PMS:Utume ni moyo wa Kanisa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
“Utume ni moyo wa Kanisa,” ndiyo mada ya video ya dakika 2 iliyohaririwa na Kurugenzi ya Kitaifa wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ya Poland kwa mwezi Oktoba mwaka 2023 katika hafla ya Siku ya Utume wa Kimisionari Ulimwenguni Nchini Poland na sasa inapatikana katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kihispania. Fundisho katika video hii fupi ni historia ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, maendeleo yao na umuhimu wake leo hii.
Katika video, mkono unaakisi historia hii kama katuni. Yote yanaanzia moyoni mwa Mwokozi ambaye anawatuma wanafunzi kwa maneno haya: “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi.”
Sura kuu ni Mwenyeheri Pauline Jaricot, ambaye mnamo mwaka 1822 alianzisha Shirika la Kipapa la Kueneza Imani, na ambalo ni shirika la kwanza kati ya Mashirika manne ya Kimisionari. Kupitia kwa hayo mashirika Papa anajali mahitaji mengi ya kichungaji ya Makanisa machanga.
Mwishoni mwa video hii, mwaliko unaelekezwa kwa wote ili kuishi asili ya umisionari kwa nguvu ya sakramenti ya ubatizo, kusikiliza mioyo ya mtu, kuweka karama za mtu katika huduma ya wengine, na kuimarisha maana ya kuwa mfuasi wa umisionari.