Sinodi,Kanisa zuri ni Kanisa lenye milango iliyofunguliwa
Na Alessandro Di Bussolo & Angella Rwezaula,- Vatican.
Uzuri wa kweli wa Kanisa Katoliki unaonekana wazi wakati milango yake iko wazi na kuwakaribisha watu. Tunatumaini kwamba Sinodi itatusaidia kuzifungua zaidi. Hivyo ndivyo Kadinali Joseph William Tobin, Askofu Mkuu wa Newark, nchini Marekani alivyoeleza mada ya sehemu ya pili ya Instrumentum laboris au kitendea kazi. Sehemu hiyo inabainisha wazi mada ya: "Ushirika unaong’aa: Tunawezaje kuwa ishara kamili zaidi na chombo cha umoja na Mungu na umoja wa wanadamu wote?" ambayo ilijadiliwa katika vikundi vidogo vidogo Jumatatu tarehe 9 Oktoba mchana na Jumanne asubuhi tarehe 10 Oktoba 2023 katika Sinodi inayoendelea. Kardinali Tobin alizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu kazi ya mkutano huo ulioongozwa na Rais wa Tume ya Habari, Dk. Paolo Ruffini, na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano.
Makabiliano katika vikundi vidogo vidogo katika sehemu ya pili
Katika vikundi vidogo vidogo, washiriki wa Mkutano Mkuu walijadili elimu, mazingira, tamaduni nyingi na kutembea na watu waliotengwa na wahamiaji. Siku ya Jumatatu 9 Oktoba 2023, walichagua wajumbe wa Tume ya Ripoti ya Muswada na wale wa Tume. Vikundi vidogo vidogo vilivyopangwa kwa msingi wa mada zinazoshughulikiwa, vilijadili vifungu vidogo vya hati hiyo B1 vilivyojikita juu ya ushirika na vitawasilisha tafakari yao katika mkutano mkuu wa tano mchana na katika kusanyiko la sita na la saba Jumatano asubuhi tarehe 11 Oktoba 2023.
Dk. Ruffini: ushirikiano mkubwa kati ya washiriki wote
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Dk. Ruffini alisisitiza kuwa katika Sinodi ya tatu, wajumbe wana fursa nyingi zaidi za kuzungumza, hasa katika vikundi vidogo. "Kuna ushirikiano mkubwa kati ya washiriki wote, kulingana na uzoefu wangu binafsi, mbayo ilianza na mafungo ya kabla ya sinodi." Kardinali Tobin kwa upande wake akijibu swali kuhusu Sinodi hiyo kuelekezwa kutoka juu kwenda chini alisema kwamba, “anajiamini kwa sababu mambo hayatujii kutoka juu bali ni mchakato unaoanzia chini kuanzia na uhusika wa Watu wa Mungu, na kufika kileleni. Sijisikii kulazimishwa au kufungwa pingu,”alisisitiza Kardinali huyo.
Sr. Echeverri: Tunasikiliza kilio cha maskini, wahamiaji na waliotengwa
Mbali na Kardinali Tobin Mtawa wa Shirika la Mkombozi na mjumbe wa Baraza la Kawaida la Sekretarieti ya Sinodi, kulikuwa na Sista Gloria Liliana Franco Echeverri, kutoka Colombia wa Shirika la Bikira Maria, na rais wa Shirikisho la Watawa wa Amerika Kusini (CLAR) na ambaye ni shuhuda wa Mchakato wa Sinodi. Kama kawaida, pia Sheila Leocádia Pires, katibu wa Tume ya Habari ya Sinodi, pia alizungumza. Kwa njia hiyo akizungumza Sr. Echeverri alisisitiza kwamba miongoni mwa washiriki wa Mkutano Mkuu wa XVI wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, kuna nia ya kuishi kama Yesu “Anayefanya ubinadamu, Anayeheshimu, Anayejumuisha, Yesu anayefungua mlango kwa ajili ya mwingine.”
Sr. huyo aliendelea kusema kuwa ni mchakato “unaoona njia tofauti, kuanzia na kuongoka katika Roho. Katika vikundi vyetu vidogo tunatambua kwa usahihi hadhi hii ya pamoja, hadhi inayotokana na heshima, ushirika na kutambuliwa kwa pande zote. Katika mjadala juu ya sehemu ya sasa, “inayovuma mioyoni mwetu ni wito wa kusikiliza kilio cha maskini. Katika meza yetu, sura ya maskini, uhamiaji, biashara haramu ya watu, kutengwa na jamii katika pembezoni kulisikika kwa sauti kubwa,” alithibitisha.
Kardinali Tobin: kuvutia kwa mazungumzo katika tamaduni nyingi
Kadhalika Kardinali Tobin, ambaye yuko katika kikundi kidogo pamoja na Sr. Echeverri, alielezea tena kwamba msichana kutoka Urussi, mama kutoka Ukraine na mchungaji wa Kipentekoste kutoka Ghana, mtaalimungu kutoka Malaysia na mratibu kutoka Singapore pia walikuwa katika kundi lao. “Ni hali bora kwangu, kuwa katika kundi la watu mbalimbali na kuweza kuwasikiliza wengine. " Hilo, alisema lilimvutia, kwa kuwa alikulia huko Detroit katika mazingira ya kiutamaduni, na ambaye kama kasisi kwa miaka 45 ameishi katika tamaduni ambazo hazikuwa zake, na hata ile aliyolelewa. Kwa njia hiyo alibainisha kwamba hiyo ni kama "Sinodi tofauti zaidi ambayo nimewahi kushiriki."
"Chaguo la Kanisa ni udugu: kuna nafasi kwa kila mtu"
Kardinali Tobin pia alishirikisha tukio halisi la kichungaji, mapokezi katika Kanisa Kuu la Newark kuhusu "hija ya watu waliohisi kutengwa kwa sababu ya mwelekeo wao wa kijinsia." Hiyo, alisema, ilikuwa tukio la wazi la Kanisa. Na alihitimisha kwamba katika ulimwengu unaodhihirishwa na utaifa wa kutengwa, na chuki dhidi ya wageni, ambapo kuna viongozi ambao wamejitolea kujenga mipaka, chaguo la Kanisa ni udugu, sinodi, ambalo ni chaguo linalotuwezesha kuelewa kuwa sisi sote ni kaka na dada. Kwa hiyo katika Kanisa ambalo tunajiona kama kaka na dada kuna nafasi kwa kila mtu, alisema Kardinali Tobin.