Tafuta

Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa umefunguliwa tarehe 31 Mei 2023 na utahitimishwa tarehe 6 Juni 2023. Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa umefunguliwa tarehe 31 Mei 2023 na utahitimishwa tarehe 6 Juni 2023. 

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa 31 Mei-6 Juni 2023

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa amezungumzia kuhusu: “hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. 2Kor 4:7. Wakurugenzi wamefafanuliwa kuhusu Katiba ya Kitume ya "Hubirini Injili, Umuhimu wa umoja na mshikamano katika utume na ushuhuda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, umefunguliwa tarehe 31 Mei 2023 na utahitimishwa tarehe 6 Juni 2023. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 31 Mei ya Kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea binamu yake Elizabeth. Bikira Maria alitangazwa kuwa ni Mwenyeheri kwa sababu alisadiki: kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana! Rej. Lk 1:45. Huu ni ushuhuda wa ujasiri wa kiimani na fadhila. Ni mkutano kati ya Agano la Kale na Agano Jipya; huruma na upendo wa Mungu unaoganga, unaookoa na kuponya. Huu ni ushuhuda wa Injili ya matumaini, kwa watu wa Agano la Kale na kama ilivyo kwa watu wa ulimwengu mamboleo! Huu mwendelezo wa utenzi wa sifa, shukrani na furaha ya ujio wa Masiha, Mkombozi wa Ulimwengu unaotambuliwa na Yohane Mbatizaji. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa amezungumzia kuhusu: “hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. 2Kor 4:7. Hii ni imani thabiti iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, lakini si sababu kwa Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuanza kulegeza kamba na kujikuta wakielemewa na uvivu na ukiritimba kwa kukosa kipaji cha ubunifu.

Mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa Kwa mwaka 2023
Mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa Kwa mwaka 2023

Wakurugenzi wa PMS wanapaswa kutenda kwa uaminifu kazi waliyokabidhiwa na sifa zimwendee Mwenyezi Mungu. Kumbe, wao wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, hata katika hali ya ukimya, lakini ikashuhudiwa na majirani wanaowazunguka. Kazi ya kimisionari inafumbatwa katika maisha ya sala, inayowawezesha kukutana na Kristo Yesu katika Neno na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko kwa Wakurugenzi wa PMS kumruhusu Roho Mtakatifu “awaundie” Kristo Yesu ndani mwao”, ili kutambua uwepo wake endelevu katika maisha na utume wao. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, anasema, Utenzi wa Bikira Maria “Magnificat” ni sala inayotoa kipaumbele cha pekee kwa Mwenyezi Mungu aliyemtendea makuu, chemchemi ya furaha yake na utimilifu wa ahadi ya Agano la Kale. Kumbe, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni kwa ajili ya watu wake wote na furaha ya kweli inajionesha pale, furaha hii inaposhirikishwa kwa wengine, kumbe, matendo makuu ya Mungu yang’are katika matukio mbalimbali ya maisha na utume wa Kanisa.

Uinjilishaji unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko
Uinjilishaji unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko

Kwa upande wake wake, Askofu mkuu Emilio Nappa, Katibu Mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa amegusia kuhusu Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katika hii ya Kitume inakazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili, dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, ameridhia Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba itaanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989. Askofu mkuu Emilio Nappa, amekazia uinjilishaji wa kina na dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa njia ya ushirikiano unaojenga mtandao wa kimisionari.

Mashirika ya Kipapa

 

02 June 2023, 14:56