya ya mtoto,” amesema Bi. Naylor.

Aidha Bi. Naylor amesema shule zinapokuwa na maji safi, vyoo na sabuni za kunawa mikono watoto wanakuwa na mazingira salama ya kujifunzia, na mahudhurio ya wanafunzi wa kike yanak uwa bora zaidi kwa kuwa wanaweza kufika shuleni hata wakati wa kipindi chao cha mabadiliko ya kila mwezi bila kuwa na hofu yoyote. Hata hivyo afisa huyo wa UNICEF amesema wanakabiliwa na kazi ngumu ya kuhakikisha kuwa fedha  zinaelekezwa katika ujenzi na ukarabati wa huduma za maji, usafi na kujisafisha kwenye shule zote za msingi na sekondari.

Ripoti hii imelenga kupima utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs namba 4  unao lihusu elimu na 6 la huduma za maji safi na kujisafisha.

Habari zaidi kuhusu wiki ya maji duniani kuanzia tarehe 26-31 Agosti 2018 unaweza kusoma katika tovuti zifuatazo http://www.worldwaterweek.org/;  www: http://www.siwi.org/ ; http://www.siwi.org/publications/world-water-week-programme-2018/

27 August 2018, 15:59