Cerca

Vatican News
Rais Sergio Mattarella wa Italia anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Rais Sergio Mattarella wa Italia anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.  (Vatican Media)

Rais Sergio Mattarella ampongeza Papa Francisko kwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mt. Petro.

Rais Sergio Mattarella wa Italia, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia amemtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Anamtakia heri na mafanikio mema katika kuliongoza Kanisa Katoliki na familia ya Mungu katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Machi 2018 ameadhimisha kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na kuamua kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira! Baba Mtakatifu ameitumia siku hii kwa kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoshiriki katika utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana. Jioni, Baba Mtakatifu katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliwaweka wakfu Maaskofu wakuu watatu, ambao amewakumbusha kwamba, kazi na dhamana ya kwanza ya Askofu licha ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu ni kusali na kumwilisha sala hii katika maisha na utume wa Kanisa!

Rais Sergio Mattarella wa Italia, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia amemtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Anamtakia heri na mafanikio mema katika kuliongoza Kanisa Katoliki na familia ya Mungu katika ujumla wake. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro mintarafu mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya upatanisho, haki na amani duniani.

Rais Mattarella anampongeza Baba Mtakatifu kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwatangazia na kuwashuhudia Injili ya matumaini. Yote haya yanajionesha katika hija za kitume ambazo Baba Mtakatifu Francisko ametekeleza Barani Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na Ulaya. Rais Mattarella anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa upendeleo wa pekee kwa familia ya Mungu nchini Italia, daima anapenda kuyaangalia matatizo, changamoto na fursa za watu wa Mungu nchini Italia, kwa jicho na upendo wa kibaba. Rais Sergio Mattarella ana mshukuru kwa hija zake za kichungaji ambazo amezifanya nchini Italia kama sehemu ya mchakato wa kuwaimarisha ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini. Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2018 iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha safari ya ujenzi wa misingi ya uhuru, haki na amani!

 

19 March 2018, 14:38