Mafungo ya Washiriki wa Sinodi,Costelloe:kuwa Kanisa nyenyekevu,utume na kusikiliza!
Na Askofu Mkuu Timothy John Costelloe, SDB,-Jimbo Kuu Perth (Australia)
Kwa hakika inafaa sana na tunaweza hata kusema kwamba ni zawadi ya Maongozi ya Kimungu, kwamba tuanze kazi yetu pamoja katika “Sinodi hii ya ksinodi” kwa kukusanyika pamoja katika mafungo katika siku ambayo Kanisa linakumbuka maisha na ushuhuda wa Mtakatifu Jerome. Tunaambiwa, alikuwa mtu mwenye mapenzi na mgumu, mtu ambaye hakuona rahisi kuvumilia yale aliyoyaona kuwa mapungufu ya wengine. Wakati huohuo, alikuwa mtu ambaye angeweza kutambua kasoro na madhaifu katika njia yake mwenyewe ya kuwafikia watu na ambaye aliudhishwa na kutambua kwamba mtazamo wake mkali kwa wengine nyakati fulani ulisababisha kosa kubwa na kuteseka. Pengine, angekuwa mhusika mgumu kumsimamia kama angekuwa mjumbe wa Sinodi inayotuita kusikilizana kwa kina na kwa heshima! Miongoni mwa mambo mengi ambayo anakumbukwa kwayo, hata hivyo, labda msemo wake maarufu, kwamba: "kutojua Maandiko ni kutomjua Kristo", ni zawadi ya thamani anayotupatia tunapoingia katika yote yaliyo mbele ya majuma kama matatu au manne yajayo.
Hatuwezi kumudu kutomjua Kristo, au kumsahau, tunapotafuta kutambua kwa pamoja ni nini hasa ambacho Mungu anaomba kwa Kanisa kwa wakati huu. Kwa namna fulani tuna jibu, au angalau kuhisi jibu, katika uhakikisho ambao Papa Francisko anatupatia kwamba Mungu anatuita kuwa, pamoja, Kanisa la Sinodi katika Utume. Safari tuliyoanza nayo hadi sasa imetufanya kuelewa kwa kina maana ya Sinodi. Sasa, katika hatua hii ya safari, tunaombwa kutafakari sio sana nini maana ya sinodi, bali jinsi gani tunavyopaswa kuishi katika kila ngazi ya maisha ya Kanisa: kama Wakristo binafsi, hakika, lakini daima kama watu walioitwa pamoja, katika jumuiya ndogo na kubwa, ili wawe ishara na vyombo hai - sakramenti hai - ya ushirika na Mungu na umoja kati ya watu wote. Katika kitabu cha Mwanzo, Mungu alipomuumba mwanamume wa kwanza, Mungu aliona si vema huyo mwanamume awe peke yake, ndipo Mungu alipomuumba mwanamke wa kwanza na kuwapa wao kwa wao ili waingie katika mahusiano ili kuunda jumuiya.
Uzoefu wetu wa safari ya sinodi umetuthibitishia ukweli huu mzito - kwamba katika muundo wa uumbaji wa Mungu tumeumbwa kwa ajili ya kila mmoja wetu, kwamba tumekusudiwa kutegemeana, na kwamba ni ndani na kupitia mahusiano yetu ndipo tunapokuja kuwa watu ambao Mungu ametuumba kuwa. Safari ya sinodi imekuza uthamini wetu wa umuhimu wa mahusiano yetu sisi kwa sisi. Kujihusisha kwetu katika “Mazungumzo katika Roho” kumefungua macho yetu kwa uwezekano ambao umakini wa kina, heshima na wa haraka kwa wengine unatushikilia sisi sote. Hizi ni zawadi za thamani kwa Kanisa zima. Tunapofikia kuelewa kwa uwazi zaidi jinsi gani uhusiano wetu na dada na kaka zetu katika imani ulivyo muhimu, tunaweza kukumbuka maneno ambayo Mtakatifu Paulo aliyaelekeza kwa jumuiya ya kwanza ya Kikristo huko Filipi: lazima uwe na nia moja iliyokuwa ndani ya Kristo Yesu. Akili hiyo na tunaweza kuongeza moyo huo, imefunuliwa kwetu katika kila ukurasa wa injili. Tunapomwona Yesu akijishughulisha na mahusiano mengi tofauti, na kuguswa na mikutano mingi tofauti na watu, tunaanza kupata maono ya jinsi gani mikutano ya kweli na ya kina ya wanadamu inavyoonekana.
Tunaweza kufikiria juu ya subira isiyo na kikomo ambayo Yesu anaonesha kwa wale, hasa wanafunzi wake wa karibu zaidi, ambao mara kwa mara wanashindwa kumwelewa na ambao mara nyingi humkatisha tamaa, kama historia ya Injili ya leo inavyotukumbusha, na jinsi subira yake inavyowazuia kukata tamaa. Tunaweza kufikiria usikivu usio wa kawaida ambao Yesu anauonesha kwa wale wanaoonekana kulemewa na mizigo ya dhambi zao wenyewe, na jinsi usikivu huo unavyowaweka huru. Tunaweza kufikiria huruma ya Yesu kwa wale waliopotea au waliochanganyikiwa au kusukumwa pembeni, na jinsi huruma hiyo inavyorejesha tumaini lao. Na tunapotafakari juu ya mifumo ya ushirika wa Yesu na watu wengi tofauti kwa njia nyingi tofauti, ingekuwa muhimu kwetu kukumbuka kwamba maneno aliyowaambia wanafunzi wake kwenye Karamu ya Mwisho ni maneno anayotuambia pia kwamba: Mimi Ndimi Njia; Mimi ndiye Kweli; Mimi Ndimi Uzima.
Ukitaka kujua jinsi ya kuwa Kanisa lenye ukaribishaji na ukarimu, jifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ndimi njia. Ukitaka kujua jinsi ya kuwa Kanisa maskini na nyenyekevu jifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ndimi njia.Ukitaka kujua jinsi ya kuwa Kanisa katika utume, jifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ndimi njia. Ukitaka kujua jinsi ya kuwa Kanisa linalosikiliza, jifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ndimi njia. Kama, katika siku zijazo, tunapambana na swali la jinsi gani ya kuwa Kanisa la kisinodi katika utume, tutahitaji kuweka mitazamo yetu kwa Kristo. Nyakati fulani mambo tunayoona yatatufariji, nyakati fulani yatatuchanganya, na nyakati fulani yanaweza hata kutukabili au kututisha. Lakini mwishowe, kwa kufafanua kifungu maarufu cha Papa Mtakatifu Yohane XX111, Kanisa ni la Kristo, sio letu. Ni yeye tunayemfuata, hakuna mwingine. Basi, na tuendelee kuomba kwamba Roho wa Kristo atuongoze na kuwa nyumbani ndani ya mioyo yetu; kwamba licha ya udhaifu wetu na dhambi Roho atatuwezesha kukua si machafuko bali maelewano; kwamba katika Roho wa Kristo tutapata umoja wetu na kuwa pamoja sakramenti hai ya ushirika na Mungu na umoja kati ya watu wote.
Na Maria, Mama wa Kanisa, atusindikize kwa maombi yake kwa ajili yetu sote.