Siku ya Nelsona Mandela Kimataifa Siku ya Nelsona Mandela Kimataifa 

Siku ya Nelson Mandela Kimataifa 2018: Mapambano dhidi ya umaskini duniani.

Maadhimisho ya Siku ya Nelson Mandela Kimataifa kwa Mwaka 2018 yamekwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka 100 tangu alipozaliwa. Ni kiongozi anayeheshimiwa duniani kutokana na moyo wake wa kusamehe na kusahau, ili kuandika ukurasa wa umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu wote pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Frsancisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii mwaka 2017 alisema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuvuka mifumo yote ya ubaguzi, hali zote za kutovumiliana pamoja na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu! Baba Mtakatifu aliandika ujumbe huu wakati Umoja wa Mataifa ulipokuwa unaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2009 na kuanza kuadhimishwa rasmi tarehe 18 Julai 2010 kama njia ya kumuenzi Mzee Nelson Mandela aliyejisadaka kwa ajili ya kupigania uhuru, haki msingi za binadamu na demokrasia ya kweli inayowaambata wananchi wote wa Afrika ya Kusini. Ni kiongozi aliyesimama kidete, kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, vitendo ambavyo vilidhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Siku ya Nelson Mandela Kimataifa kwa mwaka huu 2018 yamekwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka 100 tangu alipozaliwa! Kiongozi anayeheshimiwa sana duniani kutokana na moyo wake wa kusamehe na kusahahu, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu! Mwaka 2018, Jumuiya ya Kimataifa imeamua kumuenzi Mzee Madiba kwa kujikita katika mapambano dhidi ya balaa la umaskini pamoja na kujielekeza zaidi katika utekelezaji wa haki jamii kwa watu wote.

Mheshimiwa George Johanness, Balozi wa Afrika ya Kusini mjini Vatican anasema, kati ya mambo ambayo Mzee Nelson Mandela aliwahi kumuasa ni uadilifu katika masuala ya kisiasa pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu anaowaongoza, bila kusahau historia ya maisha na mapito yake. Alimkumbusha kwamba, uongozi wa kisiasa na unafasi kubwa sana katika jamii, kumbe, changamoto iwe ni kwa ajili ya: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Mandela Kimataifa anasema, Mzee Mandela alikuwa ni kiongozi aliyeragibisha haki na usawa na hivi kubwa ni mfao bora kwa Jumuiya ya Kimataifa katika kushuhudia ujasiri, wema na huruma. Mzee Mandela alifungwa na kutimikia adhabu ya kifo kwa miaka mingi, lakini, kamwe hakubaki kuwa ni mtumwa wa historia yake ya zamani na badala yake, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuanzisha mchakato wa haki, amani na upatanisho Afrika ya Kusini; akaonesha dira na mwelekeo wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa Afrika ya Kusini, kiasi cha kuvunjilia mbali kuta za ubaguzi wa rangi zilizowakandamiza wananchi wengi Afrika ya Kusini.

Leo, hii, Afrika ya Kusini, imecharuka katika demokrasia na maendeleo endelevu na fungamani kwa watu wake. Jumuiya ya Kimataifa, katika maadhimisho ya Miaka 100 tangu Mzee Nelson Madiba Mandela alipozaliwa, huduma yake inakumbukwa sana! Si rahisi sana katika ulimwengu kupata watu ambao wanakuwa ni changamoto kubwa kwa jamii kuota ndoto ya pamoja na kuimwilisha katika matendo. Urithi mkubwa wa Mzee Mandela kwa Jumuiya ya Kimataifa ni uwezo wake wa kusimama kidete na kupigania: usawa, utu, heshima na haki, mambo ambayo bado yanaendelea na kwamba, hii ni amana kubwa kutoka kwa Mzee Madiba.

Mzee Mandela aliwahi kusema, ni rahisi sana kuweza kuvunjilia mbali mifumo ya kibaguzi, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, jamii inaunda mashujaa watakaojifunga kibwebwe usiku na mchana ili kulinda, kutetea na kudumisha haki na amani duniani.  Leo hii dunia imegawanyika na kusambaratika sana kutokana na sababu mbali mbali, inahitaji mashuhuda na wajumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Jamii inawahitaji mashujaa watakaoweza kusimama kidete kupambana na changamoto zinazowakabili vijana wa kizazi kipya wanaotangatanga kama daladala zilizokatika usukani kwa kukosa ajira, maadili na utu wema; watu watakaoweza kupambana na ukosefu wa haki na amani, ili kujenga utamaduni wa maridhiano kati ya watu sanjari na kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kwa kutekeleza yote haya, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa kweli inaendelea kumuenzi Mzee Nelson Mandela.

Sikiliza

 

18 July 2018, 08:18