Rais Magufuli anawashukuru wote waliojitahidi kuokoa maisha ya Waziri Hamisi Kigwangalla aliyepata ajali tarehe 4.8.2018 Rais Magufuli anawashukuru wote waliojitahidi kuokoa maisha ya Waziri Hamisi Kigwangalla aliyepata ajali tarehe 4.8.2018 

Rais Magufuli awashukuru wote waliojitahidi kuokoa maisha ya Waziri wa Utalii

Rais Magufuli amemsifia Dr. Kigwangalla pamoja na wizara yake kwamba, wanaendelea kuchapa kazi barabara, na amewasihi watanzania kumwombea ili aweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli za ujenzi wa Taifa.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar es Salaam.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, Jumamosi, jioni alishiriki katika mapokezi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye alipata ajali wakati akiwa kazini. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wa Mkoa wa Arusha, Wizara ya Maliasili na Utalii, Madaktari pamoja na wale wote waliojitahidi kuokoa maisha ya Waziri Kigwangalla. Ni matumaini ya Rais Magufuli kwamba, Dr. Kigwangalla atapa matibabu muafaka kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jambo la msingi ni kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu. Rais Magufuli amemsifia Dr. Kigwangalla pamoja na wizara yake kwamba, wanaendelea kuchapa kazi barabara, na amewasihi watanzania kumwombea ili aweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli za ujenzi wa Taifa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali. Akiwa hospitalini hapo Jumapili, Agosti 5, 2018, Waziri Mkuu ambaye alikuwa ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa amesema amefarijika baada ya kumkuta Dkt. Kigwangalla na wagonjwa wengine waliolazwa katika hospitali hiyo wakihudumiwa vizuri. “Hospitali ya Muhimbili ndio kimbilio letu kwa sasa na tunawashukuru madaktari na wauguzi kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo inaliletea heshima Taifa letu kwani hata watu wa Comoro wanakuja kutibiwa Muhimbili,” amesema.

Kwa upande wake, Dkt. Kigwangalla amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ajali ilikuwa mbaya sana. “Ajali ilikuwa mbaya sana hivi sasa naongea hapa namshukuru Mungu, Serikali pamoja na madaktari na wauguzi kwa jitihada kubwa walizozifanya,”. Dkt. Kigwangalla alipata ajali Jumamosi, Agosti 4, 2018) katikati ya vijiji vya Mdolii na Minjingu wilaya ya Babati mkoani Manyara baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Hamza Temba na wengine watano akiwemo Dkt. Kigwangalla kujeruhiwa.

Pia Waziri Mkuu alimjulia hali msanii maarufu wa maigizo nchini, Bw. Amri Athumani maarufu King Majuto ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akipatiwa matibabu. Amesema amefarijika kumkuta akiwa anaendelea vizuri. Naye Mzee Majuto amesema anaishukuru Serikali kwa sababu inamuhudumia vizuri. “Mheshimiwa nakushukuru sana na naishukuru Serikali kwani hata sijui ingekuwaje kama si msaada wa Serikali. Hii ni bahati kubwa,”. Pia Waziri Mkuu amemjulia hali Bibi Hellena Baruti ambaye ni mama mzazi wa Mthamini Mkuu wa Serikali Bibi Evelyne Mugasha aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akipatiwa matibabu.

Habari zaidi zinabainisha kwamba, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kuchora ramani ya Tanzania katika Kijiji cha Makumbusho ambayo itatumika kwenye ujenzi wa nyumba za utamaduni wa makabila mbalimbali nchini. Amesema uamuzi huo utarahisisha watu kufika kwa urahisi katika nyumba za tamaduni za mikoa yao kwa kuwa watakuwa wanatumia ramani  ya Tanzania.

Waziri Mkuu aliyasema hayo Jumapili, Agosti 4, 2018 wakati akizungumza na wakazi wa mkoa wa Lindi kwenye kikao cha kujadili maandalizi ya Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania katika Kijiji cha Makumbusho, jijini Dar es Salaam. “Kwa kutumia ramani hii kila mkoa utaweza kufika kwenye eneo lake kwa kutumia ramani ya Tanzania na mkoa wa Lindi tayari umeshaoneshwa eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba inayozingatia utamaduni wetu,” alisema. Alisema kwa tamaduni za makabila ya mkoa wa Lindi nyumba zote hujengwa kwa udongo na kuezekwa kwa makuti upande wa maeneo ya pwani ya upande mwingine huezeka kwa nyasi, ambapo aina zote zitajengwa ili kuwakilisha tamaduni za wakazi wa mkoa huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaasa wananchi wa mkoa wa Lindi ambao kwa mwaka huu ndio waandaaji wa tamasha hilo wadumishe mshikamano wao ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea katika kuboresha maendeleo. Alisema katika tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuanza Agosti 26 hadi 29 wahakikishe wanapeleka kila kitu ambacho kinahusiana na utamaduni wa mkoa huo ili kuwawezesha Watanzania wengine wajue kama vyakula na mavazi .

Pia alishauri wawepo wazee wenye kujua historia ambao watasimulia utamaduni wa wananchi wa Lindi pamoja na kutambulisha ngoma zao za utamaduni. “Halmashauri zote za mkoa wa Lindi zitumie fursa hii kutangaza vivuti vya utalii vilivyopo na Kilwa walete mtu atakayeelezea kuhusu magofu,”. Waziri Mkuu alisema tamasha hilo ni muhumu kwa sababu utamaduni ulianza kufifia nchini kutokana  na mabadiliko ya kiteknolojia jambo ambalo lingeweza kuuondoa katika kumbukumbu, hivyo aliwashauri siku ya tamasha hilo wavae nguo za kitamaduni kulingana na kabila husika. Kadhalika, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi wa mkoa wa Lindi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Bw. Godfrey Zambi kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri mwenendo wa zao la korosho.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Profesa Audax Mabulla alisema mwaka huu Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania linawakilishwa na jamii kutoka mkoa wa Lindi na kwamba anatumaini watafanya vizuri kwa kuwa uwezo na nia wanayo. Profesa Mabula alisema mwaka 1994 Bodi ya Makumbusho ya Taifa ilianzisha siku ya utamaduni ili kutoa fursa kwa jamii mbalimbali nchini kuonesha utajiri walionao katika tamaduni zao na ufanisi wa siku hiyo unatokana ushirikishwaji wa wanajamii husika.

 

06 August 2018, 11:45