Tafuta

Familia ya Mungu nchini Argentina imekataa kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba! Familia ya Mungu nchini Argentina imekataa kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba! 

Wananchi wa Argentina wakataa kukumbatia utamaduni wa kifo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, linawashukuru wananchi wote waliosimama kidete: kutangaza, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa namna ya pekee, maskini hata katika umaskini wao, wameonesha jeuri ya kutaka kuendeleza maadili na utu wema, daima wakimpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wabunge wa Seneti ya Argentina, hivi karibuni, wametupilia mbali muswada wa sheria uliotaka kuhalalisha utamaduni wa kifo unaokumbatia utoaji mimba na kwamba, hili litaendelea kuwa ni kosa la jinai nchini Argentina, sheria iliyopitishwa kunako mwaka 1921. Kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia, atafungwa jela kwa muda wa miaka mine. Waamini wa Makanisa mbali mbali wamefunga na kusali, ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kupishilia mbali mawazo ya baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuchezea haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa ajili ya mafao yao binafsi katika mambo ya kisiasa.

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Argentina, linasema, kwa sasa changamoto kubwa mbele ya familia ya Mungu nchini Argentina ni kuhakikisha kwamba, watangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; pamoja na kuendelea kuhimiza umuhimu wa kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kifamilia katika maisha ya wananchi wa Argentina. Kanisa linapaswa kuwa karibu zaidi na wanawake pamoja na familia zinazokabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha, ili kuzitangazia Injili ya matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, linawashukuru wananchi wote waliosimama kidete: kutangaza, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa namna ya pekee, maskini hata katika umaskini wao, wameonesha jeuri ya kutaka kuendeleza maadili na utu wema, daima wakimpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele katika maisha yao! Maaskofu wanakaza kusema, kwa hakika, maskini ni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa.

Wachunguzi wa mambo wanasema, muswada wa Sheria ya kutoa mimba nchini Argentina, limekuwa ni jukwaa la majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa, ili kudumisha uekumene wa damu, unaofumbatwa kwa namna ya pekee, katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha anakaza kusema, Kanisa kwa kushirikiana na watu wenye mapenzi mema waendelee kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai inayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuenzi Injili ya familia, Habari Njema kwa watu wa ulimwengu mamboleo.

Upendo, ukarimu, huruma na ukaribu kwa watu wanaosumbuka ni dhamana nyeti sana kwa Kanisa nchini Argentina. Wananchi wajenge utamaduni wa kupenda na kuthamini uhadi wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa familia ambazo zinakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha, Kanisa halina budi kuzisindikiza familia hizi, ili hatimaye, ziweze kuona mwanga katika maisha na utume wao pasi na kukata tamaa! Kuna watu ambao wanataka kuneemeka kwa kutumia matatizo na changamoto za maskini kwa kuwatumbukiza watu katika utamaduni na ombwe la kifo!

 

 

 

10 August 2018, 15:30