Maadhimisho ya Juma la Chanjo Duniani 24-30 Aprili 2018 Maadhimisho ya Juma la Chanjo Duniani 24-30 Aprili 2018 

Juma la Chanjo Duniani: 24-30 Aprili 2018

UNICEF linasikitika kwamba, katika kipindi cha mwaka 2016 watoto milioni 1.4 chini ya umri wa miaka mitano walifariki dunia kutokana na magonjwa ambayo yangeweza kuzuiliwa kwa kutumia chanjo. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watoto milioni 19 wenye umri kati ya mwaka 1 hadi miaka 7 hawakufaulu kupata chanjo dhidi ya magonjwa mbali mbali katika kipindi cha mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. -Vatican.

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, katika maadhimisho ya Juma la Chanjo Duniani, kuanzia tarehe 24-30 Aprili 2018, linasikitika kusema kwamba, katika kipindi cha mwaka 2016 watoto milioni 1.4 chini ya umri wa miaka mitano walifariki dunia kutokana na magonjwa ambayo yangeweza kuzuiliwa kwa kutumia chanjo. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, zaidi ya watoto milioni 19 wenye umri kati ya mwaka 1 hadi miaka 7 hawakufaulu kupata chanjo dhidi ya magonjwa mbali mbali katika kipindi cha mwaka 2016.

Hadi sasa kuna watoto zaidi ya milioni 13 ambao hawajahi kupata chanjo kabisa katika maisha yao! Watoto wengi wamepoteza maisha kutokana na magonjwa ya mapafu, kuhara pamoja na surua; magonjwa ambayo watoto wanaweza kukingwa kwa kutumia chanjo. Takwimu za Kimataifa zinaonesha kwamba, mtoto mmoja kati ya watoto saba duniani, ambao jumla yao inakadiriwa kuwa ni milioni 13, hawajawahi kupata chanjo katika maisha, hali inayowaweka watoto hawa pamoja na ndugu zao katika hatari ya kuambukizwa magonjwa na hatimaye kupoteza maisha. Watoto wanaotoka katika familia na nchi maskini zaidi ndio waathirika wakuu na hili ni kundi ambalo si rahisi sana kupatiwa chanjo kuzuia magonjwa!

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, linasema, kwa njia ya chanjo katika kipindi cha mwaka 2017, zaidi ya watoto milioni tatu waliokolewa dhidi ya kifo. Wazazi na walezi wa watoto wanahimizwa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwapatia watoto wao chanjo ya kuzuia magonjwa mbali mbali. Bila chanjo, maisha ya watoto wengi yako hatarini. Nigeria, Ethiopia, DRC, India na Pakistani ni kati ya nchi ambazo watoto wengi hawana nafasi ya kupata chanjo.

 

24 April 2018, 14:10