SECAM: Hakuna Baraka Kwa Wapenzi wa Jinsia Moja Kwa Kanisa Barani Afrika
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lilijadiliwa katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, likapelekwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, akaridhia lichapwe kwa kuweka saini yake tarehe 18 Desemba 2023. Tamko hili linajadili kwa kina na mapana kuhusu: Baraka katika Sakramenti ya Ndoa, Maana ya baraka katika Maandiko Matakatifu, Uelewa wa baraka kitaalimungu na kichungaji, na nani anaweza kuomba baraka. Baraka kwa watu wenye “ndoa tenge” pamoja na wapenzi wa jinsia moja. Kanisa ni Sakramenti ya upendo wa Mungu. Watu wa Mungu wenye imani thabiti wanaweza kupokea baraka za Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa na kwamba, Kristo Yesu ni kielelezo cha baraka kuu kutoka kwa Mungu, baraka ambayo ni chemchemi ya wokovu. Baraka katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu: Kiini cha ndoa ya Kikristo ni maagano baina ya mume na mke au ukubaliano wao wa hiari usiotanguka. Muungano huo wa mume na mke na manufaa ya watoto wao huwataka wawe na uaminifu kamili kati yao. Kwa asili yake ndoa na mapendo ya wenye ndoa yamewekwa kwa ajili ya kuzaa watoto na kuwalea; nao ni taji yao. Kwa kweli watoto ni zawadi kuu ya Ndoa na tunu kubwa ya wazazi wenyewe. Haya ndiyo Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Ndoa na kamwe hayawezi kubadilishwa. Wakati wa kutoa baraka, Kanisa lina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba halichanganyi madhehebu ya kutoa baraka, ili kusitokee mkanganyiko na kwamba, Kanisa halina mamlaka ya kutoa baraka kwa wapenzi wa jinsia moja. Tamko hili likapokelewa kwa hisia tofauti na hivyo kuzua mjadala mkali wa kiimani, kimaadili, kisheria na utu wema kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Kardinali Fridolin Ambongo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, katika barua yake ya tarehe 20 Desemba 2023 akayaomba Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika kujadili tamko hili la “Fiducia Supplicans”, ili hatimaye, Kanisa Barani Afrika liweze kutoa msimamo na mwongozo kwa waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika, kwa kutambua dhamana na umuhimu wa Mabaraza ya Maaskofu katika kuambata mchakato wa Sinodi sanjari na kukuza urika wa Maaskofu. Tamko la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM ni matunda ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi kwa hiyo ni kwa ajili ya Kanisa zima la Bara la Afrika. Ni katika muktadha huu, SECAM, tarehe 11 Januari 2024 imetoa tamko linalosema, hakuna baraka kwa wapenzi wa jinsia moja kwa Makanisa Barani Afrika. Tamko hili limeridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Kardinali Victor Manuel Fernàndez, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Hili ni tamko linajadili mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Tendo la Ndoa; Mwongozo wa Kichungaji kwa familia ya Mungu Barani Afrika; Msimamo wa Kanisa Barani Afrika mintarafu mapenzi ya watu wa jinsia moja na hatimaye, SECAM inatoa hitimisho ya tamko lake.
Maaskofu Barani Afrika wanatambua dhamana na nafasi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kukuza umoja wa imani, ushirika na urika kati yao, daima wakiwa waaminifu kwa tunu msingi za Kiinjili. Wanatambua mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia ambayo kamwe hayawezi kubadilika na kwamba, Tamko la “Fiducia supplicans” linatambua Mapokeo ya Kanisa Katoliki yanayopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na Mamlaka Fundishi ya Kanisa “Magisterium of the Church” kwamba: Kiini cha ndoa ya Kikristo ni maagano baina ya mume na mke au ukubaliano wao wa hiari usiotanguka. Kumbe mahusiano ya watu wa jinsia moja ni jambo lisilokubalika na kwamba, Kanisa Barani Afrika haliwezi kutoa baraka. Kanisa Barani Afrika linaendelea kujitambulisha kuwa ni familia ya Mungu inayowajibika na kwamba, litaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu Barani Afrika na kwamba, Mapadre wanahimizwa kutoa huduma kwa watu wenye “ndoa tenge” na kwamba, mashoga na wasagaji waheshimiwe na utu wao uthaminiwe lakini wakumbushwe kwamba mahusiano ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha mapenzi ya Mungu na kwa mantiki hii hawawezi kupata baraka ya Kanisa kwani mahusiano haya ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. SECAM inasema Mapokeo yametamka daima kwamba matendo ya kujamiana ya jinsia moja ni maovu kwa yenyewe. Ni matendo dhidi ya sheria ya maumbile. Yanatenga paji la uhai na tendo la kijinsia. Hayatokani na kutimilizana kwa kweli kihisia na kijinsia. Kwa namna yoyote ile hayawezi kuidhinishwa. Rej. KKK 2357.
Mapenzi ya jinsia moja ni kashfa kadiri ya Maandiko Matakatifu. Katika muktadha wa Kanisa Barani Afrika, mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na ni vigumu sana watu wa namna hii kukubalika na hatimaye kupokelewa na jamii kwa sababu ni matendo yanayokwenda kinyume cha tamaduni na kwamba, huu ni uovu! SECAM inahitimisha tamko lake kwa kusema, kadiri ya Maandiko Matakatifu, Mamlaka Fundishi ya Kanisa, tamaduni, kanuni maadili na utu wema, Kanisa Barani Afrika halitatoa baraka kwa watu wa mapenzi ya jinsia moja, kwani kufanya hivi ni kuibua kashfa na kwamba, kuna umuhimu kwa watu wenye shauku ya jinsia moja kutubu na kumwongokea Mungu ili waonje huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, tayari kuwa ni chumvi na nuru ya dunia. Rej. Mt 5:13-14. SECAM inasema, kuna baadhi ya nchi Barani Afrika zimeomba, muda wa kufanya tafakari na mang’amuzi, ili kutoa maamuzi na kwamba, SECAM itaendelea kufanya tafakari kuhusu umuhimu wa baraka kwa watu wa Mungu katika shughuli zake za kila siku. Kanisa Barani Afrika linapaswa kuendelea kuwa imara na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hataki kuona ukoloni wa kiitikadi na kitamaduni Barani Afrika! Wakristo Barani Afrika wawe tayari kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya Kikristo!