Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023. Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023.   (Vatican Media)

Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee: Thamani na Umuhimu wa Wazee Duniani

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania na Rais wa WUCWO Kanda ya Afrika anauzungumzia umuhimu na jukumu la wazee katika maisha na jamii katika ujumla wake, huruma ya Mungu inajidhihirisha katika historia kupitia kwa wazee, "safari ya furaha ya upendo wa familia” Malezi ya familia ili ziwe ni mifano ya udugu na maeneo ya matumaini kwa wote, na kwamba, Wazee ni urithi ambao unahitaji kutunzwa. Wanawake wanahamaishwa.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Nairobi, Kenya.

Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa mwaka 2023 anagusia kuhusu: Bikira Maria akiwa amejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu akaondoka kwa haraka, Mkutano kati ya Bikira Maria na Elizabeti, Kati ya vijana na wazee; Iwe ni siku ya kukutana kwa furaha na kwa upya kati ya vijana wa kizazi kipya na vijana wa zamani, yaani wazee. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee kwa mwaka 2023 inaonesha ile furaha aliyokuwa nayo Bikira Maria aliyekuwa amejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu alipokutana na binadamu yake Elizabeti na kumwakia akisema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Lk 1:42. Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania na Rais wa WUCWO Kanda ya Afrika anauzungumzia umuhimu na jukumu la wazee katika maisha na jamii katika ujumla wake, huruma ya Mungu inajidhihirisha katika historia kupitia kwa wazee, "safari ya furaha ya upendo wa familia” na kwamba, Wazee ni urithi ambao unahitaji kutunzwa. “Wanawake Wakatoliki wajenzi stadi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu kwa amani ya Ulimwengu.” Tarehe 23 Julai 2023, Ulimwengu utaadhimisha siku ya Tatu ya Bibi, Babu na Wazee Duniani. Siku hii ilianzishwa rasmi mnamo mwaka 2021 na Baba Mtakatifu Francisko na inaendelea kuhamasishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha.  Sherehe hii ilizaliwa kutokana na umuhimu wa jukumu walilonalo wazee katika maisha yetu na katika jamii zetu. Uzee ni zawadi na kiungo kati ya vizazi na yenye kurithisha kwa vijana uzoefu wa maisha na imani.

Siku ya tatu ya Babu, Bibi na Wazee 2023
Siku ya tatu ya Babu, Bibi na Wazee 2023

Wazee ni: “amana na utajiri wa jamii”; wao ni: “watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii”; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana uzoefu na mang’amuzi ya maisha. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani inakuwa ni fursa ya kuboresha mahusiano kati ya kizazi kipya kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na Wazee. Tunapotafakari namna ya kurejesha maadili yetu ya kiafrika na utu wa kibinadamu, yapo mengi ya kujifunza kutoka kwa wazee. “Nikiikumbuka Imani uliyonayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi na katika mama yako Eunike, nami nasadiki nawe unayo” 2 TIMOTHEO 1:5. Napenda kuwasihi pia viongozi wenzangu waliochaguliwa kulitumikia Kanisa wasisahau hazina ya waliowakabidhi vijiti. Kauli mbiu ya mwaka huu inatoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Lk 1:50: "Huruma yake kwa wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi" ambayo inatualika kukumbuka kwamba huruma ya Mungu inajidhihirisha katika historia kupitia shuhuda zilizotolewa kutoka kizazi hadi kizazi, kutoka kwa babu/bibi hadi wajukuu.  Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwa kumtembelea binamu yake Elizabeti. Safari hii ya Bikira Maria inafungua macho ya waamini ili kuangalia historia ya wokovu, kwa wanawake hawa wawili, wanavyopokea na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao. Insikitisha kuona kuwa watoto wetu leo, hawafahamu binamu zao ambao wanaweza kuwashirikisha changamoto wanazopitia. Matokeo yake wanawashirikisha wapita njia ambao wanawarubuni na kuwapoteza. Tuwapeleke watoto wetu kwa bibi zao wawafahamu shangazi na binamu zao waweze kuwashirikisha changamoto zao katika ulimwengu mamboleo.

Wazee ni amana na utajiri wa jamii
Wazee ni amana na utajiri wa jamii

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuadhimisha Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa Ibada ya Misa Takatifu, anatoa wito kwa vijana watumie fursa hii, kuwatembelea na kuwasaidia wazee katika maisha yao. Na wazee nao, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno, wawakumbuke na kuwaombea vijana wa katika hija ya maisha ya kiroho kama sehemu ya ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika ulimwengu mamboleo. Itakumbukwa kwamba, moja ya maazimio ya WUCWO inahusu "safari ya furaha ya upendo wa familia." Napenda kuwaalika wanawake wakatoliki kote duniani, kujisadaka kwa kushikana mikono kuhimiza na kushiriki kwa ari mpya katika malezi ya familia ili familia zetu ziweze kuwa mifano ya udugu na maeneo ya matumaini kwa watu wote hasa wenye uhitaji na waliopo katika mazingira magumu/waliosukumizwa pembezoni. Wazee mara nyingi ni kundi lililopo katika mazingira magumu na wenye mahitaji katika jamii zetu. Wazee wengi wanashindwa kumudu gharama za matibabu kwa sababu hawana bima na watoto/wajukuu zao wamewasahau kabisa. Tuguswe kushiriki katika kuongeza tabasamu kwa wazee wetu kwa kuwakatia bima za matibabu ili kuwa na uhakika wa huduma bora za afya.

Bikira Maria awe ni mfano bora wa mafungamano ya kijamii
Bikira Maria awe ni mfano bora wa mafungamano ya kijamii

Nipende kuwaalika wanawake wote bila kujali dini ama itikadi zao kuchukua hatua zifuatazo: Kusoma na kusambaza andiko la kichungaji na sala vilivyotolewa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha tunaposhereheke siku ya Babu, Bibi na Wazee ili kufikisha ujumbe huu kwa kila rika. Hii inaweza kufanyika kwa kupost kwenye status na mitandao ya kijamii. Kusali rozari takatifu na sala maalum ya Mama Bikira Maria iliyoandaliwa kwa ajili siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka 2023. Kuandaa na kutuma/kupost nembo, maombi na majarida mbalimbali yanayokuza kuwajali wazee kwenye tovuti yako / mitandao ya kijamii / jarida. Kuandaa mpango thabiti utakaowahusisha Vijana na Wazee katika kusaidia, kusherehekea na kuitambua siku hii ya tatu ya Bibi, Babu na Wazee duniani tarehe 23 Julai 2023 katika familia, parokia, jimbo na hata mahali pa kazi. Wazee ni urithi ambao unahitaji kutunzwa. Tukipiga hatua moja kwa pamoja kwa wakati tunaweza kufanya tofauti kwao. Tusherehekee pamoja na wapendwa wetu vijana wa zamani. Pamoja nanyi katika sala na tafakari kuhusu hazina ya Wazee!

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania na Rais wa WUCWO Kanda ya Afrika.

Siku ya wazee Duniani
20 July 2023, 14:28