Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania na kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu amemteua Kardinali Protase Rugambwa, kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora. Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyemkirimia afya na imani na sasa anang’atuka kutoka madarakani. Anawalishukuru Taifa la Mungu nchini Tanzania tangu mwanzo alipoteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kigoma na hatimaye, kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora. Anamshukuru Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko waliombidiisha katika dhamana ya uongozi bhila kuwasahau watu wa Mungu na wote wenye mapenzi mema hadi wakati huu anapokabidhi “kijiti” kwa Kardinali Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora.
Mwaliko wa pekee kwa watu wa Mungu anasema Askofu mkuu mstaafu Ruzoka ni kumwombea Kardinali Protase Rugambwa heri na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa maombezi ya Bikira Maria. Askofu mkuu mstaafu Ruzoka anamshukuru Mungu kwa kumwongoza vyema tangu alipoteuliwa kuliongoza Jimbo Katoliki la Kigoma hadi sasa anapokabidhi Jimbo kuu la Tabora mikononi mwa Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora. Hiki ni kielelezo cha neema na bbaraka pasi na mastahili yake iliyomwezesha kuwa jinsi alivyo. Hii ni neema na baraka kwa Jimbo kuu la Tabora kustahilishwa kupewa Kardinali Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora anapong’atuka kutoka madarakani. Hiki ni kielelezo cha juu sana cha furaha yake kutoka sakafu ya moyo wake!
Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Paulo Ruzoka, alizaliwa kunako mwaka 1948 huko Nyakayenzi, Kigoma. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 20 Julai 1975 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa kuwekewa mikono na Askofu Alphons Daniel Nsabi wa Jimbo Katoliki la Kigoma, akiwa ni Padre wa sita mzalendo, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, matendo makuu ya Mungu. Tarehe 10 Novemba 1989, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma na kuwekwa wakfu na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1990 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 25 Novemba 2006, Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora na kusimikwa rasmi tarehe 28 Januari 2007. Na ilipogota tarehe 10 Novemba 2023 Baba Mtakatifu Francisko akaridhia ombi lake la kung’atuka kutoka madarakani. Kimsingi Askofu mkuu mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 48 na kama Askofu miaka 33 huku akifundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.