Papa Francisko Ateuwa Maaskofu Wasaidizi, Jimbo kuu la Kinshasa, Nchini DRC!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Julai 2023 amemteuwa Mheshimiwa Sana Padre Edouard Tsimba Ngoma, C.I.C.M. pamoja na Mheshimiwa Sana Padre Edouard Isango Nkoyo kuwa Maaskofu wasaidizi wa Jimbo kuu la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo. Itakumbukwa kwamba Askofu msaidizi mteule Edouard Tsimba Ngoma, C.I.C.M. alizaliwa tarehe 11 Aprili 1957 huko Boma, nchini DRC. Baada ya masomo, malezi na majiundo ya kitawa, Mwezi Februari 1989 akawaweka nadhiri zake za daima huko Haiti na hatimaye, tarehe 13 Agosti 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Shirika la Moyo Safi wa Bikira Maria. Tangu wakati huo kama Padre amewahi kutekeleza utume wake kwenye Parokia kadhaa na mhamasishaji wa miito ya kitawa na kimisionari; Paroko-usu, mlezi wa wanovisi; Makamu wa Rais Kitaifa kwa Malezi ya Watawa nchini Haiti. Kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2005 alichaguliwa kuwa ni Mshauri wa Shirika. Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2011 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Moyo Safi wa Bikira Maria. Kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Wakuu wa Mashirika ya Missionari, SEDOC. Amewahi kuwa ni Gambera wa seminari kuu, Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Amewahi pia kuwa Makamu Askofu kwa ajili ya watawa Jimboni Liège, nchini Ubelgiji.
Itakumbukwa kwamba, Askofu Msaidizi mteule Edouard Isango Nkoyo alizaliwa tarehe 1 Aprili 1973 huko Kinshasa. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kipadre tarehe 4 Agosti 2002 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Kinshasa, nchini DRC. Tangu wakati huo, amewahi kuwa ni Mwalimu wa Taaluma, Seminari kuu ya Mtakatifu Andrea Kaggwa kati ya mwaka 2003 hadi mwaka 2009 na hatimaye kati ya mwaka 2017 hadi mwaka 2018. Baadaye alijiendeleza kwa masomo ya juu kwenye Chuo kikuu cha Falsafa cha Munich, Baviera. Tangu wakati huo amewahi kuwa Paroko-usu, wakili Paroko na baadaye akateuliwa kuwa ni Gambera wa Seminari kuu ya Mtakatifu Andrea Kaggwa. Tangu mwaka 2021 akateuliwa kuwa Katibu mkuu wa Jimbo Katioliki la Kinshasa na kuanzia mwaka 2022 akateuliwa kuwa ni Katibu mtendaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kanda ya Kinshasa.