Noeli 2023,Kard.Re:Papa ametoa miito ya kufungua mazungumzo ya amani
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kabla ya hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali amesoma hotuba yake ya kumkaribisha na kumpongeza Baba Mtakatifu niaba ya Sekretarieti Kuu ya Vatican kama sehemu ya utamaduni wa kila mwaka wa kutakiana heri za Noeli. Akiwa katika Jumba la Kitume mjini Vatican, Alhamisi tarehe 21 Desemba 2023 amesema kuwa “Kama sauti ya wote waliohudhuria”, anampatia heri ya Noeli ya upendo, ikiambatana na ukumbusho katika maombi kwa ajili yake, kwa ajili ya afya yake na kwa nia yake. Alipenda kueleza hisia zao pamoja za shukrani na utambuzi kwa kujitolea kwake bila kuchoka na kujitolea kwake kwa bidii katika huduma ya Petro kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya ulimwengu katika mwaka huu wa kumi wa upapa wake. Kardinali Re amebanisha kuwa: “Umekuwa mwaka mgumu hasa kutokana na vita vya kutisha vinavyotokea duniani na matokeo maumivu ya kutisha na mateso ya kinyama kwa watu wengi, ambao mara nyingi hufikia umaskini mkubwa na nyumba zao kuharibiwa. Baba Mtakatifu umerudia mara kwa mara kulaani vita, ambayo ulisema kuwa "siku zote ni kushindwa kwa kila mtu" na huleta kifo na uharibifu tu.”
Kwa njia hiyo Kardinali Re amekazia kusema kuwa “Wito wake mchangamfu wa kufungua mazungumzo na kujitolea kwa dhati kwa amani ulikuwa na nguvu. Mara kadhaa, karibu kila hotuba, aliomba kila mtu aombe amani. Kwa kukabiliwa na matatizo makubwa ya leo hii na hali mbaya za maumivu, Baba Mtakatifu amefanya yote awezayo ili kuhakikisha, kwa kadiri iwezekanavyo, mshikamano thabiti na ukaribu wa upendo kwa watu. Ahadi ambayo kila wakati alijaribu kuwa karibu na mateso ya kila mtu na ikikuwa ni ya kupendeza kila siku. Kulikuwa pia na himizo la mara kwa mara, lililoelekezwa kwa washiriki wote wa Kanisa, kupeleka Injili katika jamii” ya wakati wetu, kwa upendo huo wa kichungaji ambao lazima upenyeza maamuzi na mitazamo yetu yote.”
Sinodi ushirikishwaji mpana wa majimbo ili kutembea pamoja
Kardinali Re aidha amesisitiza kuwa katika “Kikao cha Baraza Kuu la Sinodi ya Maaskofu, kilichoadhimishwa mwezi Oktoba mwaka huu na ambacho kitakuwa na mwendelezo wake wa mwisho mwakani, kiliwakilisha ushirikishwaji mpana wa majimbo na aina mbalimbali za watu, na kuwaalika kila mmoja “kutembea pamoja na mtazamo wa Yesu. Pia alisisitiza haja ya ushirikiano wa kina kati ya Maaskofu, mapadre na walei, pia kutafuta njia mpya, lakini katika mwendelezo wa uaminifu kamili kwa mafundisho kupitishwa kwetu na Mitume. Ziara nyingi za Kimataifa za Kitume, pamoja na hotuba na mahubiri mengi yanayorejea hali mbali mbali, zimesaidia kila mmoja kutafakari masuala ya sasa katika sehemu mbali mbali za dunia, na kutia moyo na kujiamini katika siku zijazo. Ziara ya kuelekea Lisbon kwa Siku ya Vijana Duniani ilikuwa na sauti kubwa duniani kote.
Shukrani kwa Waraka Laudate Deum
Decano wa Makardinali aidha alibainisha kuwa “Tunakushukuru sana kwa zawadi ya Waraka wa Kitume wa Laudate Deum, uliochapishwa tarehe 4 Oktoba, katika Sikukuu ya Mtakatifu Francis, ambayo kwa mara nyingine tena umeakisi uharaka wa kutilia maanani makao yetu ya pamoja, ambayo Mungu Muumba ametukabidhi, na kuhimiza kila mtu kuwa na tabia inayotokana na mazungumzo na ushirikiano wa karibu wa wote ili kuondokana na changamoto za leo za kimazingira na kijamii. Hata kama safari iliyopangwa ya kwenda Dubai isingewezekana kufanyika, ujumbe wake kwa COP 28 ulikuwa na sauti kubwa, na wito wa dhati wa mabadiliko ya kasi katika kujitolea kulinda uumbaji; wito wa “njia mpya ya kuendelea pamoja”, kuunganisha nguvu na kuacha migawanyiko nyuma, kwa sababu sisi sote tuko kwenye mtumbi mmoja na lazima tupige makasia pamoja. Kwa hiyo amemshukuru kwa Waraka wa Kitume kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 400 ya kuzaliwa kwa Blaise Pascal na kwa Waraka wa Kitume wakati wa kumbukumbu ya miaka 150 ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, unaotukumbusha katika akili yetu ile “njia ndogo” ya uaminifu na wa upendo.”
Hatimaye, maadhimisho ya miaka kumi ya Waraka wa Kitume Evangelii gaudium ilikuwa fursa ya kufanya upya mwaliko wa kuzidisha dhamira ya kutangaza Injili kwa ulimwengu wa leo na kurejesha furaha ya kimisionari ya Wakristo wa kwanza. Matatizo ya wakati huu ni makubwa kwelikweli, lakini imani inatuongoza kuyakabili kwa tumaini la Kikristo na kwa uhakika kwamba Mungu ndiye Bwana wa historia na mioyo. Ulimwengu unahitaji mwamko wa kidini na uamsho mkali wa maisha ya Kikristo. Kwa kuhitimisha wamemwahidi kuwa karibu naye huku wakifanya kwa upya hadi yao ya huduma kwa ushirikiano wa karibu nayeye na kuomba baraka zake za kitume.