Tafuta

FAo imemwalika Papa Francisko kuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2017 FAo imemwalika Papa Francisko kuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2017 

Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2017: Papa Francisko amealikwa kuwa mgeni rasmi.

Mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni kati ya changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030. Takwimu zinaonesha kwamba, baa la njaa linaongezeka duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililotolewa kwake na Professa Josè Graziano da Silva Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kutembea Makao makuu ya FAO yaliyoko mjini Roma, Jumatatu, tarehe 16 Oktoba 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2017. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Kubadili mwelekeo wa wahamiaji”. Huu ni Mpango mkakati wa kupambana na hatimaye kulipatia kisogo baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani ifikapo mwaka 2030.

Hii inatokana na ukweli kwamba, idadi ya watu wanaokumbwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kadiri ya takwimu za mwaka 2016 imeongezeka kwa asilimia 11%, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika kipindi cha mwaka 2015. Kwa sasa kuna zaidi ya watu 800 milioni wanaoteseka kutokana na baa la njaa, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa mwaka 2016, kwani idadi yao ilikuwa walau imefikia watu milioni 777. Waathirika wakuu ni watoto na wanawake sehemu mbali mbali za dunia. Taarifa zinazonesha kwamba, baadhi ya watu katika nchi zinazoendelea duniani wanakumbwa na uzito wa kupindukia kutokana na kula vibaya.

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wameanza kutafakari kwa kina na mapana changamoto endelevu kuhusu masuala ya usalama wa chakula duniani; athari za mabadiliko ya tabianchi; changamoto katika sekta ya kilimo pamoja na mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Wajumbe wa mkutano wanaendeelea kupembua na hatimaye, kuridhia mpango mkakati wa FAO kwa Mwaka 2018 – 2019. Jumuiya ya Kimataifa inataka kulivalia njuga tatizo la ukame ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa ni janga kubwa kwa watu wengi Barani Afrika.

Baa la njaa linakuzwa pia kutokana na vita, kinzani, ghasia na migogoro ya kijamii inayoendelea huko: Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini. Jumuiya ya Kimataifa inataka kupambana kikamilifu na baa la njaa duniani, ili hatimaye, kulitokomeza kabisa kwa kuwekeza katika usalama wa chakula sanjari na kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nalo ni changamoto kubwa katika kukabiliana na uhakika wa usalama wa chakula na lishe duniani!

 

14 October 2017, 15:36