Vita Mashariki ya Kati:Papa ampigia simu Rais wa Uturuki
Vatican News
Alhamisi tarehe 26 Oktoba kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican, Dk. Matteo Bruni alitangaza kuwa: “Naweza kuthibitisha kwamba asubuhi ya leo mazungumzo ya simu yalifanyika kati ya Papa na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan. Mawasiliano, yaliyoombwa kwa mara hii yalilenga hali ya kushangaza katika Nchi Takatifu. Papa alielezea masikitiko yake kwa kile kinachotokea na kukumbuka msimamo wa Vatican, kwa matumaini kwamba suluhisho la serikali mbili na sheria maalum kwa mji wa Yerusalemu linaweza kupatikana.”
Hata hivyo nchini Uturuki ilikuwa imefahamisha asubuhi Oktoba 26, kwamba katika mazungumzo hayo rais alionesha wasiwasi mkubwa kwa Papa kuhusu kile kinachotokea Gaza na kuyaita kama “mauaji”. Ikumbukwe katika muktadha huo mnamo Oktoba 22 iliyopita, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa na mazungumzo ya simu pia yaliyochukua takriban dakika 20 na Rais wa Marekani, Bwana Joe Biden, kuhusu hali ya migogoro duniani na hasa haja ya kutafuta njia za amani.