Tafuta

Vatican News
Nyanyaso za kijinsia zinadhalilisha maisha na utume wa Kanisa. Nyanyaso za kijinsia zinadhalilisha maisha na utume wa Kanisa.  (AFP or licensors)

Nyanyaso za kijinsia ni dalili za kumong'onyoka kwa maadili.

Kashfa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zinapotokea ndani ya Kanisa, haitoshi tu kwa wahusika kuomba radhi, bali Kanisa kuchukua hatua za kinidhamu mara moja, ili kuhakikisha kwamba, kashfa za namna hii hazijirudii tena ndani ya Kanisa anasema Kardinali Seàn Patrick O'Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya kulinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Nyanyaso za kijinsia ni vitendo ambavyo kamwe haviwezi kukubalika kimaadili na ikiwa kama vitendo hivi vinafanywa na watu wenye dhamana katika uongozi wa Kanisa, vinakera na kuudhi sana, kwani vinakwenda kinyume kabisa cha dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kashfa kama hizi zinapotokea ndani ya Kanisa, haitoshi tu kwa wahusika kuomba radhi, bali Kanisa kuchukua hatua za kinidhamu mara moja, ili kuhakikisha kwamba, kashfa za namna hii hazijirudii tena ndani ya Kanisa.

Hii ni sehemu ya tamko lililotolewa hivi karibuni na Kardinali Seàn Patrick O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, PCPM, iliyoundwa mwezi Machi 2014 na Baba Mtakatifu Francisko. Shutuma za nyanyaso za kijinsia zinazowakabili viongozi wa ngazi za juu wa Kanisa nchini Marekani zinaonekana kuwa na uzito na kwamba, zimesababisha kuchafuka tena kwa hali ya amani na utulivu miongoni mwa familia ya Mungu ndani na nje ya Marekani. Kardinali O’Malley anasema, kila mara kunapoibuka shutuma kama hizi, Kanisa linapaswa kuwa makini zaidi kutambua kwamba, hapa kuna mapambano makubwa dhidi ya kumong’onyoka kwa maadili na utu wema.

Katika mazingira kama haya, Kanisa linapaswa kuendelea kujizatiti zaidi katika kutekeleza sera na mbinu mkakati ambayo imetungwa hivi karibuni ili kuweza kukabiliana na kashfa za nyanyaso ndani ya Kanisa kwa kuunda mazingira ya ulinzi na usalama kwa malezi na makuzi ya watoto wanaokuwa katika mazingira ya Kanisa. Ukweli na uwazi katika kesi hizi ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba, haki inatendeka kwa wale wote wanaohusika. Kanisa liendelee kutoa umuhimu wa pekee katika kushughulikia kesi hizi, kwani wakati mwingine ni matokeo ya matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Kanisa.

Katika mazingira kama haya, watu wa kwanza kupewa uzito wa pekee ni waathirika, familia, ndugu na jamaa zao. Wale waliosababisha kashfa hizi, wachukuliwe hatua za kinidhamu, lakini pia kwa kuheshimu utu na haki zao msingi. Hizi ni changamoto ambazo zinaanza kuibuliwa na watu baada ya muda mrefu kupita, kumbe, umakini unahitajika sana, ili kushughulikia kesi hizi, kwani kuna baadhi ya watu wameamua kuchafua majina ya viongozi wa Kanisa kwa sababu zao binafsi.

Kanisa halina budi kutenda kwa haraka zaidi; kupembua na kuangalia sera na mikakati ya ulinzi kwa watoto wadogo na hasa kwa Maaskofu pamoja na kuwahabarisha waamini katika ukweli na uwazi jinsi ya kuwasilisha kesi za nyanyaso za kijinsia zinazowagusa na kuwapekenya viongozi wa ngazi za juu Kanisani. Kushindwa kutekeleza mambo haya msingi kutalidhohofisha na kuliondolea Kanisa nguvu yake ya kimaadili katika maisha na utume wake. Kwa sasa, Kanisa linapaswa kushughulikia kashfa hizi, dhamana ambayo Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, PCPM inatarajia kuichambua katika mkutano wake ujao.

Pamoja na mambo mengine, Tume hii inatoa mwongozo wa kuwalinda watoto wadogo; mchakato wa uponyaji kwa watu walioathirika na nyanyaso za kijinsia; malezi na majiundo makini kwa Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu, Watawa pamoja na viongozi wa Kanisa katika masuala ya elimu. Tume hii ina dhamana ya kutoa elimu kwa familia na jumuiya za Kikristo, kwa kujikita katika taalimungu na tasaufi; sheria za Kanisa pamoja na sheria za kiraia.

Tume inasema, kwa sasa inapenda kujielekeza katika mchakato wa malezi na majiundo makini mintarafu ulinzi wa watoto wadogo wanaoweza kufanyiwa nyanyaso za kijinsia. Tume itaendelea na mchakato wa uponyaji kwa kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso hizi! Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, dhambi ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni dhambi inayotisha na kwenda kinyume kabisa cha mafundisho ya Kristo, utu na heshima ya binadamu! Kanisa litawashughulikia bila huruma wale wote watakaojihusisha na vitendo hivi!

Nyanyaso za kijinsia

 

27 July 2018, 17:14