Caccia:Matokeo ya Teknolojia za kidijitali katika elimu na utamaduni
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani, Askofu Mkuu Gabriele Caccia, tarehe 31 Agosti 2023, ametoa hotuba yake katika Jukwaa kuhusu Utamaduni na Amani kwa kuongoza na mada: “Kuhamasisha utamaduni wa Amani katika Enzi za kidijitali”. Katika hotuba hiyo alibainisha kuwa Vatican inaunga mkono kuhusu kuitisha Jukwaa la Ngazi za Juu la mwaka 2023 kwa kauli mbiu hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni maendeleo ya kidijitali yameleta fursa na changamoto muhimu kwa juhudi za kimsingi za kukuza utamaduni wa amani. Kutokana na hali hiyo, Baba Mtakatifu Francisko alichagua mada ya: “Akili Bandia na Amani kwa ajili ya ujumbe wake wa Siku ya 57 ya Amani Duniani, huku akiwaalika watu wote kuchunguza jinsi ambavyo teknolojia inavyoweza kukuza amani na jinsi ya kuzuia matumizi yake mabaya, yanayochochea ukosefu wa haki, migogoro na uadui. Kwa njia hiyo akihutubia Jukwaa hilo la Ngazi ya Juu, Mwakilishi wa Vatican alipenda kuzingatia maeneo mawili maalum.
Teknolojia za kidijitali ziwe na lengo la utamaduni wa amani
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika kudadavua alisema: "kwanza kabisa teknolojia za kidijitali zina athari kubwa kwa elimu. “Zinaweza kuwa muhimu katika kukuza maadili na malengo ya utamaduni wa amani, lakini kuzitegemea kupita kiasi kunahatarisha kuishusha elimu, hadi kuwa chombo cha kusambaza maarifa ya kiufundi na kuinyima kipengele muhimu cha kibinadamu.” Aidha aliongeza kusema kuwa “Azimio la Utamaduni wa Amani linasema kwamba: “jukumu kuu katika kuendeleza utamaduni wa amani ni baada ya mengine wazazi, walimu, wanasiasa, waandishi wa habari, mashirika ya kidini na vikundi […], kwamba akili na roho hasa ya vijana huundwa. Hapo, mwanadamu hupokea malezi muhimu “katika mazungumzo, kukutana, umoja, uhalali, mshikamano na amani, kwa njia ya kukuza sifa msingi za haki na mapendo.”
Teknolojia zieneze utamaduni wa kukutana,mazungumzo na kusikiliza
Pili, teknolojia za kidijitali zina jukumu muhimu katika kueneza “utamaduni wa kukutana, utamaduni wa mazungumzo, utamaduni wa kumsikiliza mwingine na sababu zake.” Ubunifu huu mpya huruhusu watu kutumia haki yao ya uhuru wa maoni na kujieleza. Hata hivyo, lazima zitumike kwa uwajibikaji, kwa kuwa haki za binadamu pia zinamaanisha wajibu unaolingana. Kama Papa Francisko alivyothibitisha hivi karibuni “tumaini ni hili kwamba leo, katika wakati ambao kila mtu anaonekana kutoa maoni juu ya kila kitu, hata bila kujali ukweli na mara nyingi hata kabla ya kufahamishwa, tunagundua tena na kurudi katika kukuza zaidi kanuni ya ukweli. Ni ukweli wa ukweli, yaani mabadiliko ya ukweli; ambayo hayasimami na hubadilika kila mara, kuelekea mema au mabaya, ili usiwe na hatari kwa jamii ya habari kugeuka kuwa jamii ya upotoshaji. Kwa kuhitimisha, Askofu Mkuu Caccia alisema kuhamasisha utamaduni wa amani na ulimwengu bora kunawezekana kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, ikiwa hii inaambatana na maadili yanayo chochewa na maono ya manufaa ya wote, maadili ya uhuru, wajibu na udugu, yenye uwezo wa kuhamasisha maendeleo fungamani ya watu kuhusiana na wengine na kwa kazi ya uumbaji wote.