Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni: Wajibu Na Dhamana ya Vijana
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB., - Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanaanza kutimua vumbi huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Zikiwa zimebaki siku chache sana kabla ya kuadhimisha Siku ya Vijana Ulimwenguni, itakayofanyika katika Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2023; ni vyema kuanganza macho na akili zetu sisi kama vijana katika mambo kadhaa ambayo kijana wa leo anatakiwa kutambua na kutafakari, hasa katika maisha ya Ukristo ambayo yanaongozwa na upendo, unyenyekevu na kujitoa kwa wengine. Katika Siku ya Vijana Ulimwenguni mwaka 2000 katika Jimbo kuu la Roma, nchini Italia, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaambia vijana: “Vijana wapendwa wa karne hii inayoanza, kwa kusema NDIYO kwa Kristo, mnasema Ndiyo kwa kila mojawapo ya maadili yenu bora zaidi. Ninamwomba Kristo atawale mioyoni mwenu… usiogope kujitoa Kwake: Yeye atawaongoza kila mmoja wenu na kuwapa nguvu za kumfuata Yeye kila siku, katika kila hali”. Wapendwa vijana ni katika kujitoa na kusema ndiyo kwa Kristo Yesu ndipo tunapata nguvu ya kusimama imara katika Imani yetu bila kuyumbishwa na mambo ya kiulimwengu.
Hili ni neno ambalo linazidi kutupa dira na mwongozo sisi kama vijana katika maisha yetu hasa pale tunapokumbana na changamoto mbalimbali za ulimwengu huu ambazo zinatufanya kuwa mbali zaidi na wito wetu kama wabatizwa wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika Maisha yetu. Hii ni kwasababu Kanisa linakuhitaji wewe kama kijana katika kumshuhudia kwa ari, ubunifu na furaha inayojidhirisha ndani mwenu. Ndio maana Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Vijana Ulimwenguni kule Copa Cabana, nchini Brazil mwaka 2013 aliwaasa vijana na kuwaambia: “Nendeni mkahudumu bila woga”. Mara nyingi sana kijana wa leo anakumbwa na mambo mengi, anajiingiza katika makundi na mitandao mbalimbali ambayo yanamfanya asitumie muda wake mwingi katika kusali, kusoma, kutafari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha Tukumbuke kuwa hata Yesu alikuwa kijana na aliweza kuyatoa Maisha yake kwa ajili yetu sisi katika umri wa miaka 33 tu. Hata sisi vijana tunaitwa kujitoa Maisha yetu kwa wengine, tusisubiri kuwa na umri mkubwa ndio tuanze kusali na kuomba neema ya Mungu. Wakati ndio sasa kama anavyoatualika Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wa kitume wa “Christus Vivit” yaani “Kristo anaishi”, kuyatoa Maisha yetu kama vijana kwa ajili ya wengine: “ni muhimu kutambua kuwa Yesu alikuwa kijana. Aliyatoa Maisha yake… (ChrV 23). Ewe kijana unasubiri nini kuyakabidhi Maisha yako kwa Kristo na katika yale yampendezayo Mungu? Wakati ndio sasa wa kutambua wajibu wako na kuanza safari mpya iliyojaa upendo, unyenyekevu na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Bwana wetu Yesu Kristo.
Vijana tunaitwa kuwa chachu katika ulimwengu mamboleo (rej Lk 13,21), lakini hatuwezi kuwa chachu kama kwanza hatutakuwa tumejazwa na upendo wa Kristo. Mtakatifu Yohane Bosco ambaye ni Baba, Mwalimu na Rafiki wa Vijana, aliamini kuwa ndani ya kila kijana kuna kitu kizuri cha kubadilisha ulimwengu huu. Kumbe ni lazima turudi katika Maisha yanayompendeza Mungu, kushiriki Ibada ya Misa Takatifu, kusali kila siku, kusoma Maandiko Matakatifu, Sakramenti hasa ile ya toba, kufanya matendo ya Huruma, kushiriki katika vikundi mbalimbali ndani ya Kanisa na kuomba msaada wa Mama yetu Bikira Maria. Ni hapa ndipo tunapopata nguvu ya furaha na uwepo wa Mungu katika ulimwengu huu, tunapata kukutana na Kristo Yesu ambaye ni mwanga katika Maisha ya kila mmoja wetu na kupata ile neema ya Roho Mtakatifu ya kusimama daima katika ukweli. Tukumbuke maneno haya ya Biblia ambayo yanasema “Kijana, nasema Inuka! (Lk 7,14 na ChrV 20) na uamke! Nimekufanya kuwa shahidi wa mambo yote uliyoyaona (cfr Mdo 26,16). Hivi ndivyo kijana wa leo anaitwa kuamka na kuanza kujitoa ili kuwa shahidi wa mambo yote ambayo Mwenyezi Mungu ametenda katika maisha yake. Kama Maria na pamoja nae, tumeitwa kama vijana kuwa nashahidi wa ile furaha na upendo wake.
Bikira Maria alikubali mpango wa Mungu (rej Lk 1,38) na aliamka kwa haraka kwenda kumtembelea binamu yake Elizabeti (rej Lk 1,39). Ni lazima kuwa daima tayari kukubali mpango wa Mungu katika maisha yetu, kunyanyuka na kwenda kuwasaidia wengine katika mahitaji yao mbalimbali. Kijana mpendwa, ningependa kumalizia na maneno haya yaliyoko mwishoni mwa ule Waraka wa Kitume wa Papa Francisko wa “Christus Vivit” yaani “Kristu anaishi”. Maneno haya yatupatie moyo wa kuendelea mbele kwa kutokuyumbishwa na malimwengu. Ewe kijana “Endelea kukaza mwendo, kuvutiwa na ule uso wa Kristo, tunao upenda sana, tunao uabudu katika Ekaristi Takatifu na tunao ukubali katika nyuso za ndugu zetu wanaoteseka. Roho Mtakatifu awaimarishe katika safari hii. Kanisa linahitaji kasi yenu, mawazo yenu, imani yenu…” (ChrV 299). Mwenyezi Mungu na awabariki sana.