Tafuta

2025.01.31 Lila Azam Zanganeh 2025.01.31 Lila Azam Zanganeh  (copyright: Hank Gans © 2025)

Msichana mdogo katika kizingiti

Lila Azam Zanganeh ni mwandishi na mzaliwa wa Iran na uzoefu wa Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano

Na Andrea Tornielli


“Nilijihisi kama msichana mdogo aliyekaribishwa katika nyumba ambayo pia inaweza kuwa yake...” Lila Azam Zanganeh alizungumza kwa maneno mengi yenye hamasa, ambayo hakuna hata moja ambalo linahisi kuwa halihitajiki. Macho yake makubwa meusi yanamfanya msikilizaji wake, kana kwamba anasoma mioyo yao. Alizaliwa Paris kwa wazazi wa kutoka Iran, alisoma fasihi na filamu huko Harvard, na anaishi kati ya Roma, Paris, na New York, na anazungumza lugha saba. Yeye ni mwanamke wa ulimwengu anayejua ulimwengu, na mama wa mtoto wa miaka miwili. Katika siku za hivi karibuni, alishiriki katika Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano pamoja na wajumbe wengine wa Narrative 4, shirika lisilo la faida lililoanzishwa na mwandishi Colum McCann ili kuhamasisha huruma na kuelewana kupitia kushiriki historia za kibinafsi.

“Kuhudhuria Jubilei,” alisema kwa hisia, “huenda lilikuwa mojawapo ya matukio muhimu zaidi maishani mwangu, pamoja na kuzaliwa kwa mtoto wangu miaka miwili iliyopita. Nilizaliwa Paris, na mama yangu Mwiran alikuwa amesoma shule za Kikatoliki huko Tehran. Tangu utotoni, alinijengea imani iliyo wazi sana. Nilisoma katika shule ya Kikatoliki. Lakini hakuna mtu aliyewahi kuniambia kwamba mimi si Mkatoliki!” Lila alipokuwa na umri wa miaka tisa, “aligundua” kwamba hangeweza kupokea Kumunio ya kwanza kwa sababu hakuwa amebatizwa. Na kulingana na sheria, ingemlazimu kusubiri hadi alipokuwa na umri wa miaka kumi na tano ili abatizwe.

“Nakumbuka nilihudhuria katekisimu huko Ufaransa. Siku moja, nikiwa darasani, niliuliza swali: ‘Kwa nini Kristo pekee ndiye Mwana wa Mungu? sisi sote si watoto wa Mungu?’ Katekista—labda akitaja jina langu la mwisho—alijibu, ‘Ukisema mambo kama hayo, wewe sio wa hapa.’” Ilikuwa kumbukumbu chungu. “Lakini, kwa muujiza fulani na labda shukrani kwa imani ya mama yangu, niliendelea kuwa na uhusiano wa kina sana na Ukristo. Unaweza kufikiria hisia zangu baada ya kuwasili kwenye Jubilei.” Lila daima amekuwa anafuata ushuhuda wa Papa kwa umakini na mshangao. “Padre mmoja kutoka Amazonia aliniambia wakati fulani, ‘Pamoja na Papa huyo, kuna sheria ya moyo, na moyoni mwako, wewe tayari ni Mkristo. Niliguswa sana na maono ya Francisko, msisitizo wake kwamba lazima twende ulimwenguni kushirikisha ujumbe wa Yesu. Nilishangaa sana aliposema juu ya Mungu ambaye anabisha, si kuingia, bali kutoka na kuwafikia kila mtu.”

Siku ya Ijumaa, tarehe 24 Januari, kitendo cha kwanza cha Jubilei ya Wawasilianaji kilikuwa ni mkesha wa toba huko Mtakatifu Yohane, Laterano. “Mara nyingi mimi uhudhuria Misa, ingawa ninajua kwamba ‘kitaalam’ mimi si Mkatoliki,” alikiri hilo. “Na ninaweza kusema kwamba huduma ya kiliturujia niliyoshiriki huko Laterano ilikuwa nzuri zaidi ambayo nimewahi kuona. Wakati tuliambiwa kwamba mapadre sitini walikuwa wanapatikana kwa ajili ya kuungamisha. Rafiki yangu kutoka Narrativ 4, Rosa, ambaye ni Mkatoliki sana, mara moja alikwenda kuungama. Aliporudi, nilimuuliza ikiwa ilikuwa uzoefu mzuri. Alijibu, 'Sana.' Nilimwambia, 'Mimi si Mkatoliki kabisa... unafikiri ninaweza kwenda pia kwa uhakika sana kuhusu mambo haya, kwa hiyo nilitarajia aseme, 'Hapana! ’ Badala yake, alisema, ‘Ndiyo, unaweza kwenda.’”


Lila, msichana mdogo ambaye alitamani sana kupata komunio, lakini hakuweza kuupokea kwa sababu hakuwa amebatizwa, alisimama na kumwendea mmoja wa mapadre waungamishi. “Nilisimama kwenye mstari wa waungamaji waliokuwa wanazungumza Kifaransa. Nilipofika kwa Padre wa Congo, jambo la kwanza nililosema lilikuwa, ‘Baba, dhambi yangu ya kwanza ni kwamba mimi si Mkatoliki. Lakini nina imani ya Kikristo moyoni mwangu.’ Yeye akajibu, ‘Sisi sote ni wenye dhambi, na mnakaribishwa katika nyumba ya Mungu.’ Kisha akaanza kusali. Ilikuwa ni wakati mzuri sana kwamba nilianza kulia, lakini kutokana na furaha. Aliniambia mambo ya ajabu.
Alinialika kukaa na kushikamana na Roho Mtakatifu, na tulizungumza juu ya upendo, ambao wakati mwingine husababisha kukata tamaa. Aliniambia kwamba wengine daima ni sehemu yetu na akanikumbusha amri ya upendo. Nililia machozi ya furaha, na mwishowe, nilicheka na kumshukuru kwa sababu lilikuwa jambo lenye kufurahisha sana.”

Siku ya Jumatatu asubuhi yaani (27 Januari 2025), wakati wa Mkutano na kikundi cha wawasilianaji, Lila alipata fursa ya kukutana na Papa Francisko ana kwa ana na kushirikisha sehemu ya historia yake. “Alinitazama na kunitia moyo niendelee na kuwa na ujasiri. Hata muungamishi wangu wa Kikongo alikuwa ameelewa roho ya Papa ya uwazi huu wa ajabu, kama mtu ambaye yuko nje na ndani kwa wakati mmoja, anayesukumwa mbele kila wakati.” Na hivyo, katika kukumbatia Jubilei na wakati huo katika kuungama, Lila alijisikia kama msichana mdogo ambaye bado amesimama juu ya kizingiti, na bado kukaribishwa katika nyumba ambayo inaweza kuwa yake. Anasimama kwenye kizingiti, kama vile mwandishi mkuu wa Kifaransa Mkatoliki Charles Péguy, ambaye aliandika kurasa za kina na imani isiyosahaulika ambayo bado hakuweza kupokea sakramenti katika maisha yake yote kwa sababu alikuwa ameoa kiserikali na mwanamke asiyeamini Mungu na alikuwa na watoto watatu ambao hakuwabatizwa. Akitafakari juu ya miaka mitatu ya maisha ya Yesu kwa umma Péguy aliandika:

“Hakutumia kunung’unika au kulaumu ubaya wa nyakati… Hakushtaki, hakumhukumu mtu yeyote. Aliokoa. Hakuamuru ulimwengu. Aliokoa ulimwengu. Wengine, hata hivyo, wanashutumu, wanasababu, na kuamuru, kama vile madaktari wenye hasira wanaomkaripia mgonjwa. Wanalaumu mchanga wa nyakati, lakini hata katika siku za Yesu, kulikuwa na enzi na mchanga wao. Lakini kwenye mchanga huo mkavu, kwenye mchanga wa uzee, chemchemi isiyoisha ilitiririka—chemchemi ya neema.” Neema hiyo hiyo sasa inang'aa kupitia maneno na uso wa mwandishi ambaye "kitaalam" si Mkatoliki. Lakini moyoni mwake, jioni moja huko Laterano, ulimwengu na neema zilikumbatiana-mpaka wakawa karibu kutofautishwa.
 

31 Januari 2025, 17:37