WYD,Papa:Vijana kutoka mabara watapata furaha ya kukutana,Mungu,kaka&dada zao!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 30 Julai 2023 kumbukizi ya siku za Kimatafa:Urafiki na dhidi ya biashara haramu ya Binadamu, na mwito kwa Serikali ya Urussi kuhusiana na vita na ngano, vile vile alifikiria akifikiria siku ya vijana inayokuja ambapo alisema: “Ninawaomba mnisindikize kwa maombi yenu katika safari yangu ya kuelekea Ureno, ambayo nitaifanya kuanzia siku ya Jumatano ijayo, katika kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani. Vijana wengi, kutoka mabara yote, watapata furaha ya kukutana na Mungu, kaka na dada zao, wakiongozwa na Bikira Maria, ambaye baada ya Tangazo la Malaika “alisimama na kwenda kwa haraka” (Lk 1:39). Kwake yeye, nyota angavu ya safari ya Kikristo, anayeheshimiwa sana nchini Ureno, ninawakabidhi mahujaji wa (WYD)na vijana wote wa ulimwengu.” Akiwalekeza mahujaji na waamini kutoka Padre za dunia, miongoni mwake kulikuwapo na vijana Denis Amos Mwalongo na Lidia Mhoro wote wawili wanafunzi wa shahada ya Udaktari kutoka Tanzania ambao waliitembelea Radio Vatican.
Radio Vatican ilifanya mahojiano na wasomi hawa wawili, ambapo tunakuletea mahojiano maalum kabisa ambayo hayajachapishwa.
Mimi ninaitwa Denis Amos, Mwalongo. Ninatoka Tanzania na ni mwanafunzi wa degree ya (PhD) yaani udaktari katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela. Ninafanya kazi ya Tume ya Wizara ya Elimu Sayansi na Telnolojia. Nilikuwa nimekuja Italia kwa miezi mitatu katika Chuo Kikuu cha Cagliari, (Sardegna) ambacho nimekaa kwa ajili ya kufanya mapitio ya uzoefu wangu wa shule, lakini niliona sio vizuri kupita hapa Roma bila kuja hapa Vatican, ambapo imekuwa ndoto yangu sana katika maisha; sana sana kuweza kupata za Baba Mtakatifu. Na nimefurahi sana leo hii nimeweza kufika hapa na kuweza kupata baraka za Baba Mtakatifu, kwa hiyo nimefurahi lakini pia nimefurahi kuja hapa katika Radio ya Vatican, ambako kiukweli tumekuwa tunaisikiliza, lakini pia tumekuwa tunaifuatilia katika mitandao ya kijamii. Na ninaomba kuwashauri wakristo wote wakatoliki waweze kusikiliza hii Radio vipindi vyake. Lakini pia kufuatilia vipindi vyake kwa sababu ndivyo tunapata taarifa sahihi kuhusu kazi, pamoja na mambo yote yanayoendelea kuhusu Kanisa na Baba Mtakatifu.
Umeelezea juu ya suala la atomiki, je ungeweza kuelezea kidogo kuhusiana na hii?
Asante sana. Kwenye hii atomiki, mimi utafiti wangu sana sana, ninaangalia madini ya Urani (Uranium) ambayo yako kwenye madini ya Phosphate yanayotumika kutengeneza mbolea. Na hizi mbolea zinatumika kwenye mazao yetu, lakini hii Urani ina matatizo kwa sababu ina madhara ikiingia kwenye udongo, kwa hiyo kwa kuingia kwenye udogo inaweza kuchukuliwa na mmea, alafu mtu akala na akapata madhara. Kwa hiyo tunaangalia namna gani hasa mbolea yetu ya Minjingu pale ambako kuna madini mengi haya, tunawezaje kuyaondoa kutoka kwenye mbolea ili tuweze kupata mbolea ambayo ni safi kwenye mazingira, lakini pia isiweze kuathiri watu.
Je kwa upande wa suala hilo, wananchi, wakulima unawashauri nini?
Waendelee kutumia mbolea lakini pia sisi kama watafiti, kazi yetu ni kuhakikisha kuwa wanapata mbolea ambayo haina madhara kwenye udongo. Na imekuwa lengo la Tume ya Nguvu za Atomiki, kwa sababu ni Taasisi ya Serikali(Tanzania); lakini pia na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kuhakikisha kuwa tunatumia maarifa yetu kuweza kusaidia jamii ili isiweze kupata madhara na ndiyo maana tunafanya utafiti.
Chuo Kikuu hiki cha Nelson Mandela kiko upande gani wa Tanzania?
Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kiko mkoani Arusha karibu na Tengeru. Ni chuo ambacho kinatoa degree au masomo kuanzia degree ya uzamili, uzamivu yaani Masters na PHd (udaktari). Na ni chuo kizuri ambacho ni cha Sayansi, lakini pia kinafundisha masomo ya kibinadamu(humanities). Kwa hiyo tunawakaribisha wote ambao wanataka kusoma waweze kusoma.
Ndani ya Studio hizi kaka hayupo peke yake bali kuna hata dada
Tumsifu Yesu Kristo. Mimi ninaitwa Lidia Mhoro. Ni mzaliwa wa Songea, Tanzania lakini kwa sasa niko Morogoro katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine. Ni mhadhiri msaidizi ambako kwa sasa niko kwenye masomo ya shahada ya uzamili (PhD) tunasema. Niko hapa Italia kwa muda wa miezi mitatu. Nilikuwa kwenye kisiwa kimoja kinaitwa Sardegna. Nimekuja kutembelea kwa siku mbili hizi hapa Vatican. Lengo kuu kabisa lilikuwa ni kuja kuona sehemu ambayo chimbuko la ukatoliki lipo hapa ambako Baba Mtakatifu yupo hapa. Kwa hiyo kiukweli imekuwa furaha sana, kuwepo katika mazingira haya. Kiukweli imekuwa furaha kwangu, nadhani nikirudi Tanzania, nitakuwa na furaha zaidi ya kuwaelezea kwamba nimefika eneo ambalo chimbuko langu la dini ya ukatoliki liko hapa. Ninashukuru sana!
Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana aliwaomba ninyi waamini wote mliokuwapo kusali pamoja naye sala ya Malaika wa Bwana, mmuombee katika hija yake ya kwenda Ureno. Vijana wengi tayari wamekwisha kukusanyika kule. Ninyi ambao ni vijana mnawashauri nini wale ambao hasa hasa hawana fursa ya kuja huku, lakini wamebaki kule kule kwa mfano upande wa Tanzania?
Yaani Mimi ninachoweza kuwashauri vijana kwanza kabisa ni kijikita katika masuala ya kumjua Mungu. Baba Mtakatifu kwa kweli ana maono makubwa sana kwa vijana. Tuweze kumtafuta Mungu kwa namna yeyote. Tuweze kijitafuta sisi vijana kwamba tunaka nini katika maisha? Kwa hiyo ninawashauri vijana popote walipo duniani na Tanzania kwa ujumla waweze kumtafuta Mungu, waweze kuwa na bidii katika kumjua Mungu ili yote wanayofanya yaweze kuwa na baraka katika maisha yao.
Tukirudi kwa kaka yetu tena
Mimi kiukweli kwa kuwashauri vijana wenzangu ni kuwa tujikite kwenye ujumbe wa Baba Mtakatifu ambapo kwa mfano wa suleimani ambaye alipata uongozi akiwa kijana mdogo na baada ya kupata uongozi, Mungu akamwuuliza anataka kitu gani, akamwambia: 'Ninaomba unipe baraka, ili nipate kuwaongoza watu wangu kwa hekima.' Na Mungu alimpatia. Kwa hiyo sisi kama vijana na vijana wenzangu wote ambao wanasikiza saa hizi, tujikabidhi kwa Mungu na tumuombe Mungu, sisi kama vijana kwa sababu Mungu anatupenda; Je kwa nini? kwa sababu wana nguvu ya kuweza kumpinga shetani. Kwa hiyo sisi kama vijana basi tujitahidi kwa Mungu na tumuombe Mungu atupatie busara ili tuweze kumtegemea yeye katika maisha yetu yote.
Je mnalo jingine la mwisho?
Kwa upande wangu ninapenda kuwashauri wakristo, wakatoliki na wakristo wengine waweze kusikiliza Radio Vatican kwa sababu ni Radio ambayo inatoa taarifa sahihi, hata kama tutapata changamoto zozote zile, lakini ninaomba sana watu waweze kuisikiliza radio Vatican ili waweze kupata ujumbe ulio sahihi katika Kanisa.
Mungu awabariki katika safari na katika maisha yenu.
Amina!