Tafuta

Kardinali  Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu amehutubia huko Manila, Ufilippino 19 Januari 2024. Kardinali Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu amehutubia huko Manila, Ufilippino 19 Januari 2024. 

Kardinali Grech:Umuhimu wa matokeo ya Sinodi ya Oktoba 2023 na Oktoba 2024

Kardinali Mario Grech amewahutubia washiriki katika Kongamano la Uinjilishaji Mpya huko Manila,Ufilipino,akitazama matokeo muhimu ya Mkutano wa Sinodi wa mwezi Oktoba 2023 na katika kuelekea Oktoba 2024 amesema ni Kanisa la Sinodi katika Utume na matumaini yake.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Kardinali Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu  akiwahutubia washiriki wa Kongamano la Uinjilishaji Mpya linaloendelea huko Manila nchini Ufilipino(PCNE) tarehe 19 Januari 2024, alianza kushirikisha furaha yake kwa wale wote walioshiriki katika kikao cha kwanza cha Mkutano Mkuu wa XVI wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu Oktoba 2023 mjini Roma na kusisitiza matokeo ya kusanyiko hilo, huku akiwa na matumaini makubwa ya kikao kijacho mwezi Oktoba 2024. Akionesha nia yake ya kujifunza zaidi kuhusu matayarisho ya ndani na uzoefu katika mchakato mzima wa sinodi inayofanyika Ufilipino, Kadinali Grech alizungumza kuhusu vipengele vitatu vya mkutano wa kimataifa wa mwezi  Oktoba na jinsi wanavyolitazama Kanisa la Asia pia. Kwa hiyo alijikita na kukumbusha mchakato wa Sinodi ambapo washiriki wa Sinodi  iliyopita walikutana katika Ukumbi wa Paulo VI, wakiwa na mapadre na walei waliochanganyika, walioketi katika meza za mduara, watu kumi hadi kumi na wawili kama  vile kwenye karamu ya harusi au mkusanyiko mwingine mkubwa wa familia.

Jambo jipya katika Sinodi

Jambo hili jipya katika mchakato wa sinodi lilisaidia kuweka jukwaa la mazungumzo katika Roho  ya yote yaliyofanyika. Na pia alikumbuka ushiriki kamili na sawa wa wasio maaskofu, wakiwemo waamini walei, watawa kike na kiume, mashemasi na mapadre, kama washiriki wapiga kura. Na kwa hiyo "uzoefu wa kusikilizwa pia unashinda hisia zetu za kutengwa. Watu wanapotumia wakati na jitihada kutusikiliza, hilo hutupatia hisia ya kuthaminiwa, alisema pia inakuza urafiki na kujenga mshikamano." Kardinali Grech alibainisha mada kuu katika Ripoti ya Muhtasari. Ripoti hiyo kwamba  inasisitiza jinsi ambavyo Makanisa mahalia yanavyohitaji ushirikiano bora na vijana katika jumuiya zao, maisha ya kisakramenti na shughuli za kimisionari. Kwake yeye alipendekeza kwamba Ufilipino na Kanisa Katoliki katika  bara la Asia kwa ujumla liko katika nafasi nzuri ya kutoa uongozi kwa Kanisa la ulimwengu wote katika kujibu kile Kikao cha Kwanza cha Baraza Kuu kilivyorejea kama kufanya chaguo la upendeleo kwa vijana. Idadi kubwa ya vijana duniani sasa wanaishi Asia," alisema

Kilio cha dunia na maskini

Tokeo la pili la kikao cha Sinodi la Oktoba 2024 Kardinali Grech alisema linataka“kusikiliza kilio cha dunia na kilio cha maskini, ambacho ni kilio kimoja”.  Na akinukuu kutoka katika Ripoti ya Muhtasari, alisisitiza udharura huu akisema kwamba kuwa karibu na wale ambao ni maskini kunahitaji kushirikiana nao katika kutunza nyumba yetu ya kawaida ya pamoja na ukosefu wa majibu ya kilio hiki husababisha mgogoro wa kiikolojia na mabadiliko ya tabianchi hasa, tishio kwa maisha ya binadamu. Kiongozi huyo aidha alitoa mwaliko kwa Kanisa la Ufilipino kuchukua nafasi ya uongozi katika mchakato huu, ili “kuweka dhamiri sisi sote katika mambo haya, kwa kuimarisha dhamiri zetu zote katika kuitikia kilio cha dunia na kilio cha maskini.

Kusikia Furaha ya Injili ndani ya mioyo yetu

Hatimaye, Kardinali Grech alikazia kuonesha jinsi ambavyo mada kuu iliyosisitizwa katika Ripoti ya Muhtasari inavyo tukumbusha kuweka kwa makini katika  akili na mioyo yetu  Furaha ya Injili, furaha inayobubujika kutokana na kusikia utangazaji  wa Habari Njema. Kuhusu Mkutano Mkuu ujao wa hatua ya II Oktoba 2024, Kadinali Grech alielezea matumaini ya miezi ijayo kuwa: “itakuwa wakati wa kuimarisha uelewa wetu na uzoefu wa jinsi ilivyo kuishi katika Kanisa ambalo uwajibikaji pamoja wa umisionari ni uzoefu wa kila siku na inaweza kuchukuliwa kuwa ya kawaida." Katika eneo hilo pia alipendekeza "kufanya kazi kwa hatua za vitendo kuelekea mtazamo wa kuwajibika zaidi kwa utume na huduma ya Kanisa inayohusisha waamini wote, pamoja na kuwa na nguvu ya kisinodi katika maisha ya kila siku ya Kanisa, kwa undani zaidi jinsi tunavyoelewa na kuishi Sinodi katika Makanisa yetu ya mahali.”

20 January 2024, 15:48