Papa Francisko amemteua Pd.Romanus Elamu Mihali kuwa Askofu mpya wa Iringa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumanne tarehe 28 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko amepokea barua ya maombi ya kung’atuka kutoka katika shughuli za kichungaji kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Iringa nchini Tanzania yaliyowakilishwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa baada ya kufikisha umri wake wa kustaafu, na wakati huo huo, Baba Mtakatifu akamteua Askofu Mpya wa Jimbo hilo Mhes, Padre Romanus Elamu Mihali, wa jimbo la Mafinga ambaye hadi uteuzi wake alikuwa Makamu Askofu wa Jimbo la Mafinga na Paroko wa Ujewa.
Wasifu
Padre Mihali alizaliwa tarehe 10 Juni 1969 huko Itulituli, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa. Mara baada ya majiundo yake ya Falasafa na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Songea, alipewa daraja takatifu la Upadre kunako tarehe 13 Julai 2000 kwa ajili ya jimbo la Iringa.
Nyadhifa
Ameshikilia nyadhifa mbali mbali na kuendelea na masomo zaidi kama: Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume huko Ilula, Iringa (2000-2003); Mlezi na Mkufunzi wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Kizito, Mafinga(2003-2005); Masomo ya Uzamili wa Sayansi katika Sayansi ya fani ya wanyama na kupata Shahada yake katika Chuo Kikuu cha Kerala nchini India (2005-2011); Paroko Msaidizi wa Bikira Maria wa Fatima huko Usomaki, Iringa (2012-2015); Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa, Ujewa Iringa (2015-2024).
Baada ya kusimikwa jimbo la Mafinga kunako 2024 kwa kupata hata Askofu mpya wa Jimbo hilo, Padre Romanus alipewa nafasi ya kuwa Makamu Askofu wa Jimbo hilo la Mafinga na Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa (Mafinga) hadi uteuzi huu.
Askofu Mstaafu Tarcisius Ngalalekumtwa ataendelea kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Iringa hadi Askofu pale Askofu Mteule atakapowekwa wakfu wa kiaskofu kwa ajili ya jimbo hilo hilo.