Tafuta

Vatican News
Kwa mujibu wa Tamko la Umoja wa Mataifa, tarehe 12 Agosti ya kila mwaka ni Siku ya Vijana Duniani Kwa mujibu wa Tamko la Umoja wa Mataifa, tarehe 12 Agosti ya kila mwaka ni Siku ya Vijana Duniani 

Nafasi salama kwa vijana ni mada ya Siku ya Vijana Duniani !

Kila nchi duniani imeweza kuadhimisha siku ya Vijana duniani tarehe 12 Agosti kwa kujikita katika ubunifu wa matukio mbalimbali au shughuli katika mashule, jumuiya, vyama au katika kazi mbalimbali. Kwa kauli mbiu ya mwaka 2018, siku imeongezwa na nafasi salama kwa vijana kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa!

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Imeadhimishwa Siku ya Vijana Duniani tarehe 12 Agosti kama ilivyokubaliwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo kwa mwaka 2018 imeongozwa na kauli mbiu “Safe Spaces for Youth”,  yaani nafasi salama kwa vijana. Kila nchi duniani imeweza kuadhimisha siku hii ya Vijana kwa kujikita katika ubunifu wa matukio mbalimbali au shughuli katika mashule, jumuiya, vyama au katika kazi mbalimbali.

Umuhimu wa kuhusisha vijana kikamilifu katika masuala ya uongozi.

Vijana nchini Uganda ikiwemo wakimbizi wanahisi kwamba hawajapewa nafasi na fursa muafaka za kutimiza ndoto zao. Jumuiya ya kimataifa imeadhimisha siku ya vijana tarehe 12 Agosti  2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu ya nafasi salama kwa vijana. Fasili ya kaulimbiu hii ni kwamba wakati umewadia kwa vijana kuwezeshwa na kushirikishwa katika nafasi za uongozi ili kupata si tu jukwaa la kuwasilisha maoni yao, lakini pia kuhusishwa katika kutoa maamuzi kuhusu hali yao sasa na siku za usoni.

Kwa mujibu wa kauli mbiu ya mwaka huu 2018 ya siku ya vijana, dhana ya nafasi salama kwa vijana inaangazia uwezeshaji kwa vijana kupewa motisha ya kutimiza maslahi yao. Hii ina maana kuwa wakijenga uwezo wa kutoa maoni yao, kufanya maamuzi yanayohusu hali yao ya sasa na pia mustakabali wao katika mazingira ambapo hadhi yao inaheshimiwa, basi watajenga hisia chanya kushiriki katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Changamoto ya kutopewa nafasi na ukosefu wa ajira.

Vijana nchini Uganda wakiwemo wakimbizi wanahisi kwamba hawajapewa nafasi na fursa muafaka za kutimiza ndoto zao. Ila wana mtazamo kuwa viongozi wa kisiasa huwatumia tu kwa ajili ya maslahi yao badala ya kuwahusisha moja kwa moja katika kubuni mikakati ya kuwa na jumuiya inayotambua kuwa vijana ndiyo nguvu na mhimili mkubwa wa nchi. Vijana wana mtazamo kuwa changamoto kubwa kwao ni ukosefu wa nafasi za kazi hata baada ya idadi yao kubwa kukamilisha elimu ya juu. Aidha kuna hoja ya elimu wanayopokea vijana kutowawezesha kupata maarifa na stadi zinazohitajika na waajiri.

Changamoto za teknolojia

Kwa maoni ya baadhi ya vijana, teknolojia pia inazidi kuwa tishio kwao kwani waajiri wanapendelea kuwekeza katika mbinu na mitindo inayorahisisha kazi. Lakini kuna mtazamo kuwa vijana wajizatiti na kuwa wabunifu ili wasikose fursa za teknolojia kujenga mazingira ya ujasiriamali badala ya kusubiri kuajiriwa. Vijana wakimbizi nao wanataka wasisahalike lakini kuwepo na mipango ya kuwahusisha katika mazungomzo ya kuleta amani katika nchi zao!

16 August 2018, 16:06