Papa amekutana na rais wa Guinea Bissau
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumatatu tarehe 29 Januari 2024 kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Vyombo vya Habari Vatican, inataarifa kuwa: “Baba Mtakatifu Francisko amempokea, katika Jumba la Kitume mjini Vatican, Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau, Bwana Umaro Sissoco Embaló, ambaye mara baada ya mazungumzo alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, akifuatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa.”
Katika taarifa hiyo tunasoma kuwa: “Wakati wa mazungumzo yao ya ukarimu katika Sekretarieti ya Vatican, uhusiano mzuri kati ya Vatican na Guinea Bissau ulisisitizwa, na baadhi ya mambo ya hali ya kijamii ya nchi yaliakisiwa na mchango wa Kanisa kwa ajili ya manufaa ya wote ukasisitizwa, hasa katika nyanja za elimu na afya.
Katika kubadilishana zawadi za kiutamaduni, Papa Francisko amempatia rais Sanamu ya shaba, Idadi za hati za kipapa na vile vile Ujumbe wa Amani wa mwaka 2024.