Tafuta

Vatican News
Vatican imeamua kufungua ubalozi wake nchini Sudan ya Kusini. Vatican imeamua kufungua ubalozi wake nchini Sudan ya Kusini.  (ANSA)

Vatican yafungua ubalozi mpya Sudan ya Kusini!

Familia ya Mungu Kusini mwa Sudan inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kufungua Ubalozi mpya wa Vatican Kusini mwa Sudan, ushuhuda makini kwamba, kwa hakika Baba Mtakatifu anaguswa na mahangaiko, mateso na matumaini ya watu wa Mungu Kusini mwa Sudan.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Askofu Barani Eduardo Hiiboro Kussala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan anapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kuonesha jicho la pekee kwa familia ya Mungu Sudan ya Kusini, mahali ambako: vita, njaa, ujinga na umaskini unaendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu kwa kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini, ili kuonesha uwepo wa karibu ameamua kuanzisha Ubalozi wa Vatican Kusini mwa Sudan, utakaokuwa na makao yake makuu mjini Juba. Monsinyo Marco Kedima kutoka Jimbo Katoliki la Kakamega nchini Kenya, ameteuliwa kuwa mshauri wa Ubalozi wa Vatican huko Sudan ya Kusini.

Sudan ya Kusini, ilijipatia uhuru wake kunako mwaka 2011 baada ya kupiga kura ya maoni. Vatican kwa kutambua umuhimu wa kukuza na kudumisha mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu, ikamteua Askofu mkuu Charles Daniel Balvo kuwa Balozi wa Kenya na Sudan ya Kusini. Viongozi wa Kanisa daima wameonesha jicho la pekee kabisa kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini na kwamba, Serikali ya Sudan ya Kusini pamoja na mambo mengine, inapania kulinda na kudumisha ustawi, mafao na maendeleo ya waamini wa dini mbali mbali nchini humo.

Hatua hii iliyochukuliwa na Baba Mtakatifu Francisko itasaidia kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Sudan ya Kusini, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu. Askofu Barani Eduardo Hiiboro Kussala anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko si mtu wa maneno maneno tu, bali ni mtu anayemwilisha maneno yake katika matendo. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutoka katika ubinafsi na uchoyo na kuanza hija ya kuwaendea jirani zao za huruma, upendo na msamaha. Ni kiongozi ambaye amefaulu kugusa akili na nyoyo za watu mbali mbali kwa mfano wa maisha na utume wake; kwa kuwajali na kuwatetea maskini na wanyonge katika jamii; kwa kuwachangamotisha watu kuvunjilia mbali kuta za utengano, vita na kinzani na hivyo kuanza kujenga madaraka yanayowakutanisha watu; kwa kuheshimiana, kupendana na kushikamana kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro bado anayo nia ya dhati kabisa kutembelea Sudan ya Kusini, ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini ya kuwa na Sudan ya Kusini mpya inayojikita katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu! Upendo wa Baba Mtakatifu kwa Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini hauna mipaka! Hii ni chachu na mwaliko kwa familia ya Mungu katika nchi hizi kuondokana na falsafa ya: vita, chuki na kinzani na kuanza kuambata mchakato wa toba na wongofu wa ndani; haki, amani na upatanisho. Hakuna sababu ya wananchi wa Sudan ya Kusini kukata wala kukatishwa tamaa, bali kuendelea kuwa na matumaini ya ujenzi wa Sudan ya Kusini mpya na panapo majaliwa, siku moja, Khalifa wa Mtakatifu Petro ataweza kutembelea Sudan ya Kusini! Mtakatifu Josephine Bakhita, simamia na kuwaombea ndugu zako: haki, amani na utulivu!

 

08 June 2018, 16:11